Rais Jakaya Kikwete
Dodoma. Hatima ya Bunge Maalumu
la Katiba imebaki mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, ambalo limemwandikia
barua kiongozi huyo wa nchi kutaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu tarehe
ya mwisho ya kumaliza vikao vyake.
Hiyo ni kutokana
na muda uliopangwa kwenye ratiba ya bunge hilo kuzua utata wa kisheria
na kuwapo uwezekano wa mwingiliano na Bunge la Jamhuri ya Muungano na
Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar.
Ratiba ya Bunge
Maalumu la Katiba inaonyesha kuwa limepanga kuhitimisha vikao vyake
mwishoni mwa Oktoba, tofauti na tarehe iliyotolewa na Rais Jakaya
Kikwete Julai 28, mwaka huu ambayo ilitangazwa katika Gazeti la Serikali
(GN) namba 254 la Agosti Mosi.
Tangazo la Rais linaonyesha
kuwa awamu ya pili ya Bunge Maalumu ingeanza Agosti 5, 2014 na
kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba ya Bunge hilo inaonyesha kuwa
litamalizika Oktoba 31, siku ambayo mwenyekiti wa Bunge hilo atakabidhi
kwa Rais Katiba inayopendekezwa.
Hata hivyo, uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa hadi sasa Serikali bado haijatoa tangazo (GN)
lingine kuongeza muda hadi mwishoni mwa Oktoba kama alivyosema
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta wakati akitoa ufafanuzi wa
siku 60 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, Agosti 5 mwaka huu.
Sitta
alisema kwa kadiri ya tafsiri, siku za kazi ni Jumatatu hadi Ijumaa
ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na kwamba Jumamosi na Jumapili
siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na Rais.
Hata hivyo,
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hadi sasa hawajapata
maelekezo ya ziada kutoka serikalini ambako waliandika barua ya kuomba
ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo.
“Tulimwandikia
barua, Katibu Mkuu Kiongozi (Ombeni Sefue) kuomba ufafanuzi wa siku hizo
kama ambavyo sisi tungependa iwe, lakini hadi sasa bado hatujajibiwa
lakini bado siku zipo nadhani tutajibiwa tu wakati mwafaka,” alisema
Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Sefue
alikiri ofisi yake kupokea barua kutoka Bunge Maalumu ikiomba ufafanuzi
ambao ungeliwezesha kuongeza siku kwa lengo la kukamilisha kazi ya
kujadili na kuandika Katiba inayopendekezwa na kwamba maombi yao bado
yanafanyiwa kazi.
“Bado tuna muda wa kutosha tu, ni kweli
tulishayapokea maombi ya Bunge Maalumu kuhusu suala hilo na Mheshimiwa
Rais akikamilisha kazi yake watajulishwa tu,”alisema Sefue.
Utata wa kisheria
Licha
ya ahadi iliyotolewa na Sitta ni dhahiri kwamba suala hilo lina utata
wa kisheria kutokana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwanasheria wa
Serikali (AG), Jaji Frederick Werema wakati akitoa ufafanuzi wa maana ya
siku 70 ambazo Bunge lilikaa mara ya kwanza.
Baada ya kusoma
hati ya Rais ya kuitishwa kwa Bunge hilo, Februari mwaka huu, Jaji
Werema alisema siku 70 zilizotolewa kwa mujibu wa tangazo la Serikali ni
za kikalenda na siyo siku za kazi kwa sababu wajumbe wa Bunge Maalumu
siyo watumishi wa kuajiriwa.
Maelezo ya Jaji Werema
yalitokana na swali lililoulizwa na Mjumbe wa Bunge Maalumu, Ezekiah
Oluoch ambaye alitaka ufafanuzi huo kutokana na siku zilizotengwa
kuonekana kwamba ni chache na zisingetosha kukamilisha kazi ya kutunga
Katiba.
Kauli ya Jaji Werema haijawahi kutenguliwa na
Mahakama au yeye mwenyewe na kwa msingi huo, kwenda kinyume chake ni
kuvunja Sheria ya Kazi na Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura
ya 268 ya 2005.
Vifungu vya 22 (1) na (2) vya sheria hiyo
vinazungumzia ushauri wa kisheria wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu
suala lolote analotakiwa kulitolea ufafanuzi, wakati Kifungu cha 23 (1)
kinasema ushauri huo unabaki kuwa msimamo wa Serikali katika suala
husika, vinginevyo ubatilishwe ama na Mahakama au na AG mwenyewe katika
utekelezaji wa wajibu wake.
Jana katika maelezo yake, Katibu
Mkuu Kiongozi, Sefue alisema Jaji Werema alikuwa sahihi katika tafsiri
aliyoitoa kuhusu siku zilizotolewa na Rais wakati wa awamu ya kwanza ya
Bunge Maalumu.
“Jaji Werema yuko sahihi kabisa, kwa hiyo
hata Rais atakapokuwa akitoa majibu ya maombi yaliyofikishwa kwake
kuhusu nyongeza ya siku atazingatia sheria za nchi,” alisema.
Bunge la Muungano na BLW
Mgogoro
mwingine unaojitokeza ni ratiba za vikao vya Bunge la Muungano ambalo
limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo
limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22, mwaka huu.
Kwa
kawaida, vikao vya Bunge hutanguliwa na wiki mbili za vikao vya kamati
za kudumu na ikiwa ratiba itabaki kama ilivyo, basi vitaingiliana na
vikao vya Bunge Maalumu ambalo ratiba yake imepangwa kuendelea hadi
Oktoba 31, mwaka huu.
Katibu wa Bunge la Muungano, Dk Thomas
Kashililah alisema vikao vya Kamati za Bunge hilo vinatarajiwa kuanza
Oktoba 13, mwaka huu kutokana na kuwapo kwa miswada mingi ya Serikali
inayopaswa kufanyiwa kazi.
“Tuna miswada ya Serikali kama 12
hivi ambayo mingine imekaa muda mrefu, kwa hiyo kamati zetu nyingi
zinapaswa kukutana mapema ili kuifanyia kazi vinginevyo tutakwama,”
alisema Dk Kashililah ambaye pia ni Naibu Katibu wa Bunge Maalumu.
Alipoulizwa
kuhusu mwingiliano wa ratiba baina ya taasisi hizo mbili ambazo yeye ni
mtendaji wake, Dk Kashililah alisema suala hilo litatafutiwa ufumbuzi
kabla ya muda huo kuwadia.
“Nadhani wakati tunafikiria suala
la muda wa Bunge la Katiba, hatukufikiria ratiba hizi nyingine, kwa hiyo
ni dhahiri kwamba pengine tutalazimika kuangalia jinsi ya kutoka hapo,”
alisema.
Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai
mwishoni mwa wiki iliyopita alisema kwa jinsi ratiba ya Bunge Maalumu
ilivyopangwa lazima itaingilia shughuli za Bunge la Muungano, hivyo
uamuzi unapaswa ufanywe ili kuepusha mgongano huo.
“Sisi
tumeishaliona hilo kwamba ni changamoto, tulikuwa tukijaribu kujadiliana
kuona kama baadhi ya vikao vya kamati vinaweza kuanza mapema hapa
Dodoma, lakini uamuzi bado haujafanyika,” alisema Ndugai.
Naye
Hamad alikiri kwamba kalenda ya vikao vya Baraza la Wawakilishi
inaingiliana na ratiba ya Bunge Maalumu na kwamba wanafikiria jinsi ya
kuondoa kasoro hiyo.
“Kuna njia nyingi za kuondoka hapo,
pengine tunaweza kumwomba Rais asogeze mbele vikao vya Baraza la
Wawakilishi kwa wiki mbili, maana hiyo inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba.
Hata hivyo, tutalifanyia kazi ili kufahamu jinsi ya kulitatua,”alisema
Hamad.
Akizungumzia changamoto hiyo ya mwingiliano wa ratiba
za kazi za taasisi hizo, Balozi Sefue alisema jambo hilo ni miongoni
mwa yatakayozingatiwa wakati wa kufanya uamuzi.
“Tutakapokuwa
tunafanyia kazi suala hilo, tutazingatia hayo yote na tutahakikisha
kwamba hakutakuwa na mwingiliano wa aina yoyote,” alisema
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 maoni:
Post a Comment