DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, amepiga marufuku wauzaji holela wa samaki na mboga mitaani badala yake
wapeleke katika masoko maalumu
Aidha ameliagiza jeshi la polisi na
halmashauri zote mkoani humu kuwakamata wafanyabiashara watakaokiuka agizo
hilo.
Makonda alitoa kauli hiyo jana,
wakati alipotembelea Soko la Kimataifa la Samaki la Feri na kuzungumza na
wafanyabiashara wa soko hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili
katika Wilaya ya Ilala.
Wafanyabiashara hao walieleza kuwa,
moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na kuzagaa kwa wafanyabiashara
huria wa samaki hususani katika vituo vya mabasi ya daladala na pembezoni mwa
barabara mkoani humo.
Walidai kuwa, hali hiyo inahatarisha
uhai wa soko hilo kwani watu wengi hawafiki kununua samaki katika soko hilo,
badala yake huishia kununua katika vituo vya mabasi na mitaani.
Mfanyabiashara Said Ally alimueleza
mkuu huyo wa mkoa kuwa, masoko huria ya mitaani yanaendelea kushamiri huku
viongozi wa halmashauri na wananchi wakikaa kimya.
Mbali na hayo wafanyabiashara hao
waliomba kuboreshwa kwa miundombinu ya soko hilo ambayo imechakaa licha ya soko
kuwa la kimtaifa.
Kutokana na malalamiko hayo, Makonda
alipiga marufuku biashara ya samaki na mboga mitaani na kumuagiza Kamanda wa
Operesheni, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya kuwashughulikia
wafanyabiashara wote watakao kiuka agizo hilo kuanzia sasa.
0 maoni:
Post a Comment