WABUNGE wametoa kilio chao wakiiomba serikali ya Rais John Magufuli
ichukue hatua za makusudi na za haraka kuziba nafasi za watumishi wa
afya ambao wengi wametumbuliwa kutokana na kutumia vyeti feki katika
ajira yao.
Sekta ya afya nchini Tanzania ni kati ya zile zilizoathirika zaidi
kufuatia zoezi la kuhakiki vyeti feki, baadhi ya wabunge wamesema.Wabunge hao wametoa kilio chao kutokana na watumishi wengi waliotumbuliwa baada ya kubainika kuwa na vyeti feki kubainika wako katika sekta hiyo, ambayo inaupungufu wa madaktari na wahudumu mbalimbali wa afya.
Lakini wengi wa wananchi pia wanakiri kulikuwepo na hatari inayowakabili wananchi kwa huduma hiyo kutolewa na wataalamu feki katika sekta hii ambayo ni muhimu kwa maisha ya watu,
Baadhi ya vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa hii ni ishara tosha ya hatari iliyokuwa ikiwakabili wananchi kwa kuhudumiwa na watalaam feki na jinsi isivyokuwa sahihi kwa watu hawa kutetewa.
Aidha wameishauri serikali kuanza kutengeneza mfumo ambao watalaam watakuwa wanaajiriwa kutokea vyuoni; kuweka mfumo wa kumbukumbu imara zinazo onyesha wahitimu mbalimbali katika madaraja mbalimbali.
Wamesema kukiwa na mifumo inayofanya kazi na endelevu wa kufuatilia na kutathmini wa utendaji wa kada mbalimbali bila kusubiria rais au watawala kuingilia kati suala hili lingekuwa limedhibitiwa mapema kabisa kabla halijasababisha mtafaruku huu.
Mapema mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea repoti kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ikionyesha watumishi wa umma 9,932 kutoka sekta mbalimbali.
Mmoja ya mambo yaliyojitokeza katika repoti hiyo aliopewa rais ni kuwepo wafanyakazi wa afya ambao walibainika kuwa na vyeti feki vya kidato cha nne na cha sita na vile vya ualimu.
Kutokana na orodha hiyo iliyohusisha watumishi kutoka Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na Ofisi ya Rais Utumishi, imewagusa watumishi wa sekta ya afya katika hospitali, vituo vya afya na hasa kwenye zahanati.
Wiki iliyopita Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro aliwaambia waandishi wa habari kwamba serikali itajaza nafasi hizo haraka sana.
Vyanzo vya habari na wabunge wameripoti kuwa sekta ya afya imeathiriwa sana na kuondoka kwa watumishi hao walioghushi vyeti ambao wametakiwa kuondoka kwa hiari yao kabla ya Mei 15, mwaka huu.
Pia serikali imetoa agizo kuwa watakao kaidi kuondoka wenyewe watakabiliwa na mashitaka ambayo ukitiwa hatiani adhabu yake ni kifungo cha miaka saba jela.
Akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto bungeni jana, Mbunge wa Mchinga, Hamid Bobali (CUF) amesema katika jimbo lake, zahanati mbili tayari zimefungwa kutokana na wafanyakazi wake kutumbuliwa.
Bobali ameongeza kusema serikali inatakiwa kufanya jitihada kunusuru afya za wananchi wa maeneo hayo kutokana na kukosa huduma ya afya hivi sasa. Alisema licha ya Jimbo na Mkoa wa Lindi kuwa na watumishi wa kada ya udaktari wachache, kutumbuliwa kwa wafanyakazi hao kumechangia kuathiri huduma za afya zaidi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Lathifar Chande (Chadema) amesema kutokana na tumbua tumbua wafanyakazi wa afya wamepungua imesabibisha kuzorotesha huduma za afya katika Hospitali ya Mkoa ya Lindi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Jasmin Bunga (CCM) amesema serikali inatakiwa kuboresha vyuo vya maendeleo ya jamii ili kuhakikisha watumishi wanapatikana wa kutosha wa kutoa huduma hiyo.
0 maoni:
Post a Comment