Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 05 Machi, 2017 amemaliza ziara yake ya
kikazi ya siku 4 katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Kabla ya kuondoka Mjini Mtwara na kurejea
Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika
Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Mtwara na Lindi kwa nguvu kubwa
kwa manufaa ya wananchi.
Alisema Serikali imedhamiria kutilia mkazo
juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa
miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri
wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na
kuboresha maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli aliwapongeza viongozi na
wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa mafanikio yaliyopatikana katika soko la korosho
lililopita na ameagiza wale wote waliohusika kufuja fedha za wakulima
wachukuliwe hatua.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli alisema Tanzania
itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake mzuri na nchi jirani ya Msumbiji na
ametaka suala la wahamiaji haramu wanaoondolewa nchini humo wakiwemo Watanzania
lisikuzwe huku akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuwatetea watu wanaoishi
katika nchi nyingine bila kufuata sheria.
Kuhusu Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu,
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Mtwara kubadilika kwani juhudi za
Serikali kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa
hawana elimu.
“Nimeambiwa hapa watu wanapenda sana disco na
ngoma, watoto badala ya kusoma wanacheza disco, hapo tunakwenda pabaya” alisisitiza Mhe.
Rais Magufuli.
Mkutano wa Mhe. Rais Magufuli Mjini Mtwara
ulidhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter
Muhongo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, Waziri
wa Fedha na Mipango Dr. Philip Mpango, Wabunge na viongozi wa taasisi.
Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Hatimaye gazeti la MAWIO lililofutwa na
serikali ya Tanzania na kuacha
kuchapishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, limerejea mtaani kwa uamuzi wa Mahakama
Kuu.
Serikali ililifuta gazeti hilo na kulizuia
kuchapishwa kwa njia yoyote ile Januari 15, mwaka jana- 2016.
Uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Jumanne ,
umetupilia mbali amri ya serikali ya “kuliua na kulizika kabisa” gazeti hilo
lililokuwa likitoka kila wiki – Siku ya Alhamisi.
Mahakaka Kuu ilisema kuwa amri ya serikali
kuliua MAWIO haikuwa sahihi, hivyo “gazeti hilo lilionewa.”
Jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji
Sakieti Kihiyo, limesema gazeti la MAWIO halikupewa nafasi ya kujitetea kabla
ya hatua ya serikali ya kulifuta kutoka orodha ya msajili wa magazeti nchini.
Msajili wa magazeti nchini ni Idara ya Habari
Tanzania (MAELEZO).
Jaji Ignas Kitusi ndiye alisoma uamuzi wa
Mahakama kuu – kwa niaba ya jopo siku ya Jumanne, wiki iliyopita (Februari 28).
Jaji mwingine aliyekuwa kwenye jopo hilo, ni Jaji Ama-Isario Munisi.
Serikali ililifuta gazeti la MAWIO tarehe 15
Januari 2016 baada ya kudaiwa kuandika ilichoita habari na makala za
“kichochezi.”
Utawala wa Kampuni ya Victoria Media Services
Limited, wachapishaji wa gazeti la MAWIO, uliamua kufungua kesi mahakamani. Hii
ni kesi Na. 15 ya mwaka 2016.
Wakili wa MAWIO, Dk. Rugemeleza Nshalla,
amesema kuwa hatua ya serikali iliegemea falsafa ya “…Nyonga kwanza na sikiliza
baadaye.”
Dk. Nshalla amesema katika mazingira yoyote
yale, sharti walalamikiwa wapate nafasi ya kujieleza na kusiklilizwa na
mahakama kwanza kabla ya hukumu kutolewa.
Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa gazeti
la MAWIO, Simon Mkina amesema alishangazwa sana na hatua ya serikali kufuta
alichoita “mdomo wa wananchi.”
“Kufuta chombo hiki au kingine kama hiki, ni
kukiri kuwa serikali haipendi kusikia kutoka kwa wananchi…” amesema Mkina
Mkina amesema MAWIO limekuwa gazeti
linalozingatia maadili na kufuata weledi wa hali ya juu katika kuandika na
kuchapisha habari na makala na kuongeza kuwa limekuwa gazeti pekee linalotoa
uwanja mpana kwa wananchi kuandika mawazo yao ili kuchochea uwajibikaji wa
viongozi wa serikali.
Mkina amesema kufuatia uamuzi huo wa Mahakama
Kuu, MAWIO litarejea mtaani Alhamisi ya wiki hii na kuahidi kuwapa wasomaji
wake habari zilizofanyiwa kazi ya ziada.
“Kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, wakati
gazeti halipo mtaani – likiwa limefutwa na serikali, pamoja na kupoteza ajira
za watu na kuingia katika hasara kubwa, bado tulikuwa na kazi ya kujiuliza ni
wapi tulikosea na je, lini tutapewa haki yetu? Bahati nzuri haki yetu imefika,”
aliongeza Mkin.
Uamuzi na hatua ya kulifuta MAWIO, lililokuwa
likichapishwa kila Alhamisi, ulitangazwa na Nape Nnauye, Waziri wa habari,
vijana, utamaduni, sanaa na michezo.
Tangazo lililotolewa katika gazeti la
serikali, Na. 55 la Januari 15, 2016, lilisema serikali inachukua uamuzi wa
kulifuta kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo kupitia Sheria ya Magazeti ya 1976;
sura ya 229 kifungu cha 25(1).
0 maoni:
Post a Comment