JICHOPEMBUZI: Madereva 15 wa bodaboda mbaroni Morogoro. Polisi Mkoa wa Morogoro inawashikilia madereva 15 wa bodaboda
Morogoro. Polisi Mkoa wa Morogoro inawashikilia madereva 15 wa bodaboda kwa tuhuma za kufanya vurugu katika eneo la Fire zilizosababishwa na mmoja wao kumdhalilisha askari mmoja wa kike.
Ofisa Habari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji katika Kituo cha Fire, Issa Isandekeku alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi. Alisema kabla ya vurugu hizo, dereva wa pikipiki alifanya kitendo hicho kwa askari aliyekuwa akielekea kazini muda huo. Isandekeku ambaye pia ni Mkaguzi Msaidizi wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, alisema baada ya dereva kufanya kitendo hicho alikimbia, lakini alikamatwa.
Alisema muda mfupi baadaye kulizuka vurugu zilizoanzishwa na waendesha pikipiki wakipinga mwenzao kukamatwa, huku wakirundika mawe na taka katika Barabara ya Mindu, Kata ya Kingo. Isendekeku alisema hali hiyo ilisababisha shughuli mbalimbali za wananchi kusimama kwa zaidi ya saa moja kutokana na kuhofiwa kujeruhiwa katika tukio hilo. “Hizi vurugu zimesababishwa na waendesha pikipiki ambao waliweka vizuizi barabarani ili raia wasipite. Lakini muda huo mwenzao alikuwa ameshakamatwa. Tena alimdhalilisha askari akiwa na sare za kazi, hali ambayo ni kinyume cha sheria,” alisema Isendekeku.
Alisema baada ya askari wa zimamoto kuzidiwa nguvu, walitoa taarifa polisi ambao walidhibiti vurugu eneo hilo na kurejea utulivu. Alisema katika vurugu hizo, polisi Rajabu Seleman alijeruhiwa kichwani kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali. Kaimu Kamanda wa Polisi, Mussa Maramba alisema mbali na watu hao kukamatwa pia wanazishikilia pikipiki tano zilizotelekezwa katika vurugu hizo. Kamanda Maramba alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya uchunguzi kukamilika. “Vurugu hizi ukiangalia hazikuwa na sababu ya msingi... sasa sijui hao madereva walifanya fujo kwa masilahi ya nani ?” alihoji Kamanda Maramba. Katika tukio hilo, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatanya vijana waliokuwa wanafanya vurugu na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao. Hata hivyo, Kamanda Maramba alitoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati askari wanapotekeleza majukumu yao ya kazi ikiwamo kutuliza fujo katika eneo husika. ADVERTISEMENT - DESKTOP VIEWBACK TO TOP Habari Burudani Michezo Biashara Makala
0 maoni:
Post a Comment