Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Askofu Josephat Gwajima, amezindua operesheni mpya aliyoipa jina la ‘Operesheni
81Mzizima’ huku akimtaka mtu anayeitwa Daud Bashite ajitokeze hadharani kuthibitisha
uhalali wa vyeti vyake.
Hivi karibuni, Askofu Gwajima alihubiri
kanisani kwake na kusema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anatumia
vyeti vya mtu anayeitwa Paul Christian, wakati jina lake halisi ni Daud Albert
Bashite.
Akizungumza wakati wa ibada kanisani hapo,
Ubungo jijini Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima alisema operesheni hiyo
mpya ni vita ya mwisho ya kumshikisha mtu adabu.
Alisema, tangu aanzishe hoja hiyo, hadi sasa
wahusika hawajajitokeza hadharani kujibu tuhuma hizo, jambo ambalo alisema
linaonyesha alichokisema ni kweli.
“Tangu niibue hoja ya Makonda anatumia vyeti
vya Daud Albert Bashite, hakuna aliyejitokeza hadharani kukanusha madai yangu.
“Mimi naamini nilisema ukweli kwani kitendo
cha kukaa kimya kinaonyesha wazi kuwa ni kweli ninachokisema na kama anabisha,
aje hadharani kukanusha akiwa na vyeti vyake na mimi nitakuja na vyangu…
“Kuna baadhi ya watu wananisihi sana niache
kumchambua eti wanasema, Gwajima acha, hiyo inatosha.
“Mbona wakati Makonda aliponihusisha na dawa
za kulevya hakuna aliyejitokeza kumwambia aache?
“Hii ni vita ya mzizima ya kushikisha adabu
iitwayo hold the final battle of good manners,”alisema Askofu
Gwajima.
“Hizi ni salamu tu ili ajue kuwa
ukimshambulia baba wa imani, hauwezi kubaki salama kwa sababu viongozi wa dini
wanapigana vita mbalimbali ikiwamo majini na mashetani, lakini wanashinda kwa
jina la Yesu.
“Nina uhakika na nina ushahidi usio na shaka
kuhusiana na suala hilo, labda ajitokeze na kuniomba msamaha.
“Nina material na mazagazaga kibao kuhusu
Daud Bashite, niseme,” alihoji Gwajima huku waumini wake wakiitikia semaaa.
“Lakini, kwa leo sitaki nimwongelea sana, kwa
sababu namwonea huruma, ila ninachotaka kumwambia ni kwamba, usiweke miguu yako
kwenye mashine ya kusaga na kukoboa, utageuka sembe.
“Akumbuke kuwa, baba wa familia akiguswa,
hata watoto wanaamka, ndicho kilichojitokeza katika maisha yangu kwani baada ya
kushambuliwa sana, waumini wameongezeka tofauti na awali.
“Hata wale waliokuwa hawaji kanisani, hivi
sasa wanakuja,”alisema.
Katika mahubiri hayo, Askofu Gwajima alisema
kuna wakati Mungu huwainua watu wake kwa makusudi maalumu ili kutimiza kusudio
lake.
“Sasa nataka kumwambia kuwa, hizi ni salamu
tu, nimerusha ka kipande tu… kuhusu Bashite, lakini kelele kibao.
“Hapa sitaki maigizo wala ngonjera,
ninachotaka ni samahani tu, lakini anapaswa kujua kuwa, ukimshambulia baba wa
imani, awe askofu, mchungaji, padri au wa dini yoyote, hauwezi kubaki salama,
lazima na wewe utashambuliwa tu,”alisema.
Pamoja na hayo, alisema kama ataamua kukaa
kimya kama anavyoombwa na baadhi ya watu, akikaa kimya Mungu atawainua watu
wengine ili waweze kuzungumza kwa niaba yake.
Kwa mujibu wa Gwajima, hana nia ya kumchafua
mtu kwenye suala hilo wala hana mgogoro na hana tatizo, ila aliamua kusema
alichokisema kwa sababu alichokozwa.
Pia, Askofu Gwajima alisema ana historia
ndefu inayoanzia Oktoba 21, mwaka 1996 wakati alipoanzisha kanisa lake na
kupitia changamoto mbalimbali ambazo alizishinda kwa nguvu za Mungu.
Alisema kwamba, hadi sasa ana makanisa 400
yaliyopo maeneo mbalimbali ndhini na mengine 300 yaliyopo katika nchi
mbalimbali duniani.
Katika mabuhiri hayo, Askofu Gwajima
alimtolea mfano Erick Shigongo kwa kile alichosema kuwa ni miongoni mwa watu wa
kuigwa kwani wanatafuta mafanikio kadri wawezavyo.
Wiki iliyopita Jeshi la Polisi kwa mara
nyingine lilizingira nyumba ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima, kwa kile lilichodai kuwa lilifika kufanya uangalizi.
0 maoni:
Post a Comment