MAKONDA AMTISHA MWANDISHI WA HABARI ALIPOULIZWA KUHUSU KUTUMIA CHETI CHA MTU MWINGINE

Swali aliloulizwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kuhusu tuhuma zinazosambaa mitandaoni, kwamba anatumia cheti cha kidato cha nne cha mtu, zimeibua jambo jipya kuhusu tuhuma hizo.

Badala ya kujibu swali hilo, Makonda jana alitoa lugha ya vitisho kwa Mhariri wa Habari wa gazeti la JAMBOLeo, Exuperius Kachenje, akitumia simu ya mwandishi aliyemuuliza swali hilo, Salha Mohamed.

Awali gazeti la JAMBOLeo lilianza kufuatilia madai ya Makonda kukosa cheti cha kidato cha nne kutokana na hatua ambazo serikali ya Awamu ya Tano imeshazichukua dhidi ya watumishi wa umma wasiokuwa na vyeti hivyo ambao walishafukuzwa kazi na wako hatarini kupoteza mafao yao.

Ufuatiliaji

Katika jitihada za kusaka ukweli kuhusu madai hayo, gazeti la JAMBOLeo tangu wiki iliyopita lilizungumza na anayedaiwa kumpa cheti hicho Makonda, aliyejitambulisha kwa jina la Paul Pierre Christian. Gazeti hilo likapata taarifa za ziada kutoka katika chanzo chake, zilizoelezea madai ya ukaribu wa Makonda na Christian katika maisha ya ujana wao.

Jitihada ziliendelea kutafuta taarifa sahihi ambapo gazeti hilo lilikuwa katika mchakato wa kupata taarifa kutoka Shule ya Msingi Kilomije iliyopo Wilayani Kwimba, kujua jina sahihi la kwanza alilotumia Makonda alipokuwa akisoma shuleni hapo – ambalo INADAIWA SI PAUL.

Kabla ya kukamilika kwa mchakato huo, ndipo gazeti lilipata taarifa za kuwepo kwa mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa na Mkuu huyo wa Mkoa kuhusu kupatikana kwa eneo la kujengwa viwanda vidogo jijini humo. Kutokana na umuhimu wa taarifa hizo, Kachenje alimuelekeza Salha kutumia fursa hiyo kihabari kuzungumza pembeni na kiongozi huyo, ambapo katika hali ambayo haikutarajiwa, Makonda aliagiza simu ipigwe kwa Mhariri na kutoa kauli ambazo hazikutarajiwa.

Makonda

Makonda alimuagiza Salha kumpigia simu mtu aliyemtuma kuuliza swali hilo ambaye ni Kachenje ili ampe jibu mtu huyo badala ya mwandishi. Kupitia simu hiyo iliyopigwa saa 5:45 ambapo rekodi zinaonesha mazungumzo ya awali yalichukua sekunde 30 kisha akapiga tena saa 5:45 na kutumia sekunde 13, Makonda alihoji iwapo swali lililoulizwa kwake litasaidia kumtoa Mshauri ya Kampuni za Quality Group, Yusuf Manji katika kesi inayomkabili kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, Makonda alitumia simu hiyo ilipopigwa kwa mara ya pili kumtisha Mhariri huyo kwamba asisikie amemtisha mwandishi Salha.

Alipotakiwa kueleza zaidi tukio hilo, Kachenje alisema simu ya Salha ilipoingia kwake, hakuwaza jambo lolote zaidi ya kutarajia kupewa dondoo za awali za mkutano alioitisha Makonda, kwakuwa ndio utaratibu wa kawaida wa mwandishi, kumuarifu Mhariri kilichojiri katika utafutaji wa habari.

“Nilisikia sauti ya Salha ikisema, huyu hapa ongea naye, nikauliza ni nani, mwandishi akajibu RC. Kusikia hivyo nikamsalimu, badala ya kujibu salamu, akaanza kutoa maneno,” alisema Kachenje.

Sehemu ya mazungumzo ya Makonda na Mhariri huyo ni kama ifuatavyo:

Mhariri: Mheshimiwa habari?

Makonda: Unadhani majibu ya swali hili yatamtoa Manji kwenye kesi ya dawa za kulevya?

Mhariri: Mheshimiwa, hilo linakujaje?, sisi tunataka kujua kuhusu wewe.

Makonda: Nasema hivi, unadhani majibu ya swali hilo (kuhusu elimu yake) yatasaidia kumtoa Manji kwenye kesi ya dawa za kulevya? Huna akili wewe.

Alisema kisha akakata simu. Hata hivyo, sekunde chache baadaye alipiga tena simu na Mhariri alipotoka ufafanuzi zaidi, Makonda alisema, “Na nisikie unamtisha au kumnyanyasa huyu mwandishi (Salha), kisha akakata simu.

Katibu wa TEF

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Katibu wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena alisema alichofanya Makonda kinapingana na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kifungu cha 7. “Kifungu hicho kinaeleza majukumu ya kisheria kwa mwandishi wa habari kutafuta taarifa na hilo linafanyika ili kuujulisha umma, pili ni suala la weledi. Kama Mkuu wa Mkoa, Makonda alifuatwa na kuulizwa kuhusu taarifa kwamba hana cheti cha kidato cha nne, ambazo zimezagaa katika mtandao, hapo alipaswa kujibu tuhuma badala ya kumshambulia Mhariri wa Habari. Makonda asitufikishe mahali vyombo vya habari vikaacha kutuma waandishi kwenye mikutano yake. Itafika mahali tutawazuia na lazima niseme kuwa anakwenda kubaya. Asipambane na vyombo vya habari. Alitaja watu katika tuhuma, naye akitajwa asikilize na kujibu hoja,” alisema Meena.

Madai ya mtandaoni

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kulizagaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kwamba Makonda anatumia cheti cha mtu cha kidato cha nne. Taarifa hizo zinadai kuwa jina la kwanza analotumia Makonda ni la mtu mwingine anayetajwa kusoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Wavulana Tabora baada ya kufaulu vizuri kidato cha nne ambaye sasa ni mtangazaji katika redio moja ya jamii mkoani Tabora.

HT: JAMBOLeo

Jamaa atengeneza ndege YAFANIKIWA KURUKA

from Blogger http://ift.tt/2lELLmE
via IFTTT


Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

Post a Comment