WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Charles Tizeba kufanya uchunguzi kwa nini mbolea ya minjingu inayozalishwa
nchini haitumiki na badala yake inaagizwa mbolea kutoka nje ya nchi.
Ametoa agizo Desemba 3, 2016 wakati alipotembelea kiwanda cha
Fibre Board 2000 Limited ambacho kinatengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo mbolea
ya Minjingu, wakati akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani
Arusha.
Amesema mbolea hiyo licha ya kuwa na viwango vya ubora
vinavyohitajika, haitumiki nchini kwa sababu ya kuingiliwa na masuala ya
kisiasa dhidi ya matumizi yake.
Amesema kumekuwa na mijadala mingi kuhusu mbolea ya minjingu
kumbe baadhi ya watendaji wanatengeneza mianya ya kwenda kununua mbolea nje
ambako hutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya
maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha Fibre Board 2000
Limited, Tosk Hansi amesema kampuni hiyo inayozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo
mbolea ya minjingu, imetoa ajira kwa watu zaidi ya 1,800 wengi wao wakiwa ni
vijana ila inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya urasimu wakati
wanapoomba vibali vya uvunaji mazao ya misitu.
Awali, kampuni hiyo ya Fibre Board 2000 limited imemkabidhi
Waziri Mkuu mchango wa madawati 1,000 kwa ajili ya shule mbalimbali za mkoani
Arusha ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
0 maoni:
Post a Comment