IPTL NI MWIBA KWA CCM

IPTL mwiba CCM
KUNA kila dalili za Baraza la Mawaziri la Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuvunjika tena baada ya ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya sh. bilioni 200, kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zilizohifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kubainisha kuwa fedha hizo zilitolewa kinyume na taratibu.

Kashfa hii nzito ni mfululizo wa nyingi zilizotokea chini ya utawala wa Rais Kikwete na hivyo kusababisha mawaziri kadhaa kuachia ngazi akiwemo aliyekuwa Waziri wake Mkuu, Edward Lowassa aliyejiuzulu Februari 7, mwaka 2008, kufuatia kashfa ya zabuni tata kwa kampuni hewa ya kufua umeme ya Richmond.
Vigogo wa serikali wanaotajwa kuhusika katika kashfa hii ni Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospiter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof.Beno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Wadadisi wa kisiasa wanabashiri kwamba kashfa hii huenda ikiwa mwiba wa kuking’oa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, ikiwa vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vitadumu katika muungano wao na kuwaeleimisha wananchi madhara ya ufisadi huo.
Kashfa kama hii iliwahi kuking’oa chama tawala cha KANU cha nchini Kenya mwaka 2002, ambapo kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mmiliki wa Kampuni ya PAP inayodai kuinunua Kampuni ya IPTL, Habinder Singh Sethi, anatajwa kuhusika katika kashfa kubwa ya ufisadi nchini Kenya ya Goldenberg, uliogharimu takribani dola milioni 600.
Ufisadi huo pia ulihusisha mahakama, watendaji, viongozi na wanasiasa wakubwa nchini humo, ikiwemo familia ya aliyekuwa Rais wa wakati huo, Daniel Arap Moi, ambapo katika uchaguzi mkuu wa 2002, vyama vya upinzani kupitia muungano wao wa National Alliance of Rainbow Coalition (NARC) chini ya mgombea wake Mwai Kibaki, kwa kutumia kashfa hiyo, vilifanikiwa kuking’oa Chama tawala cha KANU.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ambayo imekabidhiwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa ajili ya kuipitia na kuwahoji watuhumiwa, fedha za Escrow sh. bilioni 306 ni matokeo ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kulipishwa capacity charge zaidi ya kiwango kinachotakiwa kulipwa.
Ripoti hiyo, inasema kwamba Tanesco walipaswa kurejeshewa sh. bilioni 321 zilizolipwa zaidi kwa IPTL kati ya mwaka 2002 hadi 2012. Kwa maana hiyo, Escrow ni fedha za umma. Hii ni kinyume na kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi mbalimbali wa serikali ya Rais Kikwete wakiwemo Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nishati na Madini kwamba fedha hizo ni za mmiliki wa Kampuni ya IPTL.
Kwa mara kadhaa, Waziri Muhongo amenukuriwa na vyombo vya habari akitamba na kuwabeza wabunge waliosimama kidete kuhakikisha fedha za Escrow zinarejeshwa, akidai kwamba ushahidi waliowasilisha bungeni kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuonesha kwamba fedha hizo ni za umma, ni vipeperushi feki kwani yeye anao ushahidi wa makaratasi ya kujaza gari zima la tani moja kuthibitisha kuwa fedha hizo sio za umma.
Waziri Muhongo na Katibu wake, Maswi wamekuwa wakiwatuhumu wabunge David Kafulila wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) na Zitto Kabwe wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) kwamba wamehongwa na aliyekuwa Mwanasheria wa Tanesco, Nimrod Mkono kushupalia sakata hilo ili kukwamisha bajeti ya wizara hiyo ya 2014/2015.
Kashfa ya Escrow imeghubikwa na utata ambapo Harbinder Sing Sethi, anadai alinunua asilimia 70 ya hisa za Mechmar kwa kiasi cha sh. milioni 500 ($300,000) ndani ya wiki tatu tu tangu hisa hizo kuuzwa kwa kampuni moja ya Visiwa vya Uingereza vya Virgin kwa sh. milioni sita.
Lakini barua ya TRA Mkoa wa Ilala, iliyosainiwa na Meneja, Paschal Kabunduguru, yenye kumbukumbu nambari TRA/DR/ILA/RE/175 ya tarehe 15/11/2013, inaonyesha kuwa kampuni ya Mechmar ya Malaysia iliuza hisa zake asilimia 70 katika kampuni ya IPTL kwa kampuni ya Piper Links investment limited mnamo tarehe 9/9/2013 kwa thamani ya sh. 6,000,000 (milioni sita).
Nyaraka za malipo ya kodi kwa mujibu wa barua hiyo inaonyesha Mechmar walilipa kodi ya ongezeko la mtaji sh. 596,000 na kodi ya stempu ya sh. 180,000 mnamo tarehe 6 Disemba 2013 katika Benki ya CRDB Tawi la Waterfront.
Katika hali inayotia mashaka, kampuni ya Piper Links nayo, kwa mujibu wa nyaraka toka TRA, ikauza hisa zake kwa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions mnamo tarehe 30 Oktoba, 2013, takribani wiki tatu tangu kununuliwa kwa hisa hizo toka kwa Mechmar.
Kwa mujibu wa barua ya TRA, kodi iliyolipwa ni ya ongezeko la mtaji sh. 47,940,000 na ushuru wa stempu sh. 4,800,000.
Malipo ya kodi hiyo yalilipwa siku ile ile ambayo Mechmar walilipa yaani Disemba 6, 2013, jambo linalozidi kuzua utata mkubwa kuhusu mhamala huo.
Pengine kinachotia shaka zaidi ni kwamba nyaraka zote mbili toka TRA ziliandikwa siku moja, na zote zina kumbukumbu namba zinazofanana licha ya ukweli kwamba zilikuwa zinakwenda kwa makampuni mawili tofauti, moja ikiwa Malayasia, na nyingine ikiwa visiwa vya Uingereza vya Virgin.
Pia nyaraka hizi toka TRA, zinapingana na kauli ya Sethi ambaye amenukuliwa na vyombo kadhaa vya habari akidai kwamba alinunua hisa asilimia sabini za Mechmar mwaka 2010, toka kampuni ya Piper Link—mwaka mmoja kabla ya PAP kuanzishwa.
Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema kwa mujibu wa Sheria ya kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2012, mauzo yeyote ya hisa au mali ambazo zipo Tanzania mauzo yake lazima yathibitishwe na Wizara husika baada ya kodi zote kulipwa.
Nyaraka hizi zinaonesha kuwa mauzo ya IPTL kutoka Mechmar kwenda PiperLink na kutoka PiperLink kwenda PAP yote yamelipiwa kodi siku moja tena baada ya malipo ya fedha za Escrow kwenda PAP Disemba 5, 2013.
Kwa kuzingatia nyaraka hizo, ni dhahiri kuwa mpaka kampuni ya PAP ilipokuwa inalipwa fedha za Escrow hawakuwa na umiliki wa hisa za IPTL. Hata amri ya mahakama ilipotolewa kuwa PAP wapewe mali za IPTL, kampuni hiyo haikuwa na umiliki wa wowote wa IPTL.
Pia katika hati za kuhamisha hisa ambazo ziliidhinishwa na TRA mkoa wa Ilala, mwandiko ulipo unafanana sana na mwandiko wa nyaraka za malipo ya kodi, CRDB, tawi la Water Front—jambo linaloonyesha kwamba mtu mmoja huyo huyo ndiye aliyeandika nyaraka zote hizi.
Utata mwingine ni kuwa iweje kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa na hisa asilimia 30 katika IPTL ilipwe dola za Kimarekani milioni 75 wakati Mechmar iuze asilimia 70 kwa sh. milioni 6 tu na PiperLink iuze kwa dola laki tatu tu ndani ya wiki tatu.
Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wake, Jaji Fredrick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, wamekuwa wakisisitiza kwamba fedha hizo zilitolewa kwa kuzingatia hukumu ya MahakamaKuu.
Hukumu hiyo ya Jaji John Utamwa inapingwa na Kafulila na wadau wengine kuwa imetafsiriwa visivyo, kwani hakuna popote alipotaja Akaunti ya Escrow, ingawa katika muhtasari wa kikao kati ya Tanesco, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za akaunti hiyo zipewe Kampuniya PAP.
Kupitia barua kumb. No. SAB.88/417/01/5 ya Oktoba 21, 2013, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Maswi alimwandikia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu akimtaka aruhusu fedha hizo katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, sehemu ya ripoti ya CAG kuhusu kashfa ya uchotwaji wa fedha hizo inathibitisha kuwa TRA walibaini kuwa msingi wa ukokotoaji wa kiwango cha kulipa kodi ya Ongezeko la Mtaji ulitokana na nyaraka zenye taarifa zisizo sahihi, jambo lililochangia kutolipwa kodi ya kiasi cha sh. 8,682, 521,100.
Utawala wa Rais Kikwete umeghubikwa na kashfa nzito za ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kipindi chote cha miaka tisa, lakini mara zote kumekuwa na kigugumizi cha kuwang’oa watuhumiwa mpaka pale Bunge lilipoingilia kati.
Kashfa zilizotikisa ni ile ya ununuzi wa rada mbovu kwa gharama kubwa hadi serikali ya Uingereza ikaingilia kati kushinikiza kampuni iliyouza rada hiyo irudishe chenji kwa Tanzania, pia ipo ile ya EPA iliyoaiandama serikali mwanzoni mwa utawala wa Kikwete ambapo baadaye aliyekuwa Gavana wa BoT, Daud Balali alifariki bila kuchukuliwa hatua.
Sakata lingine ni kampuni hewa ya Richmond mwaka 2008, ambapo mbali na Lowassa, mawaziri wengine waliong’oka ni Dk. Ibrahim Msabaha na Nasir Karamagi waliopata kuwa mawaziri wa Wizara ya Nishati na baadaye Baraza la Mawaziri lilivunjwa na kuundwa upya kwa Mizengo Pinda kuteuliwa kushika wadhifa wa Waziri Mkuu ambaye naye kashfa ya Escrow huenda ikamwondoa.
Zipo pia kashfa za uchangishaji fedha kinyume cha taratibu ndani ya Wizara ya Nishati na Madini iliyomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wake, David Jairo na kisha uchotwaji wa fedha uliyoihusisha kampuni ya Pan African Energy zaidi ya sh. bilioni 110, tuhuma ambazo ziliwangoa Jairo na Waziri wake, William Ngeleja.
Kashfa ya Buzwagi nayo ilitikisa Bunge mwaka 2007, ambapo Zitto alimtuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Karamagi kuwa alikiuka utaratibu kwa kusaini mkataba mbovu wa mgodi huo ikiwa hotelini nje ya nchi. Hata hivyo CCM kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilimgeuzia Zitto kibao na kumwadhibu kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge.
Pia zipo kashfa za ripoti ya CAG mwaka 2012 na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu utekelezaji wa oparesheni tokomeza mwaka 2013, ambapo mawaziri Dk. Cyril Chami, Dk. Hadji Mponda, Omary Nundu, Mustafa Mkulo, Ezekiel Maige, Dk. Athuman Mfutakamba, Dk. Lucy Nkya, Balozi Khamis Kagasheki, Dk. Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na Dk. Mathayo David waling’oka kufuatia shinikizo la Bunge.
Wabunge CCM wakamia
Wakati PAC leo ikianza kumhoji Jaji Werema kuhusu kashfa hiyo, wabunge wa CCM wanatarajia kuwa na kikao maalum kwa ajili ya kujadili sakata hilo kabla halijaingia bungeni Novemba 27.
Kashfa hiyo, itabiriwa kwamba huenda ikamwangusha Waziri Mkuu, Pinda, kutokana na wabunge wanaomuunga mkono Lowassa kujipanga kulipa kisasi cha yale ya Richmond ya mwaka 2008.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alilieleza gazeti hili kuwa kamati yao imeshaanza kazi tangu jana, lakini leo itaanza kuhoji Jaji Werema ambaye ni mmoja wa watuhumiwa.
Mwingine atakayehojiwa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na itaendelea na kazi yake kwa kuwahoji watu wengine kadri itakavyoona inafaa.
Habari zaidi kuhusu kamati hiyo iyopiga kambi nje ya viwanja vya Bunge, zinasema kuwa itafanyakazi usiku na mchana na kukamilisha kazi yake ndani ya siku tatu.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ilikabidhiwa ripoti hiyo juzi na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Mmoja wa wabunge kutoka CCM, aliliambia gazeti hili kuwa tayari wameshajulishwa kuwapo kwa kikao hicho kitakachofanyika siku yoyote wiki hii.
“Tutakuwa na kikao wiki hii, sijui wanataka kutuambia nini. Kama kuwatetea watuhumiwa itakuwa ngumu kwa sababu taarifa ya CAG inaonyesha wazi kwamba Waziri Muhongo, Katibu Mkuu, Maswi na wengine waliotajwa kuhusika, hawaponi. Sisi tutakuwa na nguvu gani kuwatetea? Alihoji.
Wabunge wengi bila kujali vyama vyao, wamepania sana mjadala huo na kulitaka Bunge litenge muda wa kutosha ili kila mchangiaji apate muda wa kutosha.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), jana aliomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge litenge zaidi ya siku moja ya mjadala wa kashfa hiyo ya IPTL.
Alisema kwa jinsi hali ilivyo, inaonyesha kuwa wabunge wengi wanataka kuchangia, hivyo aliomba mwongozo wa Spika ili Bunge liongeze muda zaidi wa kuchangia.
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema anachukua mawazo hayo na kuyapeleka kwenye Kamati ya Uongozi ili waweze kufanya uamuzi.
CREDIT: TANZANIA DAIMA
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment