WAKANDARASI UMEME WASIOWAJIBIKA KUNYANG’ANYWA TENDA

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Meza Kuu-Katikati), akizungumza na wawakilishi wa Kampuni mbalimbali zinazohusika kusambaza umeme vijijini kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhusu utekelezaji wa miradi husika.
Wawakilishi wa Kampuni mbalimbali zinazohusika kusambaza umeme vijijini kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi pamoja na baadhi ya Mameneja wa Tanesco wa Mikoa husika, wakitoa mrejesho kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Meza Kuu – Katikati), kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Miradi husika. Kulia kwa Waziri Muhongo ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga na kushoto kwa Waziri ni Kamishna Msaidizi wa Nishati sehemu ya Umeme, Mhandisi Innocent Luoga.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Dk. Lutengano Mwakahesya akizungumza katika mkutano baina ya Waziri wa Nishati na Madini na kampuni zinazosambaza umeme vijijini kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Mwakahesya aliahidi kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.

Na Veronica Simba

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka Kampuni zilizopewa tenda kusambaza umeme vijijini kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa vinginevyo watanyang’anywa tenda hizo.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma katika Mkutano baina yake na wawakilishi wa Kampuni husika kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi pamoja na Mameneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wa mikoa hiyo na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Profesa Muhongo aliitisha Mkutano huo kwa lengo la kupokea taarifa kutoka kwa Watendaji wa Kampuni hizo kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kabla ya kutembelea miradi hiyo kwa mara nyingine kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara kujiridhisha na  maendeleo yake.

Akizungumza katika Mkutano huo mara baada ya kupokea taarifa za utekelezaji kutoka pande zote, Waziri Muhongo alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dk. Lutengano Mwakahesya kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafuatiliwa kwa ukaribu na kusitisha tenda mara moja kwa kampuni zitakazobainika kutotimiza makubaliano ya mkataba walioingia.

“Fuateni utaratibu wa kisheria kwa kutumia vifungu vilivyomo kwenye mkataba vinavyoelekeza kuchukua hatua stahiki kwa kampuni isiyotekeleza wajibu wake ipasavyo,” alisisitiza Muhongo.

Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha inatimiza ahadi yake ya kuwapatia Watanzania umeme ili wajikwamue katika lindi la umaskini kwa kukuza kipato chao na cha Taifa kwa ujumla hali itakayofanya Tanzania kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

“Yeyote atakayetukwamisha au kuturudisha nyuma katika kufikia malengo yetu ya kuwaondolea Watanzania umaskini, tutapambana naye na kamwe hatutampa nafasi,” alisema Muhongo.

Vilevile, aliwataka Mameneja na watendaji wengine wa Tanesco kuachana na utamaduni wa kukaa ofisini na kusubiri ripoti za utekelezaji wa miradi badala yake watembelee miradi wanayosimamia na kuhakikisha kazi inafanyika kama inavyotakiwa.

Aidha, Waziri Muhongo aliwataka wakandarasi waliopewa tenda husika kuwa wakweli na waaminifu na kuachana na tamaa hususan wanapopewa kazi ambayo wanajua hawana uwezo wa kuitekeleza ipasavyo ili kuwapa nafasi wengine wenye uwezo huo.

Alisema ni bora kwa Mkandarasi kukubali kazi anayoimudu ili aifanye kwa ubora unaotakiwa na hivyo kujiongezea sifa za kupewa kazi nyingine kuliko kuomba kazi kubwa asiyoweza kuitekeleza kikamilifu na matokeo yake anaharibu na kupoteza sifa ya kufikiriwa kupewa kazi nyingine.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga aliwataka wote wanaohusika na utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo ya kusambaza umeme vijijini kutimiza wajibu wao   kwa vitendo.

“Achaneni na maneno maneno, mimi nataka kuona vitendo, nataka kuona matokeo,” alisisitiza na kuongeza kwamba hakuna sababu ya Wakandarasi kusuasua katika utekelezaji wa miradi hiyo kwani walioomba wenyewe wakijinadi kuwa wanaweza.

Naye Kamishna Msaidizi wa Nishati Sehemu ya Umeme, Mhandisi Innocent Luoga aliwataka Wakandarasi hao kujituma na kufanya kazi inavyostahili pasipo kusubiri kufuatwa-fuatwa na kuhimizwa kwa suala ambalo ni wajibu wao.

Wakichangia mawazo katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Edmund Mkwawa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo, Dk. Mwakahesya waliahidi kufanya kazi bega kwa bega na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ili kuhakikisha Watanzania hususan walioko vijijini wanapatiwa nishati ya umeme kama Serikali ilivyodhamiria na kuahidi.


MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUTUMIA REDIO JAMII KUELIMISHA UMMA

DSC_0009
Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Redio Sengerema mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye, akiutambulisha ujumbe wa wageni kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini kwa Wenyeviti wa bodi na mameneja wa redio za jamii nchini waliohudhuria warsha ya siku tano ya kuwajengea uwezo katika kuboresha masoko kwenye vituo vyao iliyofadhiliwa na shirika la maendeleo la Sweden (SIDA) na kuratibiwa na UNESCO.

Na Mwandishi Wetu, Sengerema
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kupitia Mradi wa kuimarisha Demokrasia na Amani (DEP) itaanza kutoa elimu inayohusu sheria ya vyama vya siasa na sheria ya gharama za uchaguzi kupitia redio za jamii ili kuwawezesha wananchi kutambua wajibu wao katika kulinda amani ya taifa kuelekea katika uchaguzi na wakati wa uchaguzi.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mradi wa kuimarisha Demokrasia na Amani (DEP) kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini, Beatrice Stephano wakati akizungumza na mameneja wa redio hizo katika warsha yao ya siku 5 iliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Sengerema.
Beatrice alikuwa akizungumzia mradi anaousimamia ambao umedhaminiwa na UNDP kupitia UNESCO kwa ajili ya kuelimisha umma wa watanzania kupitia redio za jamii katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi 2015.
Alisema uamuzi wa kutumia redio za jamii unatokana na redio hizo kuwafikia wananchi wengi zaidi, hali ambayo wadau katika masuala ya demokrasia wameona kwamba inaweza kutumika kuboresha zaidi uelewa wananchi.
DSC_0013
Meza kuu: Kutoka kushoto ni Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa mkoani Mwanza, Bw. Isaya Makoko, Mratibu wa Mradi wa kuimarisha Demokrasia na Amani (DEP) kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini, Bi. Beatrice Stephano, Mwenyekiti wa Warsha hiyo kutoka Orkonerei Radio Service Simanjiro Manyara, Bw.Baraka Ole Maika (katikati), Afisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph (wa pili kulia) pamoja na Afisa Mfawidhi Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Bw. Ludovick Ringia (kulia).
Uelewa huo upo katika sheria za uchaguzi, gharama na kuona wajibu wao wa kumsaidia Msajili wa Vyama vya Siasa kukabiliana na mazingira hatarishi ya amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Alisema ni kazi ya Ofisi Msajili wa Vyama vya Siasa kusimamia sheria ya vyama namba tano ya mwaka 1992 ya kusajili vyama na kuviangalia na ile ya namba sita ya mnwaka 2010 ambayo inagusia gharama za uchaguzi.
Mratibu huiyo amesema kwamba timu kutoka Ofisi ya Msajili itafika kwenye redio hizo za jamii na kuzungumza na wananchi kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wao katika siasa na kuimariuka kwa demokrasia.
Aidha elimu hiyo inatarajiwa kuwasaidia wananchi kutambua kwamba wana wajibu katika kuhakikisha kwamba menejimenti za uchaguzi zinawajibika pamoja na muuingiliano wake ili kuwa na michakato salama ya cuhaguzi na uchaguzi wenyewe.
DSC_0081
Mratibu wa Mradi wa kuimarisha Demokrasia na Amani (DEP) kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini, Bi. Beatrice Stephano (wa pili kushoto) akizungumza na mameneja wa redio za jamii nchini wanaohudhuria warsha ya siku tano inayofanyika kwenye kituo cha Habari na Mawasiliano cha Sengerema Telecentre mkoani Mwanza kuhusiana na ofisi yake kufanya kazi kwa pamoja na redio za jamii nchini katika kutoa elimu kwa umma.
Naye Afisa mfawidhi ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa mkoani Mwanza, Ludovick Ringia akizungumzia sheria mbili za vyama vya siasa alisema kwamba ni wajibu wao kuwaeleza wananchi kuhusu maadili na kanuni katika sheria zinazogusa ukuzaji wa amani katika duru za siasa na demokrasia.
Alisema mradi huo wa kuelimisha wananchi ambao unafanyika kwa udhamini wa Unesco kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ni moja ya njia za kufanikisha amani katika kipindi chote kuanzia uchaguzi wa mwisho hadi mwingine.
Alisema wanatumia redio za jamii kwa kuwa redio za kibiashara zimekuwa kikwazo hasa bajeti inapouma kidogo.
Alisema mradi huo ambao unafanyika kwa mwaka mmoja ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kuliwezesha taifa kuendelea kuwa na utulivu.
DSC_0073
fisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Bw. Al Amin Yusuph (wa pili kulia), akielezea uwezo wa redio za jamii zinavyoweza kufikia jamii kubwa zaidi nchini wakati ujumbe kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ulipofanya mazungumzo na Wenyeviti wa Bodi na Mameneja wa redio za jamii nchini waliohudhuria warsha ya siku tano iliyofadhiliwa na shirika maendeleo la Sweden (SIDA) na kuratibiwa na UNESCO iliyofanyika kwenye kituo cha habari na mawasiliano cha Redio Sengerema mkoani Mwanza.
Wenyeviti wa bodi na mameneja hao katika warsha hiyo walielemishwa uboreshaji wa masoko na umuhimu wa redio za jamii juu ya matumizi ya Tehama kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi na kushirikisha zaidi wananchi.
Aidha Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa UNESCO, Al Amin Yusuph akizungumzia mafunzo hayo alisema kwamba mradi huo umekuja wakati muafaka ili kutoa elimu kwa umma, kwani kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa takribani asilimia 70 ya wananchi wanaoishi vijijini wanasikiliza redio huku asilimia 5 tu ndio wanaangalia runinga.
DSC_0119
Afisa Mfawidhi Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Bw. Ludovick Ringia (kulia) akielezea ufanyaji kazi wa sheria mbili za vyama vya siasa kwa wenyeviti wa bodi na mameneja wa redio za jamii nchini wakati wa warsha ya siku tano iliyofadhiliwa na SIDA na kuratibu na  UNESCO ambayo imefanyika kwenye kituo cha Redio Sengerema mkoani Mwanza.
DSC_0034
Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa mkoani Mwanza, Bw. Isaya Makoko akiwasilimia wenyeviti wa bodi na mameneja wa redio za jamii nchini (hawapo pichani).
DSC_0135
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo akihoji swali kwa ujumbe uliotoka kwenye ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini.
DSC_0126
Pichani juu na chini ni baadhi ya wenyeviti wa bodi na mameneja wa redio za jamii nchini waliohudhuria warsha ya siku tano iliyomalizika mwishoni mwa juma kwenye kituo cha Redio Sengerema mkoani Mwanza kwa ufadhili wa SIDA na uratibu wa UNESCO.
DSC_0085
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment