Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
wa Japan, Hirotaka Ishihara baada ya kukutana naye Ofisini kwake jijini
Dar es salaam August 30, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………..
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
umefika wakati wa Japan kuhamia barani Afrika na na kuwekeza kwa nguvu
hasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumamosi, Agosti 30, 2014) wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje wa Japan, Bw. Hirotaka Ishihara na wafanyabiashara kutoka Japan
kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Bw. Ishihara
anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara 70 kutoka makampuni makubwa 14 ya
Japan.
Akizungumza na Bw. Ishihara na
baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo, Waziri Mkuu alisema
ni ukweli usiopingika kwamba Japan ni nchi yenye uchumi imara na kwamba
licha ya kuwepo kwa mikutano ya TICAD ambayo hutoa fursa kwa Japan
kushirikiana na nchi za kiafrika, bado kuna haja ya wao kuelekeza macho
yao Afrika kipekee.
“Mikutano ya TICAD imekuwa
ikifanyika kwa zaidi ya miaka 20 sasa lakini nchi za Afrika na hasa
Afrika Mashariki tumefumba macho… tumeshindwa kutumia kwa kiasi kikubwa
fursa zilizopo na kuchota utaalamu wa kiteknolojia kutoka Japan,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema Afrika
Mashariki ni soko la uhakika kwa mtu yeyote anayetaka kuwekeza barani
Afrika. “Kama nchi wanachama wa Jumuiya siyo soko la kutisha, lakini
kutokana na mahali nchi zetu zilipo, tuna fursa kubwa ya kufungua
milango ya soko kwa nchi zote jirani zinazotuzunguka na hiyo ni fursa
kubwa kwa mwekezaji yoyote,” alisisitiza.
Kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu
alisema Japan inaweza kuwekeza kwenye viwanda vya nguo na kusokota
nyuzi, kuna fursa kwenye viwanda vya kusindika samaki kwani kuna aina
nyingi za samaki waliopo katika bahari ya Hindi. Pia alisema amefarijika
kusikia kwamba wameonana na wahusika kutoka Shirikisho la Sekta Binafsi
Tanzania (TPSF) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje wa Japan ambaye ndiye kiongozi wa msafara huo alimweleza
Waziri Mkuu kuridhishwa kwake na mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo
mbili na kwamba katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na ongezeko la
ziara za viongozi baina ya nchi hizi mbili.
“Nina furaha kuzuru Tanzania kwa
mara
ya pili nikiongoza Kamati ya Pamoja ya Umma na Sekta Binafsi ya
Kukuza Biashara na Uwekezaji nchini Tanzania… tumevutiwa na kasi ya
ukuaji uchumi wa Tanzania, ndiyo maana makampuni ya Kijapani yameonyesha
nia ya kuja kuwekeza nchini Tanzania,” alisema Bw. Ishihara. Bw.
Ishihara na msafara wake wamemaliza ziara yao ya siku ya tatu hapa
nchini na wanaondoka Tanzania kurejea Japan leo jioni.
0 maoni:
Post a Comment