Dk Ngereza alisema kuwa lita moja ya mafuta hayo, huuzwa hadi Sh 50,000, wakati robo lita (ujazo wa mililita 250) huuzwa kati ya Sh 12,000 hadi Sh 15,000, na hayana kemikali yoyote.
Alisema mafuta hayo ni moja ya mafuta, yanayouzwa kwa bei ya juu na uhitaji wake katika soko la kimataifa ni mkubwa. Kwa mujibu wa mtafiti huyo, zao la nazi ambalo Tanzania ndiye mzalishaji namba moja Afrika na namba kumi duniani, lina faida nyingi katika maisha ya watu na kuleta ustawi katika mazingira yao.
Alisema mti wa mnazi, unajulikana kama mti wa uhai kutokana na bidhaa nyingi zinazopatikana katika zao hilo. “Bidhaa nyingine zinazotokana na zao la nazi ni makuti kwa ajili ya kuezeka nyumba, fagio, vikapu, mbao, samani, sakafu, karatasi na dawa za kufukuza mbu.
Pia mafuta mwali ya nazi ni moja ya mafuta yanayouzwa bei ya ghali sana na yana uhitaji mkubwa katika soko la kimataifa,” alieleza Dk Ngereza. Mafuta hayo ya mwali ya nazi, hutumika kuondoa fangasi mwilini, kulinda ngozi dhidi ya mionzi ya jua, kuondoa mwasho mwilini, kulainisha nywele, lakini pia hutumika kwenye uandaaji wa vipodozi na virutubisho katika vyakula.
Uzalishaji wa nazi Kwa mujibu wa Dk Ngereza, Tanzania inaongoza kwa uzalishaji wa zao la nazi barani Afrika. Eneo la uzalishaji wa minazi linakadiriwa kuwa hekta 700,000. Imeelezwa kuwa wastani wa uzalishaji wa nazi kwa hekta ni nazi 7,600 ambazo ni sawa na wastani wa tani 540,000.
Kuhusu takwimu za uzalishaji wa nazi nchini kuanzia mwaka 2011 hadi 2014, Kituo hicho cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni kilisema kuwa kwa mwaka 2011 eneo lililovunwa nazi lilikuwa hekta 670,000, mwaka 2012 hekta 680,000, mwaka 2013 hekta 680,000 na mwaka 2014 hekta 708,449.
“Pia uzalishaji kwa hekta ulikuwa nazi 8,209 mwaka 2011, mwaka 2012 nazi 7,647, mwaka 2013 nazi 7,794 na mwaka 2014 nazi 7,629. Katika kipindi hicho pia uzalishaji kwa tani ulikuwa tani 550,000 mwaka 2011, mwaka 2012 tani 520,000, mwaka 2013 tani 530,000 na tani 540,455 mwaka 2014,” alieleza Dk Ngereza.
Maeneo yanayozalisha nazi Kwa mujibu wa Kituo hicho cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni, zao la nazi ambalo hutoa bidhaa mbalimbali, hulimwa kwa wingi kwenye Ukanda wa Pwani hapa nchini.
Maeneo hayo yanayolima nazi kwa wingi ni pamoja na Pangani, Muheza, Korogwe, Mkuranga, Kisarawe, Kibaha, Chanika mkoani Dar es Salaam, Mafia, Kilwa, Rufiji, Morogoro Vijijini, Lindi, Mtwara Vijijini na Zanzibar.
Soko la nazi Licha ya Tanzania kuongoza kwa uzalishaji wa nazi barani Afrika, imeelezwa kuwa kiwango cha nazi kinachozalishwa, bado hakikidhi mahitaji ya soko la hapa nchini ukiacha mbali soko la nje.
Dk Ngereza alisema kuwa wastani wa mahitaji ya nazi kwa kaya ni nazi nne kwa siku. Alisema kwa kuwa soko la ndani la nazi bado ni kubwa, imekuwa siyo rahisi kuwa na soko la zao hilo nje ya nchi.
Alisema mara nyingine wakati wa kipindi cha Mfungo Mtukufu wa Ramadhani, baadhi ya nazi huagizwa kutoka Mombasa, Kenya ili kukidhi mahitaji. Aidha, uhaba wa nazi pia unasababishwa na kuwepo kwa soko la kubwa la madafu hapa nchini.
Kwa mujibu wa Dk Ngereza, dafu moja huuzwa Sh 1,000 wakati nazi huuzwa kati ya Sh 600 na Sh 700. Hali hiyo imeelezwa kuwafanya wazalishaji wengi na wauzaji wa rejareja, kupenda kufanya biashara ya madafu zaidi kuliko nazi kwa kuwa bei yake ni nzuri.
Aidha, Dk Ngereza alisema kuwa wajasiriamali wa biashara ya nazi, wanatakiwa kuongeza thamani ya zao hilo kwa kusindika mafuta badala ya kuuza nazi kama ilivyo. Alisema nazi 20 zikisindikwa, zinatoa mafuta ya mwali ya nazi lita moja, ambayo yakiuzwa huingiza faida ya Sh 50,000, wakati idadi hiyo hiyo ya nazi zikiuzwa kwa bei ya reja reja ya Sh 700 huingiza Sh 14,000.
Changamoto ya zao la nazi Kituo hicho cha utafiti kimesema kuwa minazi inayolimwa nchini, mingi ni ile ya kienyeji au ya asili, kwa kuwa inaweza kuhimili hali ya hewa tofauti na mbegu nyingine za kigeni.
Imeelezwa kuwa inachukua miezi 8 hadi 9 kuotesha miche ya minazi; na inapopandwa huchukua miaka 6 hadi 7 kuanza kuvunwa. Minazi hiyo ya asili, ina uwezo wa kuzaa nazi hadi 30 kwa kori moja na ina uwezo wa kuishi kati ya miaka 60 hadi 70.
Kwa mujibu wa Dk Ngereza, zao la mnazi linastawi vizuri zaidi kwenye udongo wa tifutifu na linahitaji milimita 2,000 za mvua kwa mwaka. Alisema moja ya changamoto ya zao hilo hapa nchini ni uhaba wa mvua, ambao pia husababisha minazi kupukutisha maua, lakini pia kushambuliwa na wadudu waharibifu.
Ripoti ya Kimataifa Mbali na Tanzania kuwa ya kwanza kwa uzalishaji wa zao la nazi barani Afrika, pia imetajwa kuwa nchi ya kumi miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao la nazi duniani. Nchi iliyotajwa kuongoza kwa uzalishaji wa nazi duniani ni Indonesia ikifuatiwa na Ufilipino, India, Sri Lanka, Brazil, Thailand, Vietnam, Mexico na Papua New Guinea.
0 maoni:
Post a Comment