MWANAUME MWENYE WAKE WAWILI ATENGANISHWA KICHWA NA KIWILIWILI

     
     
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe

WATU watatu wa familia moja, wameuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao, akiwamo baba wa familia hiyo aliyetenganishwa kichwa na kiwiliwili.


Wameuawa kutokana na ugomvi unaodhaniwa unatokana na madai kuwa baba huyo anampendelea mke mdogo, ambaye pia ameuawa.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe, amesema kuwa waliokutwa wamekufa katika eneo la tukio ni baba wa familia, Sadick Khamis (84) na mke wake, Zamda Sadick (44).

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mtoto wao Juma Sadick (15) alifia Hospitali Teule ya Wilaya iitwayo Rubya wakati akipatiwa matibabu. Familia hiyo inaishi kijiji cha Itongo tarafa ya Nshamba wilayani Muleba.

Kamanda Mwaibambe alisema wauaji hao walivamia familia hiyo saa 2.45 usiku Novemba 7 na kufanya unyama huo, ambao chanzo chake inahofiwa ni ugomvi wa urithi uliokuwepo muda mrefu katika familia hiyo.

Alisema Khamis alioa wake wanne na Zamda alikuwa mke mdogo, jambo lililosababisha ugomvi katika familia, ikidaiwa baba huyo wa familia anampendelea Zamda.

Katika tukio hilo, mtoto mwingine wa kike wa baba huyo, Aza Sadick (19), ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lukondo iliyopo Nshamba, hakujeruhiwa lakini wauaji hao walichukua simu yake ya mkononi.

Kutokana na mauaji hayo, mtoto mkubwa wa baba huyo, Issa Sadick (49) anashikiliwa Polisi akidaiwa kuhusika na mauaji hayo, kutokana na yeye kuwa na mgogoro mkubwa na baba yake.

Kamanda Mwaibambe alisema uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea na Polisi itatoa taarifa za kina baadaye.HABARILEO
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment