Uongozi
wa Klabu ya Simba, umetamka wazi kuwa, hautakuwa tayari timu yao kucheza mechi
yoyote dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga huku waamuzi wakiwa ni Watanzania.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji
Manara wakati akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu hiyo,
Kariakoo jijini Dar.
Manara
alisema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutokana na kila wanapokutana na Yanga
kuonewa kwa makusudi na waamuzi ambao wanaonesha dhahiri kwamba wametumwa,
hivyo wamechoka kuonewa, sasa wanataka haki itendeke kwa kuchezeshwa na waamuzi
kutoka nje.
“Tumecheza
na Yanga mara nyingi tu, na mchezo wetu wa mwisho wa ligi kuu tulitoka sare ya
bao 1-1, lakini mwamuzi wa kati siku ile, Martin Saanya alionekana dhahiri
kutunyonga.
“Matukio
ni mengi ya kustaajabisha yalitokea ikiwemo kulikataa bao letu halali na
kulikubali la Yanga ambalo mfungaji kabla ya kufunga, aliukumbatia mpira kama
mtoto, kisha akafunga, halafu mwamuzi eti anaita kati kuashiria bao.
“Haitoshi,
wachezaji wetu wanalalamika, anakuja kumuadhibu nahodha wetu, Jonas Mkude kwa
kumpa kadi nyekundu ya moja kwa moja, lakini kwa kuwa Mungu hamtupi mja wake,
ile kadi ikaja kufutwa na Kamati ya Saa 72 ambayo iliona mwamuzi wao kachemsha.
“Kwa
hali hii, hatutakuwa radhi kuingiza timu uwanjani endapo tu waamuzi wakiwa ni
walewale. Tumechoka kuonewa,” alisema Manara.
Katika
kukazia hilo, Manara alisema wapo radhi wao kama Simba, mapato yote ya mchezo
wao dhidi ya Yanga wagharamie kila kitu kwa waamuzi hao wa nje ili waje
wasimamie haki.
“Tutagharamia
kila kitu kwa ajili ya waamuzi kutoka nje, hata mapato yetu yote ya mchezo
tutatoa kwani tunataka haki itendeke, mbona nchi za wenzetu kama Misri wao
wanaweza kufanya hivyo kwa mechi kubwa kama yetu hii, kwa nini sisi tushindwe,”
alisema.
Aidha
Manara alisema kutokana na Simba kuonewa mara kwa mara, kamati ya utendaji ya
klabu hiyo, imefikia makubaliano ya kumuandikia barua Rais wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TF), Jamal Malinzi ili wakutane waongee ni kwa nini klabu yao imekuwa
ikionewa kila kukicha.
“Tumemwandikia
barua Malinzi ya kumtaka tukae tuzungumze tuone Simba ina tatizo gani mpaka iwe
inaonewa kila siku, tunataka tulifahamu hilo ili kuondoa hali hii ambayo sasa
imetuchosha,” alisema Manara na kuongeza.
“Tumeitisha
mkutano wetu wa wanachama kwa ajili ya mabadiliko ya katiba, halafu tunasikia
kuna mtu huyu anajiita Mohammed Kiganja (Katibu wa BMT) eti anasema
kitakachoafikiwa siku hiyo wao hawakitambui wakati waziri mwenyewe amekubali.
“Sasa
huyu Kiganja ni nani hasa mpaka atuendeshe kiasi hiki, sisi tunasema, katika
hili hakuna wa kutuzuia, tutafanya mabadiliko ya katiba kama wanachama
wakikubali, hakuna wa kutuingia katika katiba yetu hata kama serikali ilihali
hatuvunji katiba ya nchi.
“Hivi kwa soka la sasa ni nani asiyependa mabadiliko, huyu Kiganja yeye amekuwa akijitokeza kwenye migogoro tu, kwa nini katika maendeleo hayupo, tumefuata sheria zote za kuitisha mkutano na tutaufanya bila ya kizuizi chochote kile,” alimaliza Manara
0 maoni:
Post a Comment