STAILI ya uongozi ya Rais Dk. John Magufuli imewapatanisha rasmi Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, na Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, marafiki waliogeuka mahasimu wa kisiasa ambao kwa muda wamekuwa hawaivi, Raia Mwema linafahamu.
Uhusiano wa kibinafsi na kisiasa baina ya Mbowe na Zitto na ulilegalega kabla ya kuvunjika kabisa katika kipindi cha miaka minne iliyopita; hatua iliyosababisha Mbunge huyo wa Kigoma Mjini kukihama chama hicho.
Hata hivyo, wiki iliyopita, Zitto alionekana katika meza moja na Mbowe –wakati kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani bungeni alipokuwa akijibu tuhuma za yeye kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya nchini. Hii si maraya kwanza kwa Zitto na Mbowe kukaa meza moja tangu kuanzishwa kwa ACT-Wazalendo, kwani wamewahi kuonekana pamoja katika baadhi ya masuala ya kitaifa.
Lakini, hatua ya Zitto kukaa meza moja na Mbowe kwa jambo ambalo linamhusu Mbunge huyo wa Hai binafsi, inaelezwa limefungua ukurasa mpya wa uhusiano baina ya viongozi hao wawili.
Katika mkutano huo, mbali ya Mbowe kukana kujihusisha na biashara hiyo haramu, Zitto alimtetea kwamba kwa muda wote aliomfahamu, hajawahi kusikia wala kumuona akijihusisha na biashara hiyo.
Alipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Zitto alisema ameamua kusahau yaliyopita kwa sababu hivi sasa adui wa vyama vya Upinzani si Mbowe wala Chadema bali ni serikali ya Rais Magufuli.
“Ni suala la uamuzi tu. Naweza kuamua kubaki na kinyongo na chuki za mambo yaliyopita au kusonga mbele. La muhimu ni kusonga mbele.
“Kimsingi adui wa Upinzani hivi sasa ni serikali ya Rais Magufuli. Yenyewe ndiyo imepiga marufuku mikutano ya kisiasa ya vyama vyetu. Yenyewe ndiyo imewaweka gerezani wenzetu.
“Hivyo hapa uamuzi ni rahisi tu. Ama kuamua kila mmoja akae kivyake na afe kivyake au kuungana na kuwa kitu kimoja dhidi ya adui mmoja. Mimi nimeamua kwamba njia sahihi ni umoja,” alisema.
Akizungumza na Raia Mwema juzi Jumatatu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema hana tatizo na Zitto kwani mbunge huyo ni kama “mwanaye” kisiasa na hana matatizo naye kwa sasa.
“Zitto ni mwanangu, hivi mzazi mtoto akinyea kiganja utakikata” alihoji Mbowe.
Mbowe alifafanua kwamba chama chake kiko tayari kushirikiana na chama chochote cha siasa au mtu yoyote kupinga udikteta unaoanza kujitokeza kwenye mazingira ya kisiasa ya sasa kwa manufaa ya Taifa.
“ Chadema na ACT tuna tofauti zetu za kivyama lakini hilo haliondoi uwezekano wa kushirikiana kwa sababu sote tunakabiliwa na hali hii ya udikteta unaoanza kumea nchini.
“Na kama umefuatilia kwa karibu, si Zitto pekee ambaye tunashirikiana naye bali hata kwa wabunge wa chama tawala (CCM), yapo mambo ambayo hawakubaliani nayo na wanatuunga mkono,” alisema.
Chadema na Magufuli
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, Chadema kimekuwa matatani kwani hadi hivi sasa kina wabunge wawili walioko jela na viongozi wengine wa chama katika ngazi za juu wako vifungoni.
Wabunge walioko jela ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali. Pia, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Lindi, Selemani Matthew Luwongo, naye amefungwa jela mkoani Lindi. Mnadhimu wa Chadema bungeni, Tundu Lissu, naye pia amefunguliwa kesi mahakamani.
Zitto na Magufuli
Ingawa chama chake cha ACT-Wazalendo bado ni kichanga kisiasa, Zitto amekuwa ni mmoja wa viongozi wa Upinzani walioko mstari wa mbele kwenye kukosoa utendaji wa serikali ya Magufuli.
Wiki tatu zilizopita, Zitto alidaiwa kuondoka nchini baada ya kunusurika kukamatwa na askari baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara mjini Kahama.
Wakati wa Mkutano wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma wiki iliyopita, kulikuwa na taarifa kwamba Zitto alikuwa hatarini kukamatwa na Polisi, ingawa taarifa hizo zilikuja kukanushwa na Jeshi la Polisi baadaye.
Katika mwaka huo mmoja na ushee wa Magufuli, Chadema ambacho ukuaji wake umekuwa ukihusishwa na operesheni mbalimbali za kisiasa na mikutano ya hadhara, ambayo sasa imezuiwa kufanyika kikibaki kufanya mikutano ya ndani tu.
Mbowe na Zitto
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mbowe na Zitto walikuwa ni maswahiba wakubwa wakisiasa; Mwenyekiti huyo akielezwa kumpenda mwanasiasa huyo wa Kigoma pengine kuliko mwanasiasa mwingine yeyote chipukizi ndani yaChadema.
Ni Mbowe ndiye anayeelezwa kumtengeneza kisiasa Zitto kwa kumpa nafasi za juu kwenye chama angali kijana mdogo.
Hata hivyo, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, uhusiano wao ulianza kulegalega kwa sababu tofauti, ikiwamo hatua ya Zitto kutaka kuwania Uenyekiti wa Chadema, kwa kushindana na Mbowe.
Katika mojawapo ya mahojiano yake na vyombo vya habari, Zitto amewahi kukiri kwamba mojawapo ya makosa aliyowahi kuyafanya kisiasa na kuyajutia sana ni kitendo cha kutaka kuwania uenyekiti dhidi ya Mbowe.
Mgogoro huo pia unadaiwa kukolezwa na baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema waliokuwa wakitoa maneno ya uchonganishi kutoka kwa Mbowe na kwenda Zitto aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.
Hatimaye Zitto aliondoka Chadema kwa kuvuliwa uanachama na kwenda kuunda chama cha ACT-Wazalendo akiwa na wenzake Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo.
from Blogger http://ift.tt/2lnhEQt
via IFTTT
0 maoni:
Post a Comment