WZIRI Mkuu wa Ufaransa, Manuel Valls, ametangaza kwamba serikali ya nchi hiyo inajiuzulu. Baraza jipya la mawaziri inatarajiwa kutangazwa Jumanne (26.08.2014). Hatua hii ni pigo kwa rais Francois Hollande.
Kujiuzulu kwa serikali kunakuja baada ya mgogoro katika baraza la mawaziri kuhusu uchumi wa nchi. Hapo awali, waziri wa uchumi Arnaud Montebourg aliikosoa serikali kwa sera zake za kifedha. Montebourg alisema ana mashaka kama sera za Umoja wa Ulaya za kubana matumizi kweli zitasaidia kuuinua uchumi wa Ufaransa. Montebourg alimtaka rais Hollande na Waziri Mkuu Valls wafanye mabadiliko ya kimsingi katika sera ya kiuchumi ya Ufaransa.
Hollande achukiwa na wengi
Waziri wa uchumi Arnaund Monteborug alianzisha majadala kuhusu sera za kubana matumizi
Katika mahojiano na gazeti la Le Monde la Ufaransa Montebourg
aliitaka Ufaransa iwe na msimamo dhidi ya Ujerumani. Kwa muda mrefu
serikali ya Kansela Angela Merkel
imekuwa ikiziwekea nchi za Umoja wa Ulaya shinikizo ili ziweke mipango
madhubuti ya kubana matumzi. Kwa maoni ya Montebourg, raia wa Ufaransa
wakiwapigia kura wanasiasa wao, itakuwa kama vile wanazipigia kura sera
za kiuchumi za Ujerumani.Kufuatia matamshi hayo ya Montebourg, waziri mkuu Valls akapeleka ombi la kujiuzulu kwa serikali kwa rais Hollande. Ukosoaji wa Montebourg ulitibua hasira za chama tawala cha kisoshialisti, wengi wakisema kuwa kazi ya waziri wa uchumi ni kuiunga mkono serikali yake na si kuikosoa. Msemaji wa chama hicho aliliambia gazeti la Le Figaro la Ufaransa kuwa Montebourg hana jukumu la kuanzisha mjadala bali kuisaidia Ufaransa iinuke tena kiuchumi.
Kwa maoni ya wachambuzi wa kisiasa, hatua hii ni pigo kubwa kwa Francois Hollande. Miezi mitano tu imepita tangu alipojikuta katika hali kama hii. Serikali ilijiuzulu baada ya chama kisoshialisti kupata kura chache katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Kwa sasa duru zinaonyesha kuwa katika miaka 50 iliyopita, hakuna rais aliyechukiwa na raia wake kama Hollande.
0 maoni:
Post a Comment