Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania,
tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es Salaam , tumepata
fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika
Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalumu la
Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:
Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ambayo ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko hayo na
kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao,
upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.
Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa
nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya
wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki
kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa tovuti iliyokuwa na
kumbukumbu za Tume na maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa
Tume iliandaa rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda
kizalendo na kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini
zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na
kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili
linatufundisha kuwa Katiba ni maridhiano na si jambo la masilahi ya kisiasa, bali ni suala la masilahi ya wananchi.
Tunaamini kuwa kila mjumbe wa kamati ya
kukusanya maoni ya wananchi aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi
waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa
au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.
Baada ya Tume kuwasilisha rasimu kwenye
Bunge Maalumu la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa
wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya
Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya
masilahi kwa wananchi, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa
yanadhihirisha hili:
Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea.
Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya
rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga
na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona
Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa
mbalimbali ambazo wananchi hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha
baina ya kinachojadiliwa bungeni na kilichomo katika rasimu na
viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na
kwa masilahi ya nani?
Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia
kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu
ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata
Katiba bora
ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa wabunge wa Chama Tawala
(CCM), badala ya kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa
Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya wananchi.
Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba
imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha
maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge
Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake.
Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao
vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa Katiba ni matokeo
ya tendo la maridhiano na si suala la masilahi ya kikundi cha watu
wachache.
Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa
BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na
wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais,
uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na
kuwezesha maoni na masilahi ya chama tawala kwa uongozi wa kikundi cha
wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama
mapendekezo ya Katiba Mpya kwa nia ya kulinda masilahi binafsi au ya
makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya
uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;
1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na
Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake
zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza
na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.
2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi
kufutwa na kudharauliwa na chama tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la
Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika
Rasimu ya Katiba na siyo kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.
3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe
ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano mwafaka, uchaguzi mkuu
na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977
yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka
kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye
kuendelea na mchakato wa Katiba.
4. Kwamba baada ya Bunge Maalumu la
Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi
kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia
ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi katika
Bunge la Katiba.5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni
yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa
kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni
wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba
inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa
nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu
maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na
wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa
rasmi.
Jukwaa la Wakristo Tanzania na
Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais
kwamba amani ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi
hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato
unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha
sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri mshikamano,
umoja na amani ya Taifa letu.
Ifahamike kuwa wananchi wa Tanzania wako
juu ya Wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba
uepushe wananchi wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama Cha Mapinduzi
kwa kuwa tu chama hicho kimeyapuuza na kimekataa maoni yao waliyotoa kwa
dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.
“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu
katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye
yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na
fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia,
wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno,
wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye
kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu,
bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)
Ikumbukwe kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba
ni waraka halali na rasmi na ndiyo mawazo ya Watanzania na tunahimiza
kuwa Katiba ni ya wananchi na inahitaji maridhiano na sio ubabe.
Imetolewa
na Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal
Churches of Tanzania (CPCT) Christian Council of Tanzania (CCT) The
Seventh Day Adventists (SDA)
0 maoni:
Post a Comment