WAFUGAJI wa kuku wa asili mkoani Singida wamejipatia zaidi ya Sh bilioni 1.8


WAFUGAJI wa kuku wa asili mkoani Singida wamejipatia zaidi ya Sh bilioni 1.8 kutokana na kuuza kuku hao kwenye miji mikuu mbalimbali nchini katika kipindi cha Julai 2015 na Juni mwaka huu.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Idara ya Uchumi na Uzalishaji, Beatus Choaji aliyasema hayo kwenye Taarifa yake ya Uendelezaji wa Kuku wa Asili mkoani Singida katika kipindi cha 2015/2016 katika kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) kilichofanyika mjini hapa.

Choaji alisema mapato hayo yalipatikana baada ya jumla ya kuku 151,242 kuuzwa kwa kuwasafirisha nje ya mkoa hasa Arusha na jijini Dar es Salaam kwa kipindi kilichotajwa.

Alisema kuku wa asili wakifugwa vyema kwa kudhibiti ugonjwa wa mdondo na kuzingatia kanuni za ufugaji bora, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka kwa jamii kwa kujipatia pato na hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, wilaya na mkoa kwa ujumla.

Alisema mbali na kuku hao wa asili kuwa rasilimali kwa mkoa wa Singida, pia ni lishe bora hasa kwa watoto na akinamama kutokana na nyama yake pamoja na mayai.

Ili kuimarisha ufugaji kuku wa asili mkoani humu, Choaji alishauri halmashauri zote zitekeleze mkakati wa kuchanja kuku kwa wakati mmoja mara tatu kwa mwaka kwa kuwatumia watoa chanjo jamii wasiokuwa wataalamu wa mifugo.

Alisema hatua hiyo itadhibiti kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa mdondo ambao ni hatari kwa kuku wa asili.

Aidha, alisema katika kipindi hicho kulikuwa na jumla ya vikundi 97 vya ufugaji kuku wa asili ambavyo vilimiliki mashine 20 za kutotolea vifaranga wakati kulikuwepo na masoko matatu tu ya uuzaji na ununuzi wa kuku.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment