HIVI NDIVYO WIZI ULIVYO PANGWA NI MABILIONI YA STANDARD YA UINGEREZA

Dar es Salaam. Mazungumzo ya kukamilisha mchongo wa Sh13 bilioni katika mkataba wa Serikali wa kukopa Sh1.3 trilioni kutoka benki ya Standard ya Uingereza ulikamilika katika kipindi cha miezi sita, imefahamika. Taasisi ya Kuchunguza Ufisadi (SFO) ya Uingereza iliyochunguza sakata la baadhi ya maofisa kujipatia fedha hizo kinyume cha taratibu imesema katika ripoti yake kwamba mazungumzo hayo yalifanyika kati ya Mei na Novemba, 2012.
Mchongo huo ulikamilishwa na maswahiba wawili ambao ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitillya na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Stanbic, Bashir Awale (BA). SFO inasema katika ripoti yake kwamba Kitillya na Awale walifahamiana Februari ya mwaka 2008 wakati bosi huyo wa TRA alipoomba udhamini wa mkurugenzi huyo ili kutimiza matakwa ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Havard alikokuwa amepata udahili.
Benki ya Stanbic ambayo ni tawi la South African Group ya Afrika Kusini na ambayo ni tawi la benki ya Standard ndiyo ilikuwa inafanya uratibu. BA na Kaimu mkuu wa uwekezaji wa Stanbic, Shose Sinare (SS) walikuwa wakiwasiliana na ofisa wa benki ya Standard, Florian Von Hartig (FVH) ambaye alikuwa akiiwakilisha katika soko la mitaji jijini London.FVH alikuja nchini na Septemba 20, alipokuwa anaondoka kurudi Uingereza alifahamishwa juu ya ongezeko la asilimia moja ya ada na mshirika wa ndani yaani Stanbic. Mawasiliano ya baruapepe yalikuwa hivi:
BA: Barua ya mamalaka inahitajika leo. Ni muhimu sana (aliwaandikia FVH na SS).
FVH: Umeeleweka. SS kuna chochote cha kuongeza katika barua hiyo kama tulivyojadiliana? Pili, tumeshaelewana na washirika wetu kwamba wanahusika na ni sehemu ya barua? (aliijibu baruapepe hiyo na kutuma nakala kwa wafanyakazi wawili MK na MP wa Standard).
Mwisho, tunaendelea kujadiliana na washirika juu ya mkataba wetu wa pembeni kwa kubainisha mgawanyo wa ada na wajibu wa kila mmoja. Tunapaswa kuzingatia mkataba huu mara tu utakapokuwa umemalizana na barua hiyo. Tuwe na malengo.
SS: Barua ya mamlaka (aliiambatanisha na kubainisha kuwepo kwa mshirika, ada ya muamala kuwa ni asilimia 2.4 kwenye kipengele cha sahihi ya mshirika huyo) itatolewa baadaye.
MK: Mshirika anatakiwa awepo kama mtia saini?
SS: Hapana. Lengo ni kuwajumuisha kupitia mkataba wa pembeni kati yetu na washirika. Katika miamala mingine pia wameshiriki (anataja benki nyingine). Hivi ndivyo ilivyofanywa. Serikali inapenda kushughulika na mdau mmoja ambaye atawaratibu wanaobaki.
MP: Tumejadiliana na FVH. Wizara itatakiwa kuilipa benki asilimia 1.4 na mshirika asilimia moja inayosalia moja kwa moja. Kwa mshirika kulipwa kiasi hicho ni lazima abainishwe kwenye barua ya mamlaka. Una sababu zozote za msingi kwamba wizara haitaki atajwe? Baada ya majibizano hayo, walifanya mkutano kwa njia ya mtandao. Kutoka katika mkutano huu, ilikuwa dhahiri kuwa Standard haikutaka kuwa na mkataba wowote na mshirika wa ndani. Ilikubaliwa kuwa Stanbic itamlipa mshirika huyo ambaye atatajwa kwenye barua ya mamlaka.
Baada ya majadiliano hayo, FVH alituma baruapepe nyingine kwa maofisa wenzake wa Standard akieleza, “Tunahitaji ridhio la mteja kama tutakuwa na ushirika na Stanbic. Sifahamu, kwa uhakika, nini mahitaji ya mteja wa Tanzania lakini kupindisha taratibu hakukubaliki labda kama huyo mshirika wa ndani anaushawishi kwa mteja.”
Septemba 21, mwanasheria wa Stanbic aliandaa mkataba wa mgawanyo wa ada kati ya benki hiyo na mshirika wa ndani, Egma. Benki iliwakilishwa na BA wakati Dk Fratern Mboya alikuwa upande wa Egma. Hakuna aliyejua, kati ya Standard na Stanbic, ni kazi gani itafanywa na Egma kiasi cha kulipwa Sh13 bilioni.
Septemba 24, SS alituma ujumbe kwa maofisa wawili wa Serikali katika wizara ya fedha na nakala za nyaraka zilizosainiwa na FVH pamoja na BA na yeye mwenyewe.Septemba 26 Serikali ilijibu kwa mapendekezo kuhusu barua ya mamlaka na ile ya ada. SS alimtumia BA ili wajadili kwa pamoja. Serikali ilipendekeza mshirika wa ndani aondolewe kwenye barua ya mamlaka, ingawa haikuelezwa hivyo kwenye ile ya ada.
Baadaye BA na SS walilazimika kujadiliana na maofisa wa Standard ambao hawakuafiki wazo la kuwa na mshirika. BA aliwaambia, “Watatusumbua…acheni tufanye hivyo. Tusiwataje kabisa (Egma). Tunao mkataba wa pembeni ambako tutaweka kila kitu. Fahamuni kuwa hawa jamaa watauhitaji mkataba huo ili kulinda maslahi yao.”
Katika majibu ambayo hayakuwasilishwa Standard, SS aliieleza Serikali kuwa “mgawanyo wa ada hiyo ulijumuisha gharama za uratibu, maandalizi, uwezeshaji, tarishi na ushiriki. Gharama za ushauri zimeondolewa. Uwezeshaji na mipangilio ni asilimia moja ambayo inajumuisha kila kitu kama sheria na uwakala. Kiasi kinachobaki ni kwa ajili ya ushiriki.”
Serikali ya Awamu ya Tano inafanya uchunguzi wa mipango hiyo yote ili wahusika wote waweze kuwajibishwa.
By Julius Mathias, Mwananchi

from Blogger http://ift.tt/1ODgJUo
via IFTTT


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment