MICHEZO
DAR ES SALAAM: JAIZMELALEO
MRATIBU WA UHURU MARATHON 2014, INNOCENT MELLECK, AKIZUNGUMZA JAMBO KATIKA UZUNDUZI HUO KUSHOTO KWAKE NI MENEJA MASOKO Bi. CONSOLATA ADAM NA MJUMBE WA RT, TULLO CHAMBO
Mbio za Uhuru Marathon 2014 zimezinduliwa, jijini Dar es Salaam, katika hafla fupi iliyofanyika katika hotel ya Kebby, ikishuhudiwa udhamini mnono kutoka TBL kupitia kinywaji chake cha Grand Malt.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mratibu wa Uhuru Marathon Innocent Melleck alisema mwaka huu hakutakuwa na mbio za kilometa 42 kutokana na kukosekana kwa wanariadha wenye ushindani wa mbio hizo, hali inayofanya zawadi ziende kwa wageni ambao wengi wao hutoka mataifa ya Kenya na Ethiopia.
Pia Innocent aliongeza kusema mbio za kilometa 21 zitaleta ushindani na kwamba zitaanza kuwaandaa kwa ajili ya mbio ndefu katika siku za baadaye.
“Zawadi kwa mshindi wa kwanza ni shilingi milioni 2.5 za kitanzania ambapo hatutakuwa na full marathon ambayo ni kilometa 42 bali tutakuwa na kilometa 21 (half) kwa ajili ya kuwaandaa wanariadha wetu kwa mbio ndefu hapo baadaye, kwani kwa sasa tuna uhaba wa wanariadha wa mbio hizo hivyo zawadi nyingi huchukuliwa na mataifa kama Kenya na Ethiopia” aliongeza Innocent.
Mbali na mbio za kilometa 21, Uhuru Marathon mwaka huu itakuwa na mbio za baiskeli kwa kilometa 21 ili kuongeza ladha zaidi kuelekea kusheherekea miaka 53 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).
Kwa upande wake Meneja wa Kinywaji cha Grand Malt Bi. Consolata Adam alisema wametoa udhamini mkubwa mwaka huu kutokana na mafanikio waliyoyapata mwaka uliopita kwani walitoa kiasi cha shilingi milioni 20 na sasa wametoa kiasi cha shilingi milioni 35.
“Tunakabidhi hundi hii ya shilingi milioni 35 kwa waratibu wa mashindano haya ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za taifa katika kukuza riadha nchini, kwani mwaka uliopita tulitoa kiasi cha shilingi milioni 20” alisema Bi. Consolata.
Nacho Chama cha Riadha nchini (RT) kupitia mjumbe wake Tullo Chambo kilisema Uhuru Marathon imeongeza chachu kwa nchi nzima na uaminifu ndio ambao umesababisha hata wadhamini wakaongeza mkono wao katika mbio hizo na kutaka waandaji wengine kuiga mfano wa mbio hizo zinazotarajiwa kutimua vumbi Desemba 7 mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya RT nawapongeza waratibu wa mbio hizi kwa kuandaa kitu ambacho kimeonesha mrejesho katika jamii kwani natambua kwamba hii siyo kazi ndogo kama wengine wanavyodhani, pia nawapongeza TBL kwa kuwa mstari wa mbele katika kusapoti mchezo wa riadha kikubwa Mratibu aboreshe zaidi mbio hizi ila mwanzo ni mzuri,” alisema Tullo.
Kauli Mbiu mwaka huu ni “Uhuru wetu, Amani yetu, Tuitunze”.
MENEJA MASOKO WA TBL, Bi. CONSOLATA ADAM AKIMKABIDHI HUNDI YA SHILINGI MILIONI 35 MRATIBU WA UHURU MARATHON 2014, INNOCENT MELLECK.
0 maoni:
Post a Comment