Matukio
ya mauaji ya watu wasio na hatia, yameendelea kuuandama Mkoa wa Geita,
kufuatia watu watatu kuuawa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa mkuki huku
mmoja akijeruhiwa baada ya mtu mmoja anayesadikiwa ni mgonjwa wa akili
kutekeleza unyama wake.
Tukio
hilo lililotokea jana asubuhi katika kijiji cha Nyamilyango wilayani
Geita, na aliyejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita
ni Mathayo Sindamsanga, na hali yake imeelezwa ni mbaya.
Mganga
Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Adam Sijaona, alithitibisha kupokea
miili mitatu iliyohifadhiwa hospitalini hapo pamoja na majeruhi mmoja.
Dk. Sijaona aliwataja waliouawa kuwa ni Pindo Makono, Ndakazi Bertha Masabile na Jacob Bukulu, ambao ni wakazi wa kijiji hicho.
Hata hivyo, mtu huyo aliyesababisha mauaji hayo, alikamatwa na wananchi wenye hasira na kisha kumfikisha kituo cha polisi.
Dk. Sijaona alisema marehemu hao walifariki dunia kutokana na kuvuja
damu nyingi mwilini kufuatia muuaji kutumia panga na kuwacharanga na
kisha mkuki kuwatoboa miili.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa Kata ya Bugulula, Elisha Lupuga,
alisema lililotokea juzi saa 1:00 jioni katika kitongoji cha Misheni
katika kijiji cha Nyamilyango baada ya mtuhumiwa, Rashid Ramadhani,
mkazi wa kijiji hicho kutumia mkuki na panga kuwaua watu hao.
“Dhamira yake mpaka sasa haijafahamika ilikuwa nini, lakini amekuwa na
tabia ya kuvuta bangi na kwa muda mrefu, hivyo tunahisi amevurugukiwa
akili yake,” alisema Lupuga.
Hata hivyo, Lupuga alisema baadhi ya waliouawa walikuwa na mahusiano na
mtuhumiwa, lakini hakufafanua ni mahusiano ya namna gani waliyokuwa
nayo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha kutokea
tukio hilo na kwamba mtuhumiwa anashikiliwa katika kituo cha polisi
akisubiri hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.
Tukio hilo limeibua upya simanzi na vilio kwa wananchi wa mkoa huo ambao
mara kwa mara wamekuwa wakikumbwa na matukio ya mauaji ya aina
mbalimbali.
Hilo ni tukio la pili ndani ya wiki moja baada ya usiku wa kuamkia
Septemba 7, mwaka huu, watoto wanne wa familia moja kuuawa kufuatia
nyumba yao kuteketezwa na moto katika kitongoji cha Elimu kata ya
Kiangalala wilayani Geita.
Watoto walioteketea na moto huo ni Reginald Robert (9) mwanafunzi wa
darasa la nne na Sofia (6) wa Shule ya Msingi Ukombozi na Remijius (4)
wa chekechea pamoja na Scolastika (15) aliyekuwa akisoma shule ya
sekondari Mwatulole.
Katika tukio hilo, baba wa familia, Robert Reginald (49), mkewe Angelina
Reginald na watoto Robert mwenye umri wa miaka miwili na miezi mitatu
na Yohana (1), walinusurika katika janga hilo.
0 maoni:
Post a Comment