Benki yakwamisha uwekezaji KNCU wa shilingi bilioni 40

Image result for bank of tanzania image


 
 
 
 
 
 
KAMPUNI za Africado na Tanbreed, zilizoshinda zabuni ya kuwekeza katika shamba la Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) lenye ekari 3,414 yametishia kufunga virago baada ya benki moja (jina limehifadhiwa) kukwamisha uwekezaji huo wa zaidi ya Sh bilioni 40.

Kampuni ya Africado inaongoza Afrika Mashariki kwa uzalishaji wa maparachichi na kuuza katika masoko ya kimataifa imepanga kutumia shamba hilo kwa kilimo cha parachichi wakati Tanbreed inaongoza Afrika Mashariki kwa ufugaji wa kuku.

Kampuni hizo ambazo ziliingia mkataba na KNCU, Aprili mwaka huu tayari zimekwishatumia zaidi ya Sh bilioni tano kwa kununua miche ya miparachichi, vifaranga vya kuku. Aidha zilikuwa zinatarajia kuajiri wafanyakazi zaidi ya 500 mara mradi huo ukianza kazi.

Uchunguzi uliofanywa na Habari- Leo umebaini kuwa wawekezaji hao wameshindwa kuendelea na kazi licha ya kupata baraka kutoka Mkutano Mkuu wa KNCU, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi na Maendeleo Makazi na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini.

Alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu suala hilo, Wakili wa kampuni hizo, Kisaka Mnzava kutoka kampuni ya Stratton & Company Advocates ya jijini Arusha, alisema kuna urasimu usioeleweka ambao umekuwa ukikwamisha kuanza kwa shughuli katika shamba hilo kwa muda mrefu sasa.

Alisema urasimu huo unapingana na sera za Rais John Magufuli anayetaka wawekezaji kuja kwa wingi Tanzania kwa lengo la kuwekeza. Mzava alisema uongozi wote wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya na mawaziri wa wizara husika na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, walitembelea shamba hilo na kutoa baraka zote za kuanza kwa mradi huo.

“Wawekezaji wamekata tamaa, wanataka kufunga virago. Tunamuomba Rais Magufuli kunusuru hali hiyo,” alisema Wakili Mzava. Alisema uwekezaji katika shamba hilo umetengewa Sh bilioni 40 na utainufaisha nchi pamoja na vijana wa kike na kiume kupata ajira katika miradi hiyo mikubwa mkoani Kilimanjaro.

Wakili huyo alisema kuwa tayari miche ya miparachichi imeingia nchini kutoka Afrika Kusini zaidi ya miezi miwili na iko katika bandari ya Dar es Salaam lakini wanashindwa kuichukua kufuatia urasimu wa benki hiyo.

Alisema benki hiyo pia inapaswa kumlipa mpangaji wa awali stahili yake ili aweze kuondoka katika shamba hilo lakini yote hayo yanashindwa kufanywa na taasisi hiyo ya fedha bila ya sababu za msingi na kufanya wawekezaji hao kutaka kusitisha mradi huo na kufunga virago.

Alisema ilikuwa imekubaliwa katika Mkutano Mkuu wa KNCU kwamba Sh bilioni 9.3 za kampuni zilizoshinda zabuni ziwekwe katika benki hiyo kwa kuwa KNCU ndio ilikopa Sh bilioni tano kwa ajili ya shughuli mbalimbali za chama hicho.

Habari zaidi zilisema kuwa licha ya kuingizwa fedha hizo katika benki hiyo, lakini uongozi wa juu taasisi hiyo ya fedha umewakwamisha wawekezaji wakidai wanasubiri ushauri kutoka kwa Waziri Mkuu. Tangu waseme hivyo sasa ni mwaka.
Mmoja wa viongozi wa juu wa KNCU ambaye aliomba kutotajwa jina lake alisema kukwama kuanza kwa mradi huo kunasimamisha shughuli nyingi za chama hicho na uongozi wa juu hauelewi sasa ufanye nini kunusuru hali ya kiuchumi ambayo huenda ikawa mbaya kutokana na kutokelezwa kwa mradi huo.

Alisema KNCU ilikuwa taabani kifedha na kwa kupata wawekezaji hao iliona kama imepata nafuu kubwa lakini kwa sasa hali inakuwa ile ile baada ya benki hiyo kukwamisha tena mradi huo wakati fedha ziko mikononi mwao, ikiwa ni pamoja na kulipa madeni yote chama iliyokopa miaka ya nyuma.
“Tunamwomba Rais na Waziri Mkuu kuingilia kati suala hilo ili kuokoa mali za chama hicho vingine chama hicho kitakufa kifo cha mende,” alisema kiongozi huyo.

Awali gazeti hili liliripoti habari hiyo kuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ilidaiwa kuwa na urasimu katika suala la zabuni ya uuzaji wa shamba la KNCU, baada ya kushindwa kutoa kibali kwa kampuni zilizoshinda zabuni ya kununua shamba hilo na mara baada ya habari hiyo, wizara ilitoa kibali kwa kampuni hiyo kuendelea na shughuli.









































Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment