Uchaguzi mkuu wa Somalia umepangwa kufanyika
tarehe 30 mwezi huu wa Novemba baada ya kuahirishwa mara kadhaa.
Wagombea 18 wanatazamiwa kuchuana kwa ajili ya kiti cha rais mpya wa
Somalia.
Katika uchaguzi huo wawakilishi wa makabila na makundi ya
kijamii ya Somalia watachagua wawakilishi 275 wa Bunge la Taifa na
wawakilishi wengine 57 wa Baraza la Seneti.Wapinzani wawili wakubwa zaidi katika kinyang’anyiro cha kugombea kiti cha rais ni Rais wa sasa wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud na Fadumo Dayib, mmoja kati ya wanawake wawili katika orodha ya majina 18 ya wanaogombea kiti hicho.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi ya Somalia, Omar Mohamed Abdulle amewataka wanasiasa na jumuiya za kimataifa kufanya jitihada za kufanikisha zoezi hilo katika mazingira ya amani na utulivu.
Kwa muda mrefu sasa viongozi wa Somalia na jumuiya za kimataifa zimekuwa zikitoa wito wa kufanyika uchaguzi mkuu nchini Somalia lakini ukosefu amani na usalama umekuwa kizingiti kikuu cha kuitishwa uchaguzi huo. Kwa sababu hiyo uchaguzi mkuu wa Somalia umeakhirishwa mara kadhaa.
Katika uchaguzi wa sasa kila jimbo la serikali ya federali ya Somalia litachagua wawakilisi wa Baraza la Seneti ambao wao pamoja na wale wa Bunge la Taifa wanaochaguliwa na wawakilishi wa koo 14,024 za Somalia watamchagua rais mpya wa nchi hiyo.
Japokuwa mtindo huu wa uchaguzi wa rais usio wa moja kwa moja unakosolewa na baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, lakini ni wazi kuwa iwapo utafanikiwa utatayarisha uwanja mzuri wa kuwepo utawala na mfumo bora zaidi wa uchaguzi utakaowashirikisha moja kwa moja wananchi katika kuchagua kiongozi wa nchi yao, wawakilishi wa Bunge la Taifa na wale wa Baraza la Seneti.
Alaa kulli hal, uchaguzi wa sasa wa Somalia unafanyika katika mazingira magumu huku kundi la kigaidi la al Shabab likiendelea kufanya mauaji na mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu katika maeneo ya umma na taasisi za serikali. Ingawa ushirikiano wa jesh la Somalia na askari wa kulinda Amani wa Umoja wa Afrika (Amisom) katika kupambana na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al Shabab umekuwa na mafanikio ya kiwango fulani, lakini kundi hilo linaendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale na kuua raia wengi wasio na hatia. Kwa msingi huo kuna udharura wa kuwepo ushirikiano mkubwa zaidi wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kung’oa kabisa mzizi wa kundi hilo ambalo limepanua harakati zake hadi katika nchi jirani.
Katika upande mwingine Somalia inasumbuliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kijamii. Nchi hiyo ambayo ina nafasi nzuri ya kijiografia na utajiri wa maliasili, inasumbuliwa sana na umaskini, ufisadi, kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira na ukame. Tatizo la maharamia wa Somalia katika Bahari ya Hindi ambalo limekuwa moja ya changamoto kubwa kwa meli zinazosafirisha bidhaa katika eneo hilo pia limehusishwa na matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa kazi na ajira ambao unawasukuma vijana wengi katika uhalifu.
Ukame na mabadiliko ya hali ya hewa pia yamesababisha uharibifu wa mazao ya kilimo kwa kadiri kwamba, sasa unahatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni tano nchini Somalia. Hali imekuwa mbaya sana kwa kadiri kwamba, hivi karibuni Rais Hassan Sheikh Mohamud wa nchi hiyo aliiomba jamii ya kimataifa kutoa msaada wa dharura kwa ajili ya kukabiliana na ukame na njaa nchini humo.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, hali ya Somalia si nzuri, na katika mazingira kama hayo viongozi wa nchi hiyo wanatarajia kwamba, usalama utaimarishwa zaidi kwa ajili ya kufanyika uchaguzi wa amani utakaowezesha kuundwa Bunge la Taifa na Baraza la Seneti na hatimaye kuunda serikali madhubuti nchini humo.
0 maoni:
Post a Comment