Uandikishaji kuanza Januari, kampeni Machi 30
Amesema sheria ya kura ya maoni imeainisha muda wa wadau wa katiba kutoa elimu na kufanya kampeni, hivyo akataka sheria hiyo izingatiwe na kuheshimiwa ili kuepuka ugomvi.
Rais Kikwete alisema hayo jana alipokuwa akihutubia kwenye mkutano kati yake na wazee wa mkoa wa Dodoma, mjini hapa jana.
Alisema upigaji wa kura ya maoni kuhusu katiba hiyo utafanyika Aprili 30, baada ya elimu na kampeni juu ya kura hiyo kuanza rasmi Machi 30 na kuhitimishwa Aprili 29, mwakani kama sheria ya kura ya maoni inavyoelekeza.
“Tumezoea kampeni ni siku 60, lakini baada ya kushauriana na wanasheria kumbe siyo, zina amuliwa na rais kwa mujibu wa sheria,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 5 (4) cha sheria ya kura ya maoni ambayo inapaswa kuzingatiwa, imeelekeza vizuri lini wadau wanatakiwa kutoa elimu.“Utoaji wa elimu juu ya kura ya maoni bado haujafika kwa mujibu wa sheria. alisema”
Rais Kikwete alisema kwa sasa serikali na wananchi wanaongozwa na sheria ya kura ya maoni, kwani imeainisha muda wa kampeni.
“Watanzania wazingatie matakwa ya sheria ya kura ya maoni,...tukizingatia sheri hii hakutakuwa na ugomvi, tukienda kinyume cha hapo ndiyo ugomvi unatokea,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba (BMK) limekwishamaliza kazi yake na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo alikwishakabidhi katiba inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar kama sheria inavyotaka.
Aliwapongeza viongozi wa BMK kwa kumaliza mchakato wa katiba kwa kipindi kifupi tofauti na baadhi ya nchi duniani.
Pia aliipongeza iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kwa kazi nzuri waliyoifanya, ambayo ndiyo iliyotoa mwanga.
“Kilichobakia sasa tuwaachie wananchi waamue, watafanya hivyo kwenye kura ya maoni,” alisema Rais Kikwete.
Aliisifu Katiba inayopendekezwa akisema uzuri wake hauhitaji kuambiwa na mtu, bali unatakiwa uisome na kuielewa, kwani imeandikwa vizuri na kwa lugha rahisi.
Alitoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaipata katiba hiyo, kuisoma na kuielewa ili waweze kufanya maamuzi sahihi badala ya kusubiri kuelezwa na watu wengine.
Alisema tayari katiba hiyo imeshachapishwa kwenye Gazeti la Serikali, hivyo akaagiza sasa ianze kusambazwa kwa wananchi mara moja.
Aliwataka Watanzania kutokubali kulaghaiwa na watu wachache wanaotaka kuwarudisha nyuma na kutaka kuona katiba iliyobora inakosekana.
Alisema sheria ya kura ya maoni inamuagiza Rais kutangaza katiba kwenye Gazeti la Serikali siku 14 baada ya kupokea ndani ya siku hizo atangaze kura ya maoni na matokeo yake yajulikane ndani ya siku 70.
Alisema Waziri Mkuu alipowauliza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuhusu matakwa ya utekelezaji wa sheria hiyo, Nec ilisema kuwa isingeweza kutekeleza ndani ya muda huo kwa sababu wanahitaji mambo mengi na kwamba, wanahitaji kuanzia sasa mpaka Desemba wafanye marekebisho ya kuandikisha wapigakura na kutoa vitambulisho vipya.
Rais Kikwete alisema Nec waliomba miezi mitatu mpaka Machi 2015 kwamba watakuwa wamekamilisha zoezi la uandikishaji upya wa wapigakura wote.
Alisema sheria ya kura ya maoni, imetoa mamlaka kwa waziri mwenye dhamana na mwenzake wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) kubadilisha masharti hayo, hivyo akashauri wapewe nafasi ya kutayarisha.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura na kuomba watumie vizuri fursa hiyo kufanya maamuzi mazuri na kuzingatia maslahi mapana ya taifa na watoto wao na wajukuu zao siku za baadaye.
UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Alisema serikali imelazimika kuitisha uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji Desemba 14, mwaka huu, badala ya Oktoba kwa sababu BMK lilikuwa bado linaendelea na halikuwa linatoa mwelekeo wa muundo wa serikali.
Alisema hiyo ilitokana na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awali kupendekeza kwenye rasimu ya katiba serikali tatu, hivyo isingewezekana uchaguzi huo kufanyika hadi hapo muundo wa serikali ungejulikana.
“Tulikuwa tunasubiri maamuzi ya Bunge la Katiba, maana zingekuwa tatu ingebidi kuahirishwa uchaguzi wa serikkali za mitaa mpaka ufanyike uchaguzi wa Tanganyika,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Baada ya kujua mwelekeo wa Bunge la Katiba ni serikali mbili ndiyo maana tumetoa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa.”
Alisema Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaendelea vizuri na maandalizi ya uchaguzi huo na kwamba ratiba ya uchaguzi na majina ya vijiji, vitongoji na mitaa vimekwishatolewa.
Rais Kikwete alisema uandikishaji wapigakura utaanza rasmi Novemba 23, na kuhitimishwa Novemba 30 kwa orodha ya wapigakura kubandikwa kwenye mbao za matangazo katika vijiji, vitongoji na mitaa ili wananchi wajue majina na vituo vyao.
Aliwataka wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kufanya hivyo.Alisema pia vyama vya siasa vinatakiwa kuwasilisha fomu za wagombea na majina yao kwa msimamizi wa uchaguzi Novemba 20 na 23 saa 10 jioni na kwamba hakutakuwa na udhuru kwa yeyote atakayechelewa.
“Hivyo wenye nia na shauku ya kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wajitokeze kugombea,” alisema Rais Kikwete.Alisema mikutano ya kampeni itafanyika kwa siku 14, kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 13, siku moja kabla ya uchaguzi.
“Rai yangu ndugu zangu, mjitokeze kwa wingi kwenye kampeni kisha tuchague wale watakaotufaa,” alisema.Aliwataka kutoona haya kuwashawishi watu wazuri hasa vijana kujitokeza kugombea.
Alisema kadi ya kupiga kura inayotumika hivi sasa wakati wake umekwisha na kwamba, muda wa kujiandikisha ukifika, wananchi waende wote kujiandikisha ili wapate kadi mpya zitakazowawezesha kupiga kura.
KUHUSU ZIARA YAKE CHINA, VIETNAM
Rais Kikwete alisema Oktoba 21-28, mwaka huu, alifanya ziara katika nchi za China na Vietnam kwa mialiko ya marais wa nchi hizo na kwamba, ziara hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa kwa Tanzania.
Alisema alitumia fursa hiyo kuzungumzia Watanzania walikotoka, waliko hivi sasa na wanakokwenda na kwamba, ziara hizo ziliongeza kwa kiasi kikubwa uhusiano mzuri na wa karibu uliopo kwa muda mrefu baina ya Tanzania na nchi hizo.
Alisema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika ziara hiyo, ni pamoja na kuahidiwa na serikali ya China msaada wa ufadhili Katika nishati ya umeme.
Alisema China iliahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii bila masharti yoyote na kwamba, ilikubali Tanzania pia kushirikiana na Zambia, kusaidia kuimarisha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na kukuza uwekezaji na biashara kati ya nchi hizo mbili.
EBOLA
Alisema maradhi hayo licha ya sasa kuwapo katika nchi za Afrika Magharibi, yalianzia katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alisema ugonjwa huo unaendelea kuwa tishio duniani kwa sababu kasi yake inazidi kukua na umekwishaua watu wengi duaniani na kwamba, hauna dawa wala kinga.
Hata hivyo, alisema taarifa njema bado haujaingia nchini, lakini akasema hata hivyo, upo duniani.
Hivyo, akakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa taifa kwa kila mmoja na kwamba, serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuudhibiti na imejiandaa vya kutosha kukabiliana na ugonjwa huo.
MAOMBI YA WAZEE WA DODOMA
Rais Kikwete aliahidi kushughulikia maombi yaliyomo kwenye risala ya wazee hao, ikiwamo suala la ujenzi wa makao makuu, kurekebisha Bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA), mji wa Dodoma kuubadili na kuwa jiji na upatikanaji wa dawa na kwamba, majibu yatapatikana katika muda mfupi ujao.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, baadhi ya wabunge, viongozi wa serikali, mahakama, madiwani, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi, viongozi wa dini na vyama vya siasa.
Awali, akisoma risala ya wazee wa Dodoma, Katibu wa Baraza la Wazee wa mkoa huo, Alhaj Omar Makuberi, aliipongeza serikali kwa jitihada za kuinua uchumi wa wananchi ili kuondokana na umaskini.
Alimpongeza Rais kwa kuanzisha mchakato wa kupata katiba mpya licha ya misukosuko iliyojitokeza na kumtaka aendelee kusimamia mchakato huo ili ukamilike kabla ya muda wake wa kung’atuka.
CHANZO: NIPASHE
0 maoni:
Post a Comment