Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Tundu Lissu, amesema ameanza kuogopwa na viongozi wa serikali baada ya jina lake kuwa miongoni mwa majina matano bora ya wagombea wa nafasi ya urais katika Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutokana na misimamo yake ya kuitetea Katiba ya Tanzania.
Akizumgumza na waandishi wa habari Mwanza jana, Lissu alisema tangu atangaze nia yake ya kugombea urais wa TLS ameanza kuogopwa kutokana na kujulikana kwa misimamo yake kuhusu masuala ya sheria, siasa na katiba ya nchi hii.
Alisema TLS ina majukumu makubwa katika nchi ya kulinda utawala wa sheria na wanasheria ndiyo wanaojua kuliko mtu yeyote zinapotungwa sheria mbovu na zile za kikandamizaji, pia wao ndiyo wanapaswa kuwa wa kwanza kuanza kuzipigia kelele sheria hizo.
“Kwa miaka mingi TLS imeongozwa na watu ambao hawafikiri kwamba wajibu wao wa kwanza kulinda utawala wa sheria, wao wanafikiri wajibu wao wa kwanza ni kuwapendeza wanasiasa na matokeo yake TLS imepotea, wanachoogopa ni kwamba hii raha ambayo wameipata miaka yote hii wakati wanasheria wa TLS wakiwa usingizini akija huyu Lissu itaisha,” alisema Lissu.
Alisema aligombea nafasi hiyo baada ya kumsikia Rais Dk. John Magufuli akizungumza mbele ya watanzania kwamba wakili yeyote atakayewatetea watuhumiwa wanaokutwa na dawa ya kulevya au nyara za serikali wakamatwe na kuwekwa ndani.
Alisema aliposikia kauli hiyo alicheka na kusema sasa ni wakati wa yeye kuwa rais wa TLS ili kauli za aina hiyo zikome na siku mbili kabla ya Rais Dk. John Magufuli kutoa kauli hiyo, Bunge lilipitisha sheria ya msaada wa sheria.
“Sheria hiyo inasema mtu yeyote anayefunguliwa kesi ya jinai, au madai kama ni maskini hana uwezo wa kumlipa wakili atapatiwa huduma hiyo na wakili atalipwa na mtendaji mkuu wa mahakama.
“Sheria hiyo inampatia haki mwananchi yeyote atakayekuwa na kesi ya mauaji, pembe za ndovu au dawa za kulevya kupata wakili atakayelipwa na serikali.
“Siku mbili baadaye Rais anakinzana na sheria hiyo nilishangaa kweli. Tayari sheria hiyo imetungwa ni jambo muhimu kweli kwa sababu katika nchi hii watu wanasingiziwa sana, kwenye maegereza nyingi nchini wamejazana wananchi ambao hawana hatia na wapo huko kwa sababu hawakuwa na mawakili wa kuwatetea,” alisema Lissu.
Lissu alisema endapo atachaguliwa kuwa rais wa TLS atahakikisha sheria ya msaada wa sheria inatekelezwa.
Kuhusu hoja ya Waziri wa katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ya kutishia kukifuta chama hicho hicho kwa kuwa kimeanza kujiingiza katika masuala ya siasa, Lissu alisema wanaoleta hoja za kutaka kukifuta chama hicho kama ni wanasheria ujuzi wao wa sheria ni wa shaka lakini kama ni wasiojua sheria wanasamehewa.
Alisema sheria ya iliyoanzisha TLS inasema mwanachama yeyote aliyekidhi vigezo vya chama hicho ana haki ya kuwa mgombea wa nafasi yoyote ya uongozi na haijasema ukiwa mwanachama wa chama chochote cha siasa unapungukiwa sifa ya kugombea.
“Watu wanazungumza kana kwamba ni makosa mwanasheria kuwa mwanasiasa, katika nchi hii katiba imeruhusu siasa za vyama vingi, kuwa wanachamaau kiongozi wa chama.
“Kuwa tu mwanachama una kuwa na fursa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi serikalini lakini sasa watu wanataka kuaminishwa kuwa ukiwa mwanasiasa huna haki,” alisema
from Blogger http://ift.tt/2kTYBJG
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment