Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio linalozitaka
nchi kuchukua hatua ya kuzuia usajili na usafirishaji wa wapiganaji wa
kigeni nchini Iraq na Syria.
Azimio hilo lililoidhinishwa kwa kauli moja na baraza hilo lenye nchi
wanachama 15 linayahitaji mataifa yote kuidhinisha sheria ambazo
zitafanya iwe ni uhalifu kwa raia wake kujiunga na makundi yenye itikadi
kali kama vile Dola la Kiislamu – IS na Al-Nusra Front. Rais Barack
Obama wa Marekani aliyeongoza kikao hicho maalum, amezitaja hatua hizo
kuwa ni za "kihistoria", ikiwa ni mara ya sita pekee katika historia ya
Umoja wa Mataifa ambapo Baraza hilo limewahi kukutana katika kiwango cha
viongozi wakuu wa nchi:
Hata hivyo, Obama alionya kuwa "maazimio hayo pekee hayatoshi" na akatoa
wito kwa serikali kushirikiana katika kuzuia usafirishaji wa wapiganaji
wa kigeni nchini Iraq na Syria "siyo kwa siku chache zijazo, bali kwa
miaka mingi ijayo".
Azimio hilo lililotayarishwa na Marekani linazitaka serikali
kuchukua hatua dhidi ya raia wanaosafiri au wanaopanga kusafiri kwenda
nchi nyingine ili kujiunga na makundi ya itikadi kali na pia linapiga
marufuku ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya usajili wa wapiganaji.
Takribani wapiganaji wa kigeni 15,000 kutoka nchi 80 wamejiunga na
wapiganaji wa siasa kali nchini Syria, kwa mujibu wa takwimu za kijasusi
za Marekani. Wataalamu wanasema kuwa idadi kubwa ya wapiganaji wa
kigeni walioko sasa nchini Syria na Iraq wanatokea Mashariki ya Kati na
nchi za Kiarabu, huku Saudi Arabia, Tunisia na Morocco zikiongoza kwenye
orodha hiyo.
Mateka wa Kifaransa achinjwa Algeria
Azimio hili la Baraza la Usalama limesadifiana kupitishwa siku ile ile
ambapo wanamgambo wenye itikadi kali nchini Algeria wametoa vidio
inayoonesha wakimchinja mateka wa Kifaransa aiyekamatwa Jumapili
iliyopita, Herve Gourdel ili kuiadhibu Ufaransa kwa
kujiunga katika mashambulizi ya anga dhidi ya kundi linalojiita Dola la
Kiislamu, IS, nchini Iraq.
Akionyesha kuunga mkono azimio hilo dhidi ya ugaidi, Rais Francois
Hollande wa Ufaransa alisema kuwa tukio hilo ni ishara kuwa ugaidi
unastahili kukabiliwa kwa dharura na akatoa wito kwa nchi wanachama wa
Umoja wa Mataifa kuungana katika vita hivyo. Hollande alisema tukio hilo
la kinyama haliwezi kuzuia azimio la kuuangamiza ugaidi, na kuwa
Ufaransa itaendeleza mashambulizi yake kwa muda usiojulikana.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 maoni:
Post a Comment