Naibu katibu mkuu wizara ya elimu sayansi na teknolojia, Profesa Simon Msanjila, amesema serikali imebaini kuwa idadi kubwa ya wanafunzi walioomba mikopo kupitia bodi ya mikopo ya elimu ya juu nchini, wameandika na kujaza taarifa za udanganyifu katika fomu zao za maombi.
Profesa Msanjila ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya nne ya chuo kikuu cha Sayansi na teknolojia mkoani Mbeya (MUST), ambapo wanafunzi zaidi ya 800 walihitimu kozi mbalimbali ikiwemo usanifu wa majengo na uhandisi. Alisema serikali imeanza uhakiki wa kupitia fomu zote zilizowasilishwa katika bodi hiyo na kueleza kuwa atakayebainika kujaza nafasi zisizokuwa sahihi lazima afikishwe katika vyombo vya sheria.
“Siku hizi kuna changamoto kwamba kila mwanafunzi akipata udahili ni definition kwamba ametoka familia maskini sasa sijui kama hilo ni kweli. Lakini tuelewe kwamba kuna vigezo ambavyo vimewekwa na ambavyo tunapima ni nani apate mikopo hiyo na vigezo vimewekwa na serikali. Changamoto nyingine ni kwamba waombaji wengine sio wote baadhi wanatoa taarifa zisizo sahihi wanawasilisha document za kuombea mikopo na kufoji na vinginevyo,” alisema Msanjila.
“Serikali imeanza kufanya uhakiki wa fomu zote zilizotumika kwenye maombi na wale watakaogundulika kutumia taarifa za uongo sheria itachukua mkondo wake,” aliongeza.
0 maoni:
Post a Comment