MWENYEKITI WA CCM APANDISHWA KIZIMBANI AKITUHUMIWA KUMBAKA MWALIMU HUKO SIMIYU


WASHITAKIWA wanne akiwemo Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mwamanyili wilayani Busega mkoani Simiyu, wanaotuhumiwa kufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha na kubaka kwa kundi, wamepandishwa kizimbani na kunyimwa dhamana.
Mwenyekiti huyo Ramadhan Msoka na wenzake, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Magu, chini ya ulinzi mkali wa polisi, wakikabiliwa na mashitaka mawili.
Akiwasomea mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Robert Masige, Mwendesha Mashitaka Mrakibu wa Polisi, Mkiwa, alidai kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo Agosti 23 mwaka huu saa 7 usiku katika eneo la Nassa Ginnery Kijiji cha Mwagulanja wilayani Busega.
Alidai kuwa, washitakiwa hao wanadaiwa kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha kupora mamilioni ya shilingi kisha kubaka.
Mkiwa, alidai kuwa siku ya tukio washitakiwa wakiwa na silaha za jadi, mapanga na fimbo, walimvamia Mwalimu Samuel Mkumbo na kumpora sh milioni 18 na kisha kundi hilo kumbaka kwa zamu mpangaji wa mwalimu huyo (jina linahifadhiwa), ambaye pia ni Mwalimu.
Katika kesi hiyo mshitakiwa wa kwanza ni Libent Rwegarulila, Ramadhani Msoka, Meshack Samson na Kubin Nkondo wote wakazi wa Kijiji cha Mwagulanja.
Mwendesha mashitaka huyo, aliiomba mahakama kutowapa dhamana washitakiwa hao na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mfawidhi Masige, alikubaliana na ombi hilo kwa hoja mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha ni kati yanayozuiwa kutoa dhamana chini ya kifungu cha sheria namba 148.
“Chini ya kifungu namba 148, kifungu kidogo cha 5 a (1) cha mwenendo wa sheria ya mwenendo wa mashitaka ya jinai, sura ya 20 kama ilivyo rekebishwa mwaka 2002, mahakama hii inawanyima dhamana, hivyo mtakwenda rumande hadi hapo Septemba 9, mwaka huu,” alisema.
Washitakiwa hao ambao awali walikana makosa hayo, walirudishwa mahabusu.
Msoka ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Mwamanyili na Rwegarulila ni mshauri wa mahakama ya Mwanzo ya Nyashimo.
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu, linaendelea na jitihada za kumsaka mtuhumiwa mwingine, Mashaka Obedi, ambaye ni Mchumi wa CCM Wilaya kwa kuhusishwa na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, amesema kuwa mtuhumiwa huyo anasakwa kwa udi na uvumba.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment