Kiburi cha kocha, Ndayiragije , kimezidi kuongezeka mara baada ya kukiongoza vyema kikosi cha Mbao na kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuwasukumiza nje ya mashindano mabingwa watetezi Yanga SC katika hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa goli 1 kwa 0.
Ndayiragije, amesema mkataba wake unamzuia kuanza kufikiria kujiunga na timu nyingine ambazo zinatajwa kumuwania.
Leo Jumamosi kocha huyo ataiongoza Mbao kucheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Ndayiragije ambaye aliwahi kuinoa Vital’O ya nchini kwao, ameyasema hayo huku kukiwa na tetesi kwamba anatakiwa kwenda kuchukua mikoba ya Mmalawi, Kinnah Phiri ya kukinoa kikosi cha Mbeya City.
Mrundi huyo amesema kuwa, kutokana na mkataba wake alioingia na Mbao, unamnyima nafasi ya kuanza kupigia hesabu timu nyingine.
“Si kweli kama nataka kwenda Mbeya City, mimi ni kocha wa Mbao na watu wanatakiwa kulitambua hilo kwamba sina mpango wa kuondoka sasa hivi.
“Mkataba wangu na Mbao unanizuia kuanza kufikiria kujiunga na timu nyingine, inawezekana ipo timu inayonihitaji lakini binafsi sina taarifa hizo na sijafanya mazungumzo na timu nyingine,” alisema Ndayiragije.
Ikumbukwe kuwa, kocha huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja ambao unaisha hivi karibuni, lakini mwenyewe amesisitiza kuna makubaliano ambayo aliingia na mabosi wake. Makubaliano hayo alidai ni siri yao.
0 maoni:
Post a Comment