MIKATABA YA GESI YAWAFIKISHA MABOSI WA TPDC POLISI


Mwenyekiti wa TPDC akipanda gari la Polisi chini ya ulinzi kwenda kituo baada ya kukamatwa kwa amri ya Kamati ya Bunge.
Usiri katika mikataba ya utafiti na uchimbaji wa gesi umesababisha Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) (pichani kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa kukaidi agizo la kuwasilisha mikataba hiyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).


Mwenyekiti huyo, Michael Mwanda na Kaimu Mkurugenzi, James Andilile, walitiwa mbaroni jana jijini Dar es Salaam baada ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, kutoa taarifa polisi baada ya menejimenti ya TPDC kukaidi agizo la kukabidhi mikataba hiyo kwa PAC.

Kabla ya kukamatwa, viongozi hao waliingia katika kikao cha PAC na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto na Makamu wake, Deo Filikunjombe, walitaka kujua sababu zilizowafanya washindwe kuwasilisha mikataba hiyo wakati ni haki ya kisheria wabunge kuiona na kuikagua kwa niaba ya wananchi.

Katika kikao hicho Andilile alionekana kuzidiwa maswali aliyokuwa akiulizwa na wajumbe wa kamati hiyo na kuanza kujibu kana kwamba hana uhakika na alichokuwa akikijibu.

Baadaye ilifika zamu ya Mwanda aliyetakiwa kujibu sababu za kutopeleka mikataba hiyo. Aliitupia mzigo Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba waliandika barua ofisi zote mbili kuomba mwongozo kuhusu ombi la PAC kutaka kupitia mikataba ya gesi.

Mwenda aliongeza kuwa licha ya jitihada zilizofanywa na TPDC kuomba mwongozo huo kwa wizara hawakujibiwa hadi jana.

Baada ya mahojiano hayo, Zitto akizungumza na waandishi wa habari alisema TPDC wameonyesha dharau kwa Bunge kwa kukaidi agizo halali la kamati hiyo la kutakiwa kupeleka mikataba 26  ya gesi ili kujiridhisha juu ya uhalali wake pamoja na manufaa yake kwa Watanzania.

Naye Filikunjombe alisema uongozi wa TPDC umeonyesha dhahiri kuwatetea wawekezaji badala ya kujali maslahi ya taifa na kwamba kamati hiyo kamwe haitakubali na wabunge wataendelea kutimiza wajibu wake.

Hata hivyo, dalili za kukamatwa kwa viongozi hao zilionekana mapema asubuhi kutokana na askari kuonekana maeneo ya ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam na kuruhisiwa  kuingia katika kikao hicho.

Baada ya askari kuingia ndani ya kikao, waandishi wa habari walitolewa nje na baada ya muda mfupi ndipo Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC na Kaimu Mkurugenzi walipowekwa chini ya ulinzi na kuchukuliwa toka katika ofisi za Bunge kupelekwa kituo cha polisi kati.

WAACHIWA HURU
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana jioni alisema Jeshi la Polisi limewaachia huru Mwanda na Andilile kusubiri  ufafanuzi wa Bunge kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.

“Tumeona hakuna sababu ya kuendelea kuwashikilia viongozi hao na badala yake wameachiwa huru tukisubiri taratibu na sheria,” alisema.

Alisema tukio la kukamatwa kwa viongozi hao lilitokea jana saa 5:00 asubuhi katika ukumbi wa Bunge, jijini Dar es Salaam katika chumba cha mikutano ambako kulikuwa na kikao cha PAC.

Kamishna Kova alisema katika kikao hicho ajenda ya mkutano ilikuwa ni kuwasilisha mahesabu ya TPDC katika kipindi kinachoishia 30 June, 2013 na baada ya majadiliano ya muda kuhusu hati mbalimbali zilizotakiwa na PAC hatimaye Zitto alitoa agizo kwa askari waliokuwapo katika eneo hilo wawakamate vigogo wa TPDC.

“Kutokana na maelezo ya mashahidi waliokuwapo kwenye tukio hilo katika ukumbi wa Bunge, Mwenyekiti Zitto alisema wapelekwe Polisi waende kusubiri mwongozo wa Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maagizo ya mwisho,” alisema.

Alisema baada ya agizo la Zitto vigogo hao wa TPDC walikamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi Kati chini ya ulinzi, lakini Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilishindwa kuchukua hatua kwani shauri hilo halikuwa na mlalamikaji alikwenda kufungua jalada na kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi hao.

Aidha, maofisa wawili wa sekretarieti ya Bunge waliitwa Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo wakiwapo pia mawakili wa watuhumiwa na hatimaye kilifanyika kikao cha dharura ili kupata ufafanuzi wa kisheria.

Kova alisema iligundulika kwamba katika Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge sura ya 296 Kif 12 (3) kinaonyesha kwamba Mwenyekiti wa PAC alitakiwa kwanza apendekeze kwa  Spika wa Bunge juu ya jambo lolote aliloliona kama ni kosa.

Alisema kwa mujibu wa utaratibu, Spika akisharidhika kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa mezani kwake na Mwenyekiti wa PAC, ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa.

Kova alisema katika kikao hicho na jopo la wanasheria iligundulika kwamba katika sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya bunge, agizo la kukamatwa viongozi wa TPDC lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge lilihitaji kuzingatiwa kwanza kabla ya utekelezaji wake.

Mwaka jana PAC ilitoa agizo kwa menejimenti ya TPDC kuwasilisha mikataba ya utafiti na uchimbaji wa gesi 26 kwa kamati ili ikaguliwe, katika kikao baina yao mwaka huu.

Hata hivyo, Oktoba 28, mwaka huu menejimenti ya TPDC ikiongozwa na Mwanda, ilihudhuria kikao hicho bila ya kuwa na nyaraka hizo muhimu, kinyume cha maagizo ya kamati hiyo.

Hivyo, akasema kama PAC wanahitaji nyaraka hizo, basi wanatakiwa wamwandikie waziri huyo kumuomba awapatie na siyo kuwabana TPDC wafanye hivyo.Waziri wa Nishati na Madini, alifanya mkutano na wajumbe wa bodi ya TPDC, Septemba 15 mwaka jana  na kuwaagiza kupitia upya mikataba, ambayo tayari ilishaingiwa na kuwakataza kusaini mikataba mipya hadi watakapokuwa wametoa ripoti ya mikataba hiyo.
 
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment