MAMA SALMA KIKWETE AHUTUBIA MKUTANO WA ELIMU NA AFYA KWA VIJANA DUNIANI ULIOANDALIWA NA TAASISI YA MAMA SARAH BROWN


Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo,WAMA, Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mama Sarah Brown, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza na Mwenyekiti Mtendaji wa Global Business Coalition for Education muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa ‘Getting Serious About Results: The Grand Convergence of Education and Health” ulioandaliwa na Taasisi ya Mama Sarah Brown kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa. Mkutano huo umefanyika huko New York tarehe 23.9.2014.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Bwana Gordon Brown kabla ya kuanza mkutano uliozungumzia mambo ya elimu na afya kwa vijana duniani tarehe 23.9.2014.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akibadilishana mawazo na Dkt. Sarah Maongezi, Mkurugenzi wa Idara ya Afya katika Taasisi ya WAMA muda mfupi kabla kuanza mkutano huo.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa :’Getting serious about Results: The Grand Convergence of Education and Health’ ambao ulizungumzia mambo ya elimu na afya kwa vijana hapa duniani. Mkutano huo ilifanyika huko New York tarehe 23.9.2014.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza wakati wa mkutano uliojadili masuala ya elimu na afya kwa vijana duniani huku viongozi wengine mashuhuri wakisubiri kuzungumza. Kushoto kwa Mama Salma ni Dkt. Rajiv Shah, Afisa Mtendaji kutoka USAID, akifuatiwa na Bwana Mark Dybul, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Fund to fight AIDS na wa mwisho ni Bwana V. Shanker, Afisa Mtendaji Mkuu wa Afrika, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani kutoka Standard Chartered.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Mama Salma Kikwete akisalimiana na Dkt. Andy Shih, Makamu wa Rais Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya sayansi kutoka katika Shirika la ‘Autism Speaks” (masuala ya usonji) wakati mgeni huyo alipomtembelea Mama Salma kwenye hotelin aliyofikia huko New York, nchini Marekani tarehe 23.9.2014.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Dkt. Andy Shih.
Mke wa Rais na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete akimkabidhi Dkt. Andy Shih jarida la WAMA mara baada ya kufanya mazungumzo ya ushirikiano baina ya Taasisi zao.

Baadhi ya Washirika wakiwa kwenye Mkutano huo.PICHA NA JOHN LUKUWI

Na Anna Nkinda – Maelezo, New York

Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika ikiwemo Tanzania zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa fursa za elimu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule, ubora na usahihi wa elimu, masuala mtambuka kama Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ugonjwa wa Ukimwi.

Changamoto nyingine ni upatikanaji wa huduma rafiki za afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana na udahili mchache wa wasichana katika masomo ya sayansi.

Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea katika majadiliano ya elimu na afya kwa vijana yaliyoandaliwa na Umoja wa kimataifa wa Taasisi za Biashara kwa ajili ya Elimu na kufanyika katika Hoteli ya Reed Smith mjini New York.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kwa upande wa sekta ya afya ina changamoto ambazo zina uhusiano mkubwa na elimu na kutoa mfano wa vifo vya akina mama vinavyotokana na matatizo ya uzazi, vifo vya watoto, ndoa za utotoni, mimba katika umri mdogo, utapiamlo na upungufu wa nguvu kazi.

Alisema Serikali na wananchi wa Tanzania walitambua mapema umuhimu wa kuwekeza kikamilifu katika elimu kama msingi wa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia hususan lengo la pili linalohusu Elimu kwa wote.

“Serikali yetu ilianzisha  Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi  na mpango wa maendeleo ya Elimu ya Sekondari. Mipango yote hii miwili ina malengo ya kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wote walio katika umri wa kwenda shule, kuongeza ubora na usahihi wa elimu.

Kuboresha urari wa kijinsi na walimu na ufundishaji, kuongeza tija katika uongozi na utawala bora, kurasimisha masuala mtambuka kama vile UKIMWI, Elimu ya Stadi za Maisha,  elimu ya mazingira na jinsia”, alisema Mama Kikwete.

Alisema mpango wa  matokeo makubwa sasa katika elimu unalenga kujenga uwezo wa walimu kwa kutoa mafunzo ya pahala pa kazi, kusaidia watoto wasiofanya vizuri kwa kuandaa vitendea kazi mahususi vinavyozingatia umri na mahitaji, kuboresha miundo mbinu, kwa kujenga madarasa, maabara na nyumba za walimu.

Kuboresha vifaa vya ufundishaji kama vile madawati, vifaa vya maabara, kemikali na  kutoa vitu vya kuongeza motisha kwa walimu.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alimalizia kwa kusema elimu bora itapatikana ikiwa afya za vijana zitaboreshwa na kuwa na mikakati ambayo inatambua uhusiano mkubwa wa masuala hayo kwani bila ya elimu timilifu ni vigumu kufikia malengo yaliyopo.

Kwa upande wake Mke wa waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Mama Sara Brown ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Umoja wa kimataifa wa Taasisi za Biashara alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi anayoifanya ya kutoa elimu kwa watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuboresha afya ya mama na mtoto.

“Nilitembelea nchini Tanzania mwaka 2007 na kujionea kazi anayoifanya Mama Kikwete nampongeza kwa hili. Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu na afya bora ili waweze kuwa na maisha bora hapo baadaye”, alisema Mama Brown.

Nao wachangia mada katika mjadala huo walisema ni muhimu watoto wa kike wakapata elimu sawa na watoto wa kiume kwani wakipata elimu unyanyasaji wa kijinsia ambao unazidi kuongezeka dhidi yao utapungua na kutakuwa na usawa katika mambo mengi.

Walisema, “Wafadhili mbalimbali wamekuwa wakiwekeza katika afya na elimu hasa kwa watoto wa kike ili kuwajengea mazingira mazuri ya kusoma ikiwa ni pamoja na kuwajengea madarasa na vyoo. Ni vyema vijana wakapata elimu na afya bora ili waweze kujihusisha na shughuli za maendeleo”.


Mkutano huo ni moja ya maandalizi ya Mkutano wa  69 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UN) unaotarajiwa kufunguliwa tarehe 24/9/2014    mjini humo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment