1. Mwandishi
Yussuf Shoka Hamad (kulia) akiwa na Professa Said Ahmed Muhamed ali[omtembelea
nyumbani kwake Limbani Wete hivi karibuni.
Na: Ali Othman Ali
Mwandishi anayechipukia kwa
kasi katika tasnia ya fasihi ya Kiswahili ambaye pia ni Mhadhiri wa Kiswahili
katika Chuo Kikuu Cha London, SOAS na Cambridge nchini Uingereza, Bwana Yussuf
Shoka Hamad, hivi karibuni anatarajia kutoa kitabu chake kipya na cha kwanza
kuchapishwa kinachoitwa; ‘Paka wa Binti
Hatibu na Hadithi Nyingine’.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii kwa simu kutoka nyumbani kwake jijini London, Bwana Yussuf
alisema; ‘ Msomi kama binadamu hufa, huzikwa na husahaulika kama watu wengine
wengi. Lakini msomi kama mwanataaluma na mwandishi hafi, hazikwi, na wala
hawezi kusahaulika kwani mawazo, fikra na falsafa zake hubakia katika maandishi
anayoyaacha. Na maaandishi hayo huwa ukumbusho na urithi auachiyao jamii yake
milele na milele.’
Bwana
Yussuf pia alifafanua kwa upana kwanini ameamua kuandika kitabu chake kwa
kutumia lugha ya Kiswahili kwa kusema kwamba hadithi zilizomo humo zinawalenga
waswahili wenyewe na sio watu wa jamii nyengine. Kwa hivyo, sambamba na kukuza
na kukitangaza Kiswahili kimataifa, kitabu hicho kitatumika kuufiskisha ujumbe
uliokusudiwa kwa jamii kwa urahisi na kwa wepesi kwani lugha iliyotumika ni
nyepesi na yenye kufahamika kwa walengwa.
Alipoulizwa
kwanini alichagua kukipa kitabu chake hicho jina la ‘Paka wa Bini Hatibu’
mwandishi alisema; ‘ Paka wa Binti Hatibu ni usemi uliozoeleka na wengi. Ingawa
kufahamika kwake kimaana na kimantiki kumekuwa kukileta mashaka yatokanayo na
bezo, kebehi na dharau, usemi huu unabaki kuwa na maana pana, tena zaidi ya ile
iliyozoeleka kimazowea ya kuukamilisha usemi wenyewe. Jina la Paka wa Binti
Hatibu, halimmuliki paka kama paka peke yake na Binti Hatibu kama tumjuavyo,
bali kinaimuilika jamii yote na wanajamii, wote kwa ujumla.’
Akitoa
ufafanuzi kuhusu kitabu chake hicho ambacho utangulizi wake umeandikwa na Mhadhiri
wa masomo ya Fasihi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Bi Asha Khamis Hamad,
mwandishi huyo alisema kitabu chake kina hadithi saba na kila hadithi kama
kawaida yake ina ncha nyengine saba zinazoimulika jamii kwa undani na kwa kina kipevu cha udadisi na
upekuzi. Kila hadithi imebeba mikasa, vitimbi na viteweji kedekede ambavyo kwa
ujumla hutoa ujumbe na kuleta ladha ya ucheshi usio kikomo.
Akijibu
suala la vipi na wapi aliuota ujuzi huo wa uandishi, mwandishi alisema kuwa.
Amekuwa akisoma kazi mbali mbali za waandishi, na pia ametembea sana na kusikia
mengi kutoka kwa magwiji wa simulizi na uandishi wakiwemo waandishi nguli
katika fasihi ya Kiswahili kama vile Professa Said Ahmed, Farouk Topan na Ali
Mwalimu Rashid ambao kwa pamoja walimpa moyo na ari ya kuandika.
Kitabu
cha Paka wa Binti hatibu kinachapishwa na ‘The
Jomo Kenyatta Foundation’ ya Nairobi nchini Kenya na kitatumika kama kitabu
cha kiada katika masomo ya Fasihi katika chuo kikuu cha London, SOAS nchini
Uingereza mara tu baada ya kutoka hivi karibuni.
Mbali na kitabu hiki, mwandishi huyu pia amekamilisha miswada mengine minne ya riwaya na Hadithi fupi zinazosubiri kuchapishwa. Mwandihi hivi sasa anaandika vitabu vya kitaaluma vya kufundishia Kiswahili shuleni na vitabu vitokanavyo na utafiti wa mambo mbali mbali yahusuyo jamii na utamaduni wa watu wa Pemba. Moja ya muswada wa kitabu kitokanacho na utafiti wake ni kile cha ‘Watu 40 Mashuhuri kutoka Pemba’ ambacho utafiti wake unaendelea hivi sasa.
0 maoni:
Post a Comment