MKUU wa Mkoa wa Singida,
Mathew Mtigumwe ameagiza kukamatwa na kufunguliwa mashitaka Mwenyekiti wa
Baraza la usuluhishi Kata ya Rungwa wilayani Manyoni, kwa tuhuma za kumtoza
faini ya Sh 200,000 mwanafunzi wa kike anayedaiwa kujihusisha na vitendo vya ngono.
Mwenyekiti huyo, Zuberi
Manjemi anadaiwa kumtoza faini hiyo mwanafunzi wa darasa la nne kisha kumwachia
bila adhabu yoyote kijana aliyedhaniwa kuwa ni mpenzi wa binti huyo, hali
iliyozua hasira ya wazazi wa binti huyo na kuamua kutoa malalamiko yao kwenye
mkutano wa hadhara.
Katika utetezi wake,
Mwenyekiti huyo amedai kuwa aliamua kumtoza faini binti huyo pekee baada ya
kukiri kupokea simu ya mkononi kutoka kwa mvulana huyo, hivyo alitoa adhabu
hiyo ili iwe fundisho kwa wananfunzi wengine wa kike.
Utetezi huo umetupiliwa
mbali na Mkuu wa Mkoa na kuagiza mwenyekiti huyo akamatwe kwa kosa la kutoa
adhabu ya upande mmoja huku akimwachia huru mtuhumiwa wa kiume aliyemrubuni
mwanafunzi huyo kufanya naye mapenzi.
Habari zilizopatikana eneo
la tukio zinadai kuwa baada ya walimu wa shule ya Msingi Rungwa, kutilia shaka
umiliki wa simu ya mkononi ya mwanafunzi huyo, walimhoji na alikiri mwenyewe
kupewa na mvulana huyo.
Walimu hao wamedai kuweka
mtego kwa mwanafunzi huyo kumpigia mvulana huyo na kutokana na mazungumzo yao
walibaini kuwa wana mahusiano ya kimapenzi ya muda mrefu, hivyo kuamua
kuwapeleka baraza la kata ambapo mwanafunzi alitozwa faini na mpenzi wake
kuachiwa huru.
0 maoni:
Post a Comment