TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI



TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS 
RELEASE” TAREHE 06.03.2017.






Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Kufuatia mapambano yanayoendelea nchi nzima dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-

KUUAWA KWA WATU WANAOSADIKIWA KUWA MAJAMBAZI NA KUPATIKANA KWA SILAHA.

Mnamo tarehe 05.03.2017 majira ya saa 21:30 usiku huko katika eneo la mlima nyoka, Uyole, Jijini Mbeya katika barabara ya Mbeya/Njombe, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipambana na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wanaokadiriwa kuwa watano [05] wakiwa na silaha na kufanikiwa kuwaua majambazi wawili [02] wenye umri wa miaka kati ya 30-35.

Katika tukio hilo silaha tatu zilikamatwa ambazo ni Pistol moja yenye namba 550285 na magobole mawili pamoja na risasi moja ya pistol ambazo zilikuwa zikitumiwa na majambazi hayo.

Majambazi hao walifika katika eneo hilo kwa lengo la kufanya uhalifu ambapo Polisi walipata taarifa na kufika eneo hilo. Eneo la Mlima Nyoka ni eneo lenye mlima na mteremko mkali hivyo magari hulazimika kupunguza mwendo na kupanda mlima taratibu hivyo wahalifu hutumia nafasi hiyo kudandia magari na kufanya uhalifu.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa utambuzi. ufuatiliaji unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa wahalifu hao.

KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA [BHANGI]
Katika Operesheni na Misako inayoendelea kuhusiana na watu wanaojihusisha na usafirishaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kukamata watu wawili wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya [Mateja] ambao ni 1.  EDSON MWANGOKA [32] Mkazi wa Mama John na 2. ABRAHAM EZEKIA [20] Mkazi wa Airport.


Aidha katika Oparesheni hiyo walikamatwa watu sita wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi ambao ni
1. GWAMAKA SHWAIBU [30] Mkazi wa Mwakibete
2. LAZARO AFRIKA [30] mkazi wa Ngyeke
3. DAUDI MSOMA [30] mkazi wa mbalizi
4. JOSEPH MWAMBUNGU [23] mkazi wa Sistila
5. JOHN MNANDI [28] mkazi wa Sistila
6. DAVID PROTAS [20] mkazi wa Sistila

Bhangi yenye jumla ya uzito wa gram 535 ilikamatwa. Watuhumiwa ni wauzaji wa dawa za kulevya na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya mnamo tarehe 04.03.2017 lilifanya Oparesheni dhidi ya dawa za kulevya. Oparesheni ilifanyika huko katika milima ya Mbeya, kijiji cha Ihombe na katika milima ya Uwanji, iliyopo Kata ya Chimala tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali.

Katika Oparesheni hizo, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata mashamba makubwa ya Bhangi. Shamba la bhangi lenye ukubwa wa ekari tatu lilikamatwa katika Kijiji cha Ihombe likiwa limelimwa Bhangi pamoja na mahindi. Pia shamba la Bhangi lenye ukubwa wa robo ekari likiwa limelimwa bhangi pamoja na mahindi lilikamatwa katika milima ya Uwanji Wilaya ya Mbarali.

Mashamba yote ya Bhangi yaliteketezwa kwa kuchomwa moto. Msako unaendelea kuwatafuta wamiliki wa mashamba hayo kwani katika Oparesheni hizo walikimbia na kutelekeza mashamba hayo.

KUPATIKANA NA POMBE MOSHI [GONGO]

Kuanzia tarehe 01.03.2017 hadi tarehe 05.03.2017 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya misako katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na Pombe Moshi [Gongo] na mitambo miwili ya kutengenezea Pombe hiyo.

Watuhumiwa waliokamatwa katika misako hiyo ni
1. ELIZABETH BONIFACE [40] mkazi wa isoko – Wilaya ya Chunya
2. NAOMI SAMANDANGWA [50] mkazi wa Isoko - Wilaya ya Chunya
3. ENEA DICKSON [30] mkazi wa Kabanga – Wilaya ya Kyela

Watuhumiwa walikutwa na Pombe Moshi [Gongo] kiasi cha lita 58 na mitambo miwili ya kutengenezea pombe hiyo. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika. 







Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na tukio 01 la ajali ya kifo kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 05.03.2017 majira ya saa 08:10 asubuhi huko katika Kijiji cha Sinjilili, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Chunya kuelekea Mbeya, Gari lenye namba za usajili T 489 BZW Toyota Progress Saloon iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika iliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha ANNA KIBALI [50] Muuguzi Hospitali ya Wilaya ya Chunya na Mkazi wa Sinjilili

Aidha katika ajali hiyo watu watatu walijeruhiwa ambao ni 1. PATRISIA CHISOTI [44] muuguzi Hospitali ya Wilaya ya Chunya na Mkazi wa Chunya ambaye aliumia kichwani na kifua 2. DAVID LOBISON [24] Mkazi wa Sinjilili ambaye aliumia kifua na kichwani na 3. SADOKI ERASTO [32] mfanyabiashara na Mkazi wa Chunya ambaye aliumia kifuani na mikono yote. 

Chanzo cha ajali ni mwendo kasi. Dereva wa gari alikimbia baada ya tukio.  Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospital ya Wilaya ya Chunya na majeruhi wanaendelea kupata matibabu Hospitalini hapo. Juhudi za kumtafuta dereva zinaendelea.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na tukio 01 la mauaji kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 04.03.2017 majira ya saa 22:30 usiku huko katika Kijiji cha Ntaganoijombe, Kata ya Ijombe, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi na Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NSAALU MWANGOKA, [82] Mkazi wa Ijombe aligundulika kuuawa na mtu/watu wasiofahamika kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali karibu na jicho la kushoto na mdomoni upande wa kushoto na kupelekea damu nyingi kumwagika na kusababisha kifo chake.

Chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika. Aidha kufuatia tukio hilo watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa mahojiano ambao ni 1. ELIAS JAPHET [27] 2. CLEMENCE WILIAM [40] na 3. TITO BARNABAS [32] wote wakazi wa Ijombe ambao wanaishi majirani wa marehemu.

Marehemu alikuwa akiishi nyumbani kwake pekee yake na mwili wake ulikutwa na majeraha makubwa sehemu ya usoni karibu na jicho la kushoto na sehemu ya  mdomoni upande wa kushoto. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Igawilo Uyole. Upelelezi unaendelea





WITO:

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi EMANUEL G. LUKULA anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu na mtandao wa wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Aidha Kamanda LUKULA anatoa wito kwa wananchi kufanya kazi na kuacha kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu kwa ujumla kwani Jeshi la Polisi halitavumilia aina yoyote ya uhalifu.


Imesainiwa na:
[EMANUEL G. LUKULA - ACP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.



Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment