Mwinyi alionesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya kombe la Chalenji iliyofanyika Kenya wakati akiitumikia timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na kuisaidia kikosi hicho kumaliza nafasi ya pili baada ya kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Kenya.
“Ni kweli nimeandika barua kuomba kuondoka Yanga kwa sababu sipati nafasi ya kucheza, jana jioni baba ambaye ndio meneja wangu aliifikisha barua hiyo kwa kwa viongozi,” Mwinyi ameiambia shaffihdauda.co.tz.
“Mimi ninaamini nina uwezo mkubwa lakini nashangaa nimeendelea kukaa nje kwa muda mrefu. Kama unakumbuka nimecheza mechi nyingi msimu uliopita kuanzia VPL, FA, na hata michuano ya CAF iweje leo kiwango kimeshuka hadi kukosa kabisa nafasi?”
“Namshukuru sana kocha wangu wa timu ya taifa ya Zanzibar Hemed Morocco kwa kuniamini na kuniita kwenye kikosi chake kisha kunipa nafasi, hii inaonesha ni namna gani alivyokuwa na imani na uwezo wangu.”
“Nadhani kila mtu aliona nilichofanya kwenye mashindano ya Chalenji licha kwamba nimekuwa nje kwa muda mrefu. Kuchaguliwa kwenye kikosi cha wachezaji bora wa Chalenji pia inadhihirisha uwezo wangu.”
Tangu Gadiel Michael asajiliwe Yanga akitokea Azam, Mwinyi amekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza.
Mlinzi huyo amethibitisha kwamba, AFC Leopards ya Kenya imeonesha kuvutiwa na uwezo wake na ipo tayari kumsajili kwa ajili ya kuitumikia.
“AFC Leopards imeonesha nia ya kutaka kunisajili ndio maana nimeomba kuondoka Yanga, kama sina nafasi wala situmiki bora niende sehemu nyingine ambako naweza kucheza ili kuendelea kulinda kipaji changu kwa sababu sisi wachezaji mpira ndio kazi yetu.”
0 maoni:
Post a Comment