Rais wa Tanzania
John Magufuli amekanusha taarifa ambazo zimekuwa zikienea katika baadhi
ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba amezuia mziigo ya mke
wa Rais Mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete, Mama Salma.
Taarifa
zimekuwa zikidai taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), inayoongozwa
na Mama Salma, imeshindwa kulipia kodi mizigo mikubwa iliyoiingiza
nchini Tanzania na hivyo kuwa hatarini kupigwa mnada.Aidha, habari hizo zilikuwa zimedai Rais Magufuli anahusika kuzuia mizigo hiyo bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.
Taarifa ya ikulu imesema Rais Magufuli hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma.
"Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma Kikwete, tafadhali wale mnaotengeneza uzushi huu acheni mara moja na muacheni Rais Mstaafu Kikwete apumzike," amesema Dkt Magufuli, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.
"Rais Mstaafu Kikwete amefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa hili, amestaafu anapumzika, narudia muacheni apumzike, Serikali haitaendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi huu unaofanywa kwa makusudi ili kuwachafua viongozi wastaafu".
Dkt Magufuli amewataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuacha kuandika na kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake vizingatie weledi na kufuata sheria.
0 maoni:
Post a Comment