WALIMU na wanafunzi wa shule ya
sekondari Iwawa, wilayani Makete mkoa wa Njombe wametakiwa kutoridhika matokeo ya
kitato cha sita iliyoyapata shule hiyo na kushika nafasi ya nne kitaifa 2014
yaliyotangazwa miezi michache iliyopita.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na
mkuu wa wilaya ya Makete, Josephine Matiro, katika hafla ya kuwapongeza walimu
wa Iwawa sekondari baada ya shule hiyo kushika nafasi ya nne kitaifa, nafasi ya
pili kikanda na nafasi ya 1 kwa mkoa wa Njombe katika matokeo ya kidato cha
sita mwaka huu.
Matiro aliwataka walimu hao kuongeza
jitihada zao za kufundisha pamoja na kuwapongeza wanafunzi kwa moyo wa
kujisomea ambavyo kwa pamoja vimepelekea kuitangaza wilaya ya Makete kielimu na
kuwataka kupanda na kushika nafasi za juu katika mitihani inayofuata.
“Mnastahili pongezi lakini nawaombeni
ongezeni bidii ili mitihani inayokuja mwakani mpande zaidi ya hapa, muitangaze
wilaya yetu, tukishirikina pamoja tunaweza" alisema Matiro
Aidha mkuu huyo wa wilaya aliwataka
wananchi kushirikiana katika kuchangia maendeleo ya shule kwani serikali
inaunga mkono jitihada zao pale tu inapoona wamechangia.
Alisema kumekuwa na kasumba ya watu
wachache kuwakatisha tamaa wananchi wengi wenye moyo wakuchangia miradi ya
shule, na kusema wananchi wasikatishwe tamaa na watu wa aina hiyo kwani
serikali haiwaachii peke yao, wao wakichangia kwa kiasi fulani serikali nayo
humalizia.
Matiro alisisitiza kuwa kwa shule zenye
upungufu wa walimu, serikali inalitambua tatizo hilo na ndiyo maana inapanga
walimu wapya kila mwaka katika shule hizo na mwishowe upungufu huo utamalizika.
Awali akisoma taarifa ya shule, mkuu wa
shule hiyo Antony Ng'wavi, alisema shule yake inakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na walimu jambo
ambalo linachangia kupungua kasi ya ufaulu kwa kiasi kikubwa zaidi, huku
akiahidi kuwa mwakani shule yake itafanya vizuri kuliko mwaka huu
Mwisho.
0 maoni:
Post a Comment