Wagoma kufanya uchaguzi wakidai kijiji



Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtataru mwenye flana ya njano, akizungumza na wakazi wa Sadani



Wananchi wakisikiliza kwa makini

 

Afisa maendeleo ya jamii Wilaya ya Mufindi, Hatibu Bwashehe, akifafanua jambo wakati wa mkutano huo

Na Mathias Canal, Mufindi
Baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Mbugi, Kata ya Sadani, Wilayani Mufindi, wamegoma kufanya maandalizi ikiwa ni pamoja na uchaguzi utakaofanyika Disemba 14 mwaka huu wa kuchagua viongozi wa serikali ya kijiji kutokana na serikali kushindwa kutekeleza adhma yao ya kuwapatia Kijiji walichoomba.

Wakizungumza na Mjengwablog kijijini hapo wanakijiji hao wamesema kuwa hawapo tayari kufanya uchaguzi hadi pale serikali itakapokuwa imewapa heshima ya kijiji ambayo wamekuwa wakiidai kwa muda mrefu sasa.

Akizungumza na Mjengwablog, Gregory Mgimwa, ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mbugi alisema kuwa serikali imekuwa ikilifumbia macho jambo hilo takribani miaka minne bado halijapatiwa ufumbuzi.

Mgimwa alisema sababu inayowafanya hadi wafikie hatua ya kutaka kijiji chao ni kutokana na uvivu wa wananchi wa Kijiji cha Utosi katika shughuli za maendeleo hususani katika ujenzi wa daraja na Zahanati.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu, akizungumza na wakazi hao wakati wa ziara yake aliwaomba wananchi hao kuchagua viongozi wa kijiji kwani athari ya kutokuwa na viongozi hawataiona leo wala kesho bali ni baada ya kukosa maendeleo kwa muda mrefu.

"Mimi nimeamua kuingilia kati jambo hili hivyo naahidi kulifatilia kwa ukaribu hadi mpatiwe kijiji kama vigezo vyote mnavyo, lakini chagueni viongozi ambao nitasaidiana nao kulifatilia jambo hili kwa kuwa mimi peke yangu sitaweza" Alisema Mtaturu

Akizungumzia swala la ugawaji wa vijiji, Mtaturu alisema kuwa hiyo sio kazi ya diwani, mbunge, chama cha mapinduzi wala chama chochote kile bali ni kazi ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

"Kumbukeni uchaguzi unafanyika kwa wakati lakini TAMISEMI wanagawa vijiji kutokana na vigezo pia ni lazima wajiridhishe, hivyo tutakapokuwa tunafatilia ni lazima tuwe na uongozi ili shughuli za maendeleo ziwe zinasonga mbele" Alisema Mtaturu

Sambamba na hayo Mtaturu aliwapatia mifuko 30 huku akiahidi tarehe 8/11/2014 kufika kijijini hapo na mbunge wa Jimbo hilo Mahamoud Mgimwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ambayo itakamilika haraka endapo kama wananchi watajitokeza kwa wingi katika kazi hiyo.

Hata hivyo Aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na imani na mbunge wao kwani atashirikiana naye kwa ajili ya kuhakikisha TAMISEMI wanatoa majibu mazuri kutokana na vigezo vyao.

Hadi Mjengwablog inaondoka Kijijini hapo wananchi hao walikuwa wamekubaliana na katibu huyo kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa serikali ya kijiji, ambapo waliamua viongozi wote wa vitongoji waliokuwa kwenye serikali ya mpito kuendelea na madaraka yao na hatimaye kugombea uchaguzi wa serikali za mitaa Disemba 14 Mwaka huu bila bugza yoyote.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment