Dk Abbas: Nina kitu cha kujivunia kwenye tasnia ya habari



MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo, Dk Hassan Abbas na wahitimu wengine wawili, wametunukiwa shahada ya juu ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma.
Dk Abbas ametunukiwa shahada hiyo katika mahafali ya 18 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino mwishoni mwa wiki jijini Mwanza. Wengine waliotunukiwa PhD ni Naibu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo nchini, Cosmas Mwaisobwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gideon Kamfipo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Dk Abbas alisema ana furaha kubwa kutunukiwa shahada hiyo ya uzamivu katika mawasiliano ya umma ingawa amepitia changamoto nyingi.
“Kuna wakati nilihama mjini na kwenda vijijini na kuna wakati nilikaa miezi sita bila ya mshahara, nilikaa pia mbali na familia yangu ili kukamilisha mambo ya kitaaluma hasa shughuli za utafiti,” alisema Dk Abbas.
Alisema ni safari ndefu kwa mtu kuhitimu shahada ya Uzamivu, ambayo mtu hawezi kuifanya peke yake na kwamba kuna wakati inabidi mtu kukaa mbali na dunia amalize vitu vya msingi vinavyohitajika zikiwemo shughuli za utafiti.
“Ilikuwa safari ndefu na nikiri kuwa sikuifanya peke yangu, nimesaidiwa na watu zaidi ya kumi kutoka mataifa tofauti katika kukamilisha thesis (utafiti) yangu. Wengi walitoka nchi mbalimbali kama vile Kenya, Uingereza, Ireland, Canada na Zimbabwe na sasa nina kitu cha kujivunia kwenye tasnia ya habari,” alisema Dk Abbas.
Alisema matarajio yake ni kuendelea kuitumikia sekta ya habari nchini akiwa kama mwanataaluma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo, kwa kufundisha na kutoa mihadhara ya kitaaluma kwenye vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi pale atakapokuwa akihitajika.
“Shahada hii ya uzamivu imenipa upeo mkubwa na dhamira yangu ni kuisimamia vyema sekta ya habari ili tuwe na responsible journalism ambayo itachangia kwenye maendeleo ya uchumi wa nchi na mabadiliko yanayoendelea nchini,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Thadeus Mkamwa amemuelezea Dk Abbas na wahitimu wenzake Dk Cosmas Mwaisobwa na Dk Gideon Kamfipo kuwa wao ni matunda ya pili ya chuo katika kuhitimu shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano ya Umma.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment