HALMASHAURI YA KILOLO YAWASIMAMISHA KAZI VIGOGO WANNE, AFISA HABARI WAKE AWAKERA WANAHABARI

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Rukia Muwango

PAMOJA na jitihada za anayedaiwa kuwa Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa kuwakwamisha wanahabari kupata taarifa za kinidhamu zinazoihusu halmashauri hiyo, taarifa za uhakika zinaonesha kwamba vigogo wanne, akiwemo Mweka Hazina wake wamesimamishwa kazi.

Mbali na mweka hazina, vigogo wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Afisa Manunuzi, Afisa Misitu na Mwanasheria wa Halmashauri.

Afisa habari huyo aliyetajwa kwa jina la Namwinga alipoombwa namba ya mmoja wa vigogo hao alijibu kwa jeuri akisema; “siwezi kutoa namba yake, siwajibiki kwake, labda kama ungeniomba namba ya Mkurugenzi ningekupa.”

Alipoulizwa majukumu yake kama afisa habari wa halmashauri hiyo ni yepi? …..alisema “ nachoweza kufanya kama afisa habari labda ni kumpa huyo unayeteka namba yake ili yeye mwenyewe akupigie.”

Alipoulizwa toka lini amekuwa Afisa Habari wa Halmashauri hiyo na kama kazi anayofanya ilitangazwa ili kuwashindanisha na watu wengine wenye sifa zaidi yake, Namwinga kwa kuonesha jeuri ya kazi yake hiyo alikaa kimya bila kujibu chochote kwa zaidi ya dakika tatu za mawasiliano.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Rukia Muwango alitoa ushirikiano wa hali ya juu huku akikiri watumishi hao kusimamishwa kuendelea na majukumu yao ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazoelekezwa dhidi yao.

Katika ufafanuzi wake aliotahadharisha kwamba hawezi kuutoa kwa kina ili kutoingilia suala hilo linaloendelea kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria, alisema watumishi hao wanahusishwa katika mikataba tata iliyoiletea halmashauri hiyo hasara.

Alitaja mikataba hiyo kuwa ni ile inayohusiana na uvunaji wa miti katika msitu wa halmashauri hiyo na wa kampuni ya New Forest inayozalisha nguzo katika eneo la Viwengi wilayani humo.

“Siwezi kufafanua nini kipo katika mikataba hiyo na hawa watumishi wanatuhumiwaje katika mikataba hiyo. Kwa kuwa wanatakiwa kujieleza au kujitetea, tunasubiri wafanye hivyo,” alisema.

Pamoja na kukataa kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo na jinsi watumishi hao wanavyohusishwa, Muwango alisema yapo mengi yanayotakiwa kuendelea kuthibitishwa.

Alisema watumishi hao wamesimamisha kazi ili kutoathiri uchunguzi unaoendelea kufanywa dhidi ya tuhuma hizo.

“Suala hili linafanywa kwa kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa umma, kwahiyo sitaweza kulisemea kwa kina kwasababu halijifika mwisho,” alisema.

Alisema watumishi hao wamekwishaandikiwa barua za kusimamishwa kazi na wanatakiwa kujitetea kwa kujieleza kuhusiana na tuhuma hizo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Joseph Muhumba alikiri watumishi hao kupewa barua za kusimamishwa kazi.

“Ni utaratibu wa kiutumishi. Wamesimamishwa na wanatakiwa kujitetea kabla maamuzi ya mwisho hayajachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment