MKAZI wa Mrito, kata ya Kemambo Nyamongo aliyefahamika kwa jina Chacha Magige (30) amehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kumkatakata kwa panga sehemu mbalimbali Mackrina Isaya.
Mtuhumiwa huyo alimkata Mackrina mikono yote miwili hadi kukatika kabisa na kusababisha kifo chake. Akisomewa hukumu hiyo katika kesi ya mauaji Mahakama Kuu yenye namba 181/2 /2017, Mei 5, mwaka huu katika kikao cha Mahakama Kuu kinachoendelea katika Mahakama wilayani ya Tarime mkoani Mara Jaji wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza, Joaquine De- Mello alidai kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na mwanasheria wa serikali, Harry Mbogoro.
Mwanasheria huyo wa serikali alidai kuwa mtuhumiwa Chacha Magige alitenda kosa hilo Julai 2, mwaka 2011 asubuhi katika Kijiji cha Mrito kwa kumshambulia kwa kumkatakata kwa panga Mackrina, mikono yote miwili na kukatika, alimshambulia kichwani na kumsababisha kifo, baada ya kumnyang’anya mwanamke huyo simu yake ya mkononi na Sh 1,000,000.
Katika mashitaka hayo mtuhumiwa alikiri kumuua mwanamke huyo na kudai kuwa ilikuwa ni hasira za kumdai shilingi 10,000,000 alizodai alimpa amhifadhie na kwamba walikuwa na mahusiano ya karibu na Mackrian na kuiomba mahakama hiyo kumuadhibu kwa kuua bila kukusudia.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali Mbogoro alipinga utetezi huo na kudai kuwa mtuhumiwa alikuwa na nia ya kuua kwani Mackrina alikutwa na majeraha manne makubwa ya kukatwa mikono yote miwili, jeraha kubwa ubavuni na kichwani.
Jaji Joaquine akitoa hukumu alikubaliana na maelezo ya mwanasheria wa serikali na kumtia hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia. Mtuhumiwa baada ya hukumu hiyo aliomba maji ya kunywa.
0 maoni:
Post a Comment