Halima Ramadhani ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Mwandaliwa cha Mbweni Dar es Salaam akipokea msaada wa vyakula pamoja na mahitaji mengine kutoka kwa Alex Msama.
Sehemu ya msaada uliotolewa kwa vikundi 10 vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akiwa amembeba mtoto, Haidin Edwin wakati wa hafla ya kukabidhi misaada mbalimbali ikiwemo vyakula kwa vikundi 10 vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akiwabidhi watoto Haidan Edwin na Gatson Edwin sehemu ya msaada wa vitu mbalimbali alivyotoa kwa kikundi cha Tuwakomboe cha Temeke jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mapato ya matamasha yaliyopita.
Watoto wakipata vinywaji baridi wakati wakisubiri kukabidhiwa msaada wa vitu mbalimbali kutoka Kampuni ya Msama Promotions.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari.
KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam chini ya Mkurugenzi wake, Alex Msama, ilikabidhi misaada ya vitu mbalimbali kwa vituo 10 vya kulea watoto yatima ikiwa ni sehemu ya mapato ya matamasha yaliyopita.
Akikabidhi misaada hiyo kwa watoto hao, Msama alisema wamefanya hivyo kwa kutambua nafasi yao katika jamii kwamba, watoto hao wanayo haki ya kupata mahitaji muhimu katika makuzi kama wengine wenye wazazi wao.
Msama alisema msaada huo wenye thamani ya sh. milioni 7.5, ni sehemu ya fedha ambazo zimekuwa zikipatikana kupitia matamasha ya muziki wa Injili ambayo ni wakati wa Pasaka na Krismasi.
“Msaada huu ni sehemu ya fedha ambazo tumekuwa tukizipata kwa njia ya matamasha ambayo tumekuwa tukifanya jijini Dar es Salaam na mikoani; Pasaka na Krismasi,” alisema.
Msama, alisema wamekuwa wakisaidia watoto yatima na makundi mengine maalumu katika jamii kwa kutambua kuwa huo ni wajibu wa kila mmoja na ametoa wito kwa wengine kuwa na moyo wa kusaidia makundi hayo.
Vituo vilivyopata misaada hiyo ni Umra, Zaidia, Hiari, Malaika, Maunga, Mwandaliwa, Sifa, Honoratha, Chakuwama na Rahman vya jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa vitu vilivyokabidhiwa ni unga wa sembe, mchele, unga wa ngano, sukari, sabuni, mafuta ya kupikia, mafuta ya kupaka, dawa za meno na vinginevyo.Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupokea misaada hiyo ya kiutu, viongozi wa vituo hivyo walisema ni faraja kubwa kwao na watoto hao wenye mahitaji maalumu.
Maombio Jonas, mwakilishi wa Kituo cha Sifa Group Foundation cha Bunju, ametoa shukrani kwa Msama kwa moyo wa kujitolea kusaidia watoto wenye mahitaji na kutoa wito kwa wengine kuiga mfano wa moyo huo wa upendo.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Hiari cha Chang’ombe, Aminajat Klemia, alitoa pongezi kwa Msama kutokana na misaada hiyo akisema ni faraja kubwa kwa watoto hao ambao wanahitaji kuthaminiwa kama wengine.
Misaada hiyo imetolewa wakati ambapo kampuni hiyo ipo katika maandalizi ya Tamasha la Krimasi litakalofanyika Desemba 25 kwa ajili ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi kuvuka salama katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
BY Michuzijr
from Blogger http://ift.tt/1Ijnr0n
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment