Serikali kupitia, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuwa halijakwamisha uzalishaji wa saruji katika kiwanda cha Mfanyabiashara Mkubwa wa Nigeria Alhaj Aliko Dangote kilichopo Mkoani Mtwara.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPBC)
Kaimu Mkurugenzi wa TPDC Kapulya Musomba,amewambia wanahabari leo jijini Dar es Salaam  kuwa Kiwanda cha Dangote hakijaanza kununua Gesi kutoka kwa TPDC na kwamba kilichopo kwa sasa TPDC imefanya majadiliano ya mkataba wa awali na kiwanda hicho  kwa ajili ya kukiuzia gesi asilia itakayotumika kuzalisha umeme utakaotumiwa na kiwanda hicho.

Kapulya Musomba
Aidha, ameendelea kusema kuwa  hadi kufikia mwezi Januari 2017 miundombinu ya gesi asilia itakuwa imeshaunganishwa na mitambo ya kufua umeme utakaotumika kwenye kiwanda hicho, na kuongeza kuwa TPDC inafanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, na kuwajali wawekezaji katika kukuza uchumi wa nchi.
Akizungmzia kuhusu malalamiko ya ubora wa makaa ya mawe yanayotumiwa na Kiwanda cha Saruji cha Dangote Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Nishati na Madini John Shija amesema kuwa kuna  makubaliano ya kimkataba kati ya makampuni yanayohitaji makaa ya mawe pamoja na  kampuni ya Ngaka Col Mine ambayo inazalisha  makaa ya mawe.

Kiwanda cha Dangote
Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara chenye thamani ya Dola za Marekani milioni 600 kina uwekezaji mkubwa katika uzalishaji saruji kuliko viwanda vyote katika Afrika Mashariki. Kina uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kimetoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1,000 wa Mkoani Mtwara.