Kamishna Msaidizi wa Nishati Mbadala kutoka Wizara ya Nishati na
Madini, Leonard Ishengoma akisoma hotuba ya ufunguzi (kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa Wizara, Eliakim Maswi) wa semina ya mafunzo kwa
Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, juu ya mpango kazi
wa mazingira wa sekta za nishati na madini, Septemba 1, 2014.
Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa katika picha ya
pamoja na Maafisa na Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini baada
ya ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku tatu kwa Wanamazingira hao
Septemba 1, 2014 jijini Mwanza. Kutoka kushoto (waliokaa) ni Kamishna
Msaidizi na Afisa Madini Kanda ya Ziwa Magharibi, David Mulabwa,
Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Mbadala, Leonard Ishegoma
na Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini,
Gideon Kasege.
Afisa Misitu Mkuu kutoka Kitengo cha Mazingira – Wizara ya Nishati na
Madini, Theodory Silinge akisisitiza jambo wakati wa semina ya mafunzo
kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, inayofanyika jijini
Mwanza.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara ya Nishati na Madini,
Gideon Kasege akizungumza na Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka
Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini Mwanza, wakati wa semina ya
mafunzo kwa wanamazingira hao.
Afisa Mazingira wa Mji wa Kahama, Martin Masele akiuliza swali wakati wa
semina ya mafunzo kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya
Ziwa iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini jijini Mwanza.
Wajumbe wa Sekretariet wakiandika kumbukumbu za Semina ya Maafisa
Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini
Mwanza. Kutoka Kushoto ni Nassor Abdullattif na Emmanuel Shija.
Kamishna Msaidizi na Afisa Madini wa Kanda ya Ziwa Magharibi, David
Mulabwa akifafanua jambo kwa wajumbe wa semina ya Maafisa Mazingira
wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa, Septemba 1, 2014 jijini Mwanza. Semina
hiyo ya siku tatu imeandaliwa na Kitengo cha Mazingira cha Wizara ya
Nishati na Madini.
Afisa Sheria kutoka Wizara ya Nishati na Madini Renatus Damian, akitoa
ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na shughuli za utunzaji mazingira wakati
wa semina kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya kutoka Kanda ya Ziwa,
Septemba 1, 2014 jijini Mwanza.
Na Veronica Simba
Maafisa Mazingira nchini kote wamepewa changamoto kuhakikisha kuwa
uwekezaji mkubwa unaoendelea hivi sasa katika sekta za nishati na
madini, hauathiri binadamu na viumbe hai wengine.
Changamoto hiyo imetolewa leo jijini Mwanza na Kamishna Msaidizi wa
Nishati Mbadala kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Leonard Ishengoma
wakati akifungua semina ya mafunzo kwa Maafisa Mazingira wa Wilaya
kutoka Kanda ya Ziwa Viktoria, juu ya mpango kazi wa mazingira wa sekta
za nishati na madini.
Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara husika,
Eliakim Maswi, Kamishna Msaidizi amesema hivi sasa, sekta za nishati
na madini zinapata uwekezaji mkubwa sana na kutolea mfano sekta ya
nishati ambapo shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zinaendelea na
hivyo kuwataka wanamazingira hao kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha
mazingira hayaathiriwi na shughuli husika.
Ameongeza kuwa, upande wa sekta ya umeme, uwekezaji unategemewa
kuongezeka kwa kiwango kikubwa pia kwa siku za hivi karibuni ikiwa
ni mikakati ya Wizara kuhakikisha inakidhi mahitaji ya nishati hiyo kwa
wananchi na hivyo amesema uwekezaji huo utaleta changamoto nyingi za
kimazingira, kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia sababu nyingine zinazochangia kuharibu mazingira,
hususan zinazohusiana na sekta za nishati na madini, Ishengoma
amesema matumizi ya nishati yanachangia kwa kiasi kikubwa kuleta
mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha madhara mbalimbali kama
vile majanga ya mafuriko, ukame na maradhi ya milipuko.
Kwa upande wa sekta ya madini, Kamishna Msaidizi Ishengoma amesema
kwa miaka ya hivi karibuni, sekta hiyo imekua kwa kasi kubwa sana,
hususan uchimbaji na uzalishaji wa madini, shughuli ambazo zinachangia
katika uharibifu wa mazingira.
Vilevile, amesema wengi wa wachimbaji wadogo na wa kati wa madini
wana mwamko mdogo sana katika kuhifadhi mazingira katika maeneo
yao ya kazi na ameongeza kwamba hata baadhi ya wawekezaji wakubwa
wanakwepa kutimiza taratibu za utunzaji wa mazingira kwa lengo la kupata
faida kubwa.
“Ni kwa sababu hiyo, Wizara ya Nishati na Madini imeandaa Mpango
Kazi wa Mazingira Kisekta ambao utekelezaji wake utaenda hadi ngazi
ya wilaya ili kuhakikisha shughuli za maendeleo zinazofanyika, haziathiri
mazingira,” amesisitiza Ishengoma.
Aidha, amewahamasisha Maafisa Mazingira kuhakikisha wanahuisha
masuala ya mazingira katika mipango na bajeti zao za wilaya kwa kuwa
wana nafasi nzuri katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwani huko
ndiko kuliko chimbuko la maendeleo.
Semina hiyo ya Mafunzo kwa Maafisa Mazingira, ni mwendelezo wa
semina zinazotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo chake
cha Mazingira ili kuongeza uelewa na hivyo kutekeleza kwa dhati azma ya
utunzaji mazingira.
Maafisa Mazingira wanaoshiriki katika semina hiyo ya mafunzo ya siku tatu
ni kutoka Wilaya 18 za mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Mara, Kigoma
na Tabora.
0 maoni:
Post a Comment