TUME iliyoundwa na Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, John Mongela kufanya uhakiki wa wanafunzi hewa katika
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imebaini kuwepo kwa wanafunzi hewa 7,728.
Wanafunzi hao
waliisababishia serikali hasara ya Sh milioni 177. Wamebainika baada ya
kufanyika uhakiki wa awamu ya pili.
Akiwasilisha taarifa hiyo
jana kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Waryoba Sanya, alisema tume yake ilitumia muda wa siku 28 kufanya uhakiki wake
kwa kutumia hadidu za rejea mbili zilizochunguza na kubaini idadi halisi na
isiyo halisi ya walimu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika
halmashauri ya jiji la Mwanza.
Alisema tume yake ilitumia
takwimu zilizotumika hadi Desemba mwaka 2015 za kuwaletea wanafunzi fedha za
elimu bila malipo, ambapo ilibaini kuwepo wanafunzi 102, 065, ambapo kati yao
75,002 walikuwa wanapokea fedha za elimu bila malipo kutoka serikalini.
Alisema katika kufanya
uhakiki huo, tume ilitembelea shule 110 na kubaini wanafunzi 27,063 ndio
wanaostahili kupelekewa fedha za elimu bila malipo.
Aidha alisema tume ilibaini
kuwa walimu 5,385 ndio waliokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi na walimu 32
hawakuwepo kwenye vituo vya kazi kwa sababu mbalimbali na kuongeza kuwa kiasi
cha Sh bilioni 1.9 kilikuwa kimetumika kwa ajili ya kulipia mpango wa elimu
bila malipo kwa shule za msingi na sekondari kwa halmashauri ya jiji la Mwanza
kuanzia Desemba 2015 hadi Agosti mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa, Mongela
alisema aliamua kuunda Tume hiyo ili kuondoa mkanganyiko uliokuwepo kati ya
uongozi wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya na Taifa na Mkurugenzi wa Jiji la
Mwanza, Kiomoni Kibamba, ambapo CWT ilipinga taarifa ya walimu na watumishi
hewa iliyotolewa na uongozi wa jiji hilo.
Katika uhakiki wa awali,
Kibamba alibaini kuwepo kwa wanafunzi hewa 13,000 na walimu hewa 13,000.
0 maoni:
Post a Comment