Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (kulia) na Mkurugenzi wa Fedha wa
Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro (kushoto) kwa pamoja wakionyesha hundi ya
shilingi milioni mia moja iliyotolewa kwa wakazi wa kata Mvuleni, Manzese
mkoani Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS) ili kuboresha makazi
yao
Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa hafla ya
kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kata Mvuleni,
Manzese ikiwa ni mkopo uliyotolewa kwa wakazi hao ili kuboresha makazi yao.
Mkopo huo ulitolewa na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS). Kutoka kulia ni
Mwakilishi toka UN HABITAT Bw, Phillemon Mutashubirwa, Mkurugenzi
wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro, na Mkurugenzi wa Bodi ya
wakurugenzi ya TAFSUS Bw. John Ulanga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa hafla ya
kukabidhi hundi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kata Mvuleni,
Manzese ikiwa ni mkopo uliyotolewa kwa wakazi hao ili kuboresha makazi yao.
Mkopo huo ulitolewa na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS). Wa kwa kulia ni
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro, na Mkurugenzi wa
Bodi ya wakurugenzi ya TAFSUS Bw. John Ulanga (wa pili kulia) na wa
kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mvuleni, Manzese Bw. Muhidini
Lyomeko.
Mkurugenzi wa Fedha wa
Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi
hundi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kata Mvuleni, Manzese ikiwa ni
mkopo uliyotolewa kwa wakazi hao ili kuboresha makazi yao. Mkopo huo ulitolewa
na Benki ya Azania kupitia asasi ya Tanzania
Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS) ili kuboresha makazi ya
wakazi hao. Wapili kulia ni Mkurugenzi wa Bodi ya wakurugenzi ya TAFSUS
Bw. John Ulanga, mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (wapili kushoto) na Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa Mvuleni, Manzese Bw. Muhidini Lyomeko (wa kwanza kushoto)
Wakazi
wa kata ya Manzese na mtaa wa Mvuleni iliyopo Jijini Dar es Salaam wamepokea
zaidi ya shilingi milioni 100 kutoka benki ya Azania kwa ajili ya kuboresha
makazi yao duni.
Fedha
hizo zinazotolewa kwa udhamini wa asasi inayoshughulikia na uboreshwaji wa
makazi duni nchini Tanzaia ya Tanzania
Financial Services for Underserved Settlement (TAFSUS) itatolewa kama mikopo ya kati ya
shilingi milioni 1.5 mpaka milioni 9 kwa kila
kaya.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya
makabidhiano iliyofanyika katika kata ya Mvuleni mwishoni mwa wiki, Waziri
wa Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi, Mh. Prof. Anna Tibaijuka alisema
mradi wa kuboresha nyumba Manzese Mvuleni umeonyesha mafanikio makubwa na
kuboresha maisha ya wakazi hao.
“Ninafurahi kuwepo katika uzinduzi huu wa
awamu ya pili na tatu ya mradi huu, kwani hii ni moja ya juhudi ambazo
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ingependa kuziona kote
nchini katika kuboresha makazi ya Watanzania.
“Kama unavyofahamu, namna bora ya kuboresha
maisha ya mwanadamu ni kwanza kuboresha makazi yake. Ukishakuwa na
makazi bora, basi hata afya yako itakuwa bora zaidi, watoto wako wataishi na
kukua katika mazingira bora zaidi, watajisomea katika mazingira bora zaidi, na
mambo mengine mengi yatakuwa bora zaidi,” alisema Prof. Tibaijuka.
Naye
mkurugenzi wa bodi ya wakurugenzi ya TAFSUS Bw. John Ulanga alisema TAFSUS ni chombo cha Kitaifa kinachotoa huduma za
udhamini wa kifedha ili kusaidia kuboresha makazi hapa Tanzania hasa katika
maeneo ambayo yana changamoto ya ubora wa makazi na ufinyu wa huduma
mbalimbali.
“Lengo la msingi la TAFSUS ni kuhamasisha na
kuwezesha taasisi za fedha kutoa mikopo ya kuboresha makazi pale ambapo kwa
taratibu za kawaida, mikopo hiyo isingetolewa. Mikopo hiyo hutolewa kuboresha
makazi yakiwemo yale yasiyo rasmi na kuziwezesha jamii zenye kipato cha chini
kuwa na maisha bora,” alisema Bw. Ulanga.
Aliongeza kuwa lengo ni kufikia kaya 2000 na
kutekeleza miradi yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.58 kufikia
mwishoni mwa mwaka 2015.
“Ili kutimiza malengo haya, TAFSUS ilipokea
dola za kimarekani zipatazo million moja na laki mbili kutoka UN-Habitat, kwa
ajili ya kuwezesha miradi ya Jamii kupata mikopo ya uboreshaji makazi,” Bw.
Ulanga alisema.
Bw. Ulanga aliongeza kuwa TAFSUS
imetenga fungu la fedha la mikopo yenye thamani ya shilingi 250,000,000
kwa ajili ya kuboresha nyumba za Mvuleni, takwimu zikionyesha kwamba mtaa huo
wa Manzese Mvuleni una jumla ya kaya 2180 na makadirio ya jumla ya wakazi ni
10,645.
“Ningependa kusema kuwa sisi kama TAFSUS
tunajipanga vizuri zaidi kuhakikisha huduma zetu zinakuwa bora zaidi na
tunawakifikia watu wengi zaidi, ikiwemo kubuni miradi itayosaidia kuboresha
makazi ya Jiji letu na majiji mengine hapa Tanzania, na kuchangia katika
kuboresha maisha ya Watanzania hasa wenye kipato cha chini,” Bw. Ulanga
aliongeza.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Azania Bw. Rukwaro Senkoro alisema
benki hiyo iliitikia wito wa kutoa mikopo ya riba na masharti nafuu kwa ajili
ya kuunga mkoni mradi huo wa kuboresha makazi ya watu, wakitambua kwamba wateja
wao wanatokana na jamii, na hivyo kuwasaidia kuboresha maisha yao ni fahari ya
benki hiyo.
Wakazi wa Manzese Mvuleni walishauriwa na
Waziri Tibaijuka kutumia Ushiriki wa Nyumba (Housing Cooperative)
waliyoianzisha kukusanya hela za kutosha na kuchukua mikopo kutoka kwenye
mabenki au kushirikiana na wawekezaji wengine kujenga majengo ya vitega uchumi
kwenye eneo hilo.
0 maoni:
Post a Comment