Ofisa wa TFF na mkasa wa kipa wa African Sports 1969
Na Zaka Zakazi
Hatimaye mzizi wa fitna umekatwa na aliyepata, kapata…aliyekosa kakosa! Kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji ya shirikisho la soka hapa nchini, TFF, imetoa hukumu juu ya kesi iliyofunga msimu wa 2015/16 na kufungua msimu qa 2016/17…usajili wa mlinzi wa kulia wa, Hassan Ramadhan Kessy, kutoka Simba kwenda Yanga.
Kamati imeikuta na hatia klabu ya Yanga na kuitaka iilipe Simba fidia ya shilingi milioni hamsini pamoja na faini shilingi milioni tatu.
Aya ya mwisho ya taarifa ya TFF juu ya hukumu hiyo inasema – Ofisa wa TTF aliyehusika ama kwa kushirikiana na Uongozi wa Klabu ya Young Africans au kwa kutochukua hatua stahiki kwa wakati apelekwe kwenye mamlaka yake ya nidhamu, yaani, Katibu Mkuu wa TFF ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Huyu ofisa wa TFF ndiyo msingi wa makala hii. Kosa la ofisa huyo liliwahi kufanyika mwaka 1969 na kusababisha balaa.
Mwaka 1969, ligi ya Tanzania, ikiitwa ligi ya taifa, ilikaribia kuvunjika baada ya ‘ofisa’ mmoja wa FAT kuidhinisha usajili wa kipa wa African Sports ya Tanga.
Mzozo ulianza pale Sunderland (Simba) ilipokata rufaa kutaka ipewe ushindi dhidi ya African Sports katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1. Sunderland walilalamika kwamba Sports walimchezesha kipa wa timu ya Ujamaa kwenye mchezo huo. Ujamaa ilikuwa timu kutoka Tanga na ilikuwa ikishiriki ligi ya taifa pia.
Baada ya uchunguzi ikabainika kwamba Sports walipata baraka kutoka FAT kumchezesha kipa huyo kwani kipa wao namba moja alikuwa anaumwa macho na wa akiba alikuwa safarini. Waliiomba FAT iwaruhusu kusajili kipa mwingine…FAT ikakubali bila kujua kipa huyo anaitwa nani na anatoka timu gani!
FAT ilipobaini mapungufu hayo ikakiri kosa. Kosa hili na makosa mengine huko nyuma yakaikera serikali na kuisimamisha FAT yote na kuunda kamati ya mpito.
Sunderland hawakuridhika na maamuzi ya serikali kwani wao shida yao ilikuwa pointi mbili za mchezo ule(wakati huo timu ikishinda hupata pointi na tatu za sasa). Wakasema hawataendelea na ligi kama wasingepewa pointi zao!
Msimamo wa Sunderland ukaleta hofu kwamba yawezekana pambano lao na watani wao Yanga, 03/03/1969 ambalo lingekuwa la kwanza kufanyika uwanja wa taifa, lisingefanyika.
Matumaini yalirejea pale kamati ilipoirudishia Sunderland pesa zao za kukatia rufaa…ikaaminika kwamba rufaa yao ilifanikiwa. Lakini hata hivyo, kamati ikaitupilia mbali rufaa ya Sunderland ikisema kosa la FAT kuiruhusu Sports kumcheza kipa yule halikuwa na athari za moja kwa moja na matokeo.
Sunderland ikanuna na kususia pambano lao la 03/03/1969 dhidi ya Yanga. Kamati ikaipiga Sunderland faini ya shilingi 500/= na kusema kama faini hiyo isingelipwa, timu hiyo ingeondolewa kwenye ligi.
Hofu ya kuvunjika kwa ligi ikazuka na hali ya hewa ikawa imechafuka. Baadaye pande zilizohusika zikakaa na kuyajenga. Sunderland hawakupewa pointi walizozitaka kutoka Sports, hawakulipa faini waliyopigwa na kamati wala hawakuondolewa kwenye ligi.
Mkasa huu pamoja na mkasa wa Francis Mwekalo wa 1986, ni moja ya mikasa ya usajili iliyotikisa nchi!
0 maoni:
Post a Comment