Bodaboda wameguka, Msigwa Kuchangia Chama Kipya

  • TSH MILIONI 3 NA BODABODA 10


Mchungaji Msigwa akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na madereva wa bodaboda wanaotaka kuanzisha chama kipya
Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda na Bajaj Iringa, Mwambope Joseph naye alikuwa na mkutano na wanachama wake


Hali ilivyokuwa nje ya ukumbi ambao mkutano wa Mchungaji Msigwa ulifanyika
Mwenyekiti wa Bodaboda (wa tatu kulia) akiondolewa na wanachama wake katika eneo la mkutano wa Mchungaji Msigwa. Walioko kwenye gari ni askari Polisi waliofika kutuliza vuta nikuvute iliyojitokeza
Hali ilivyokuwa katika uwanja wa Mwembetogwa baada ya Mwenyekiti wa Bodaboda na wanaomtii walipoondoka katika mkutano wa Mchungaji Msigwa na kufanya mkutano na wanahabari
Huyu ndiye Jarome Mwakipesile atakayekuwa kiungo cha uanzishaji wa chama kipya na ofisi ya mbunge wa Iringa Mjini
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Boda Boda na Bajaj Iringa, Ezekiel Lukosi akisisitiza jambo
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ameahidi kuchangia Sh Milioni 3 taslimu na pikipiki (bodaboda) kumi kwa chama kipya cha bodaboda kinachotarajia kuanzishwa kwa uratibu wa ofisi yake wakati wowote kuanzia sasa.

Endapo azma hiyo itatimia manispaa ya Iringa itakuwa na vyama viwili tofauti vya madereva hao vinavyoelezwa na baadhi ya wadau kwamba vitatofautiana kwa mitizamo ya itikadi za kisiasa.

Chama pekee kinachotambulika hivisasa ni kile Chama cha Bodaboda na Bajaj Iringa kinachotuhumiwa na baadhi ya madereva walioamua kuanzisha chama kingine kwa uratibu wa ofisi ya mbunge huyo kwamba kinaendeshwa kwa kuzingatia itikadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika mazingira yaliyoashiria mgawanyiko huo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini aliitisha mkutano na madereva wa bodaboda mapema hii leo katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo, huku Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda na Bajaj Iringa, Mwambope Joseph naye akiitisha kikao na madereva hao katika uwanja wa Mwembetogwa, Makorongoni.

Katika mkutano wa Makorongoni, Joseph alimtuhumu Mchungaji Msigwa akisema anataka kudhohofisha maslai ya madereva hao kwa kuwagawa kisiasa.

“Mchungaji alinipigia simu Agosti 18 akinieleza kwamba anataka mkutano na madereva wa bodaboda na tukakubalina akutane na viongozi jumatatu ya leo kabla ya mkutano huo uliokuwa ufanyike kesho jumanne,” alisema.

Alisema katika mazungumzo yao Mchungaji Msigwa aliahidi kuchangia Sh Milioni 10 kama mchango wake katika harakati za bodaboda hao za kujileleta maendeleo yao.

Badala ya kukutana na viongozi, Joseph alisema Mchungaji Msigwa aliitisha kinyemela mkutano na madereva wa bodaboda na bajaj hii leo bila kuwashirikisha huku akiwa na ajenda ya kuwagawa.

Alisema Chama cha Bodaboda na Bajaj Iringa hakikuanzishwa kwa kuzingatia itikadi ya CCM kama inavyoelezwa japokuwa hakizuii madereva wenye itikadi hiyo na ya vyama vingine kujiunga nacho.

“Akijua kwamba leo tumepanga kukutana ili tuwaeleze bodaboda kwamba kesho tutakuwa na mkutano naye, kaamua kupitia mlango wa nyuma ili atimize azma yake ya kuanzisha chama kingine cha bodaboda wa kushirikiana na afisa mmoja wa mwanamke wa halmashauri ya manispaa ambaye sitamtaja,” alisema na kuwaruhusu madereva hao kwenda katika mkutano ulioitishwa na Mchungaji Msigwa ili wakahoji kulikoni.

Baada ya madereva hao zaidi ya 100 kufika katika ukumbi ambao Mchungaji Msigwa alikuwa akiendelea na mkutano wake na madereva wengine, Mwenyekiti huyo alizuiwa kuingia kwa kile kilichoelezwa kwamba atasababisha vurugu.

Taarifa ya vuta nikuvute baina ya pande hizo mbili ilifika mezani mwa Polisi  waliotuma makachero wake waliokuja na kusaidia kutuliza hali hiyo kwa kumuondoa mwenyekiti huyo wa bodaboda.

Madereva waliochangia katika mkutano huo walisema hawataki kuendelea na chama hicho kwa madai kwamba kina muelekeo wa chama fulani cha siasa, taarifa zake za mapato na matumizi ni ngumu kuzipata, viongozi wake ni wababe na hakifanyi mikutano kwa mujibu wa katiba.

Katika utetezi wake, Joseph alisema tuhuma dhidi ya chama na uongozi wake sio za kweli bali zinakuzwa ili kujenga chuki dhidi yake.

Mwambope alisema chama hicho kilianzishwa kikiwa na wanachama 38 waliongia kwa ada ya Sh3,000 kila mmoja na kwa mara ywa kwanza kilifanya mkutano wake Agosti 31, mwaka jana.

Alisema kwa mujibu wa katiba yao, mkutano mkuu wa chama hicho unakutana mara moja kila mwaka na kwamba Agosti 31, mwaka huu watakutana katika Mkutano Mkuu wa pili ambao mbali na mambo mengine utapokea taarifa mbalimbali za chama zikiwemo za mapato na matumizi.

Hata hivyo Joseph alisema pamoja na kwamba manispaa ya Iringa ina madereva zaidi ya 1,000 na wengi wao wakiwa wamesomeshwa udereva na mlezi wao, Salim Asas, chama hicho kina wanachama 171 tu.

“Hao ndio wenye haki na chama hiki, hao ndio wanaostahili kupata taarifa zote za chama chao. Na tutakapoistisha mkutano mkuu hao ndio watakaohudhuria. Madereva wengine tunashirikiana nao kama ndugu na wadau tuliopo katika sekta moja ya usafirishaji na wenye matatizo yanayofanana,” alisema.

Alisema katika mazingira ya kutatanisha baadhi ya madereva wasio wanachama wamekuwa wakifanya kila wanaloweza kwa kushirikiana na mbunge huyo kudhohofisha umoja wao.

Alisema wengi wa madereva waliokutana katika mkutano wa Mchungaji Msigwa sio wanachama wa chama hicho, hawajui katiba ya chama hicho na ndio maana wanatoa lawama zisizo na msingi. 

“Mheshimiwa Mbunge umetuita hapa na tunaomba upokee ombi letu la kusutusaidia kuanzisha chama kipya,” alisema Chadi Michaelm mmoja wa madereva aliyeshiriki mkutano wa Mchungaji Msigwa.

Ombi la Michael lilirudiwa na Gidion Kamugisha, Tabibu Mwakamanga, Kevin Charles, Stanley Mshana na wengine waliopata fursa ya kutoa dukuduku zao.

Katika majibu yake kwa madereva hao Mchungaji Msigwa alisema; “niko tayari kusaidia uanzishaji wa chama kipya lakini ni lazima kiwe na viongozi waadilifu watakaokuwa wanaitisha vikao na kutoa taarifa zote za chama zikiwemo za mapato na matumizi.”

Alisema utayari wake wa kufanya hivyo hauna maana anataka kuwatumiakia kisiasa madereva hao au wawe wafuasi wake.

“Msikubali mtumike, wala mimi msikubali niwatumie. Nitafadhili uanzishaji wa chama kipya lakini niwahakikishie sitawaweka mfukoni. Na tukifanikiwa msitoke na kwenda kuwafanyia fujo wenzenu. Vyama hivi ni vya hiari, kama hukubaliani na taratibu zake jitoe na kajiunge na kingine,” alisema.

Alisema atakipa chama hicho kipya sh Milioni 3 na mpaka Februari mwakani atawasaidia bodaboda kumi sio kwa lengo la kujihakikishia kura kwa vijana hao katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani bali kwasababu anaguswa na matatizo yao.

“Mambo ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani maamuzi yako mikononi mwenu, nasema ya mwakani mtajua wenyewe kama mnipe au msinipe, mimi nimewaita kutekeleza majukumu yangu ya kibunge,” alisema.

Pamoja na kuasaidia uanzishwaji wa chama hicho, Mchungaji Msigwa aliwataka madereva hao kuzingatia taratibu za biashara yao ya usafirishaji.

“Zingatieni kanuni, za usafirishaji, mimi kama mbunge ni lazima niwe fair, bodaboda, taxi, daladala na maroli ni lazima wote wapate nafasi sawa kwa mujibu wa taratibu za kufanya biashara yao, maana sisi wote ni watanzania, tukisema kazi hii iwe ya bodaboda pekee yao mimi nitakuwa kiongozi mbaya,” alisema.

Katika harakati zao za kuanzisha chama kipya madereva hao walimteua dereva mwenzao waliyemtaja kwa jina la Jarome Mwakipesile kwamba ndiye atakeye kuwa akiratibu shughuli za uanzishwaji wa chama hicho kwa upande wao.

Akikubali uteuzi huo, Mwakipesile alisema watakutana Jumapili ijayo ili kuanza mkakati wa kupata uongozi wa muda wa chama na kupanga utekelezaji wa taraibu zingine kwa kushirikiana na ofisi ya mbunge.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment