Klabu ya soka ya wekundu wa
msimbazi ya simba imetwaa ubingwa wa kombe la shirikisho la TFF baada ya
jioni ya leo kuinyuka Mbao FC bao 2-1 kwenye mechi ya fainali
iliyopigwa kunako dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.
Wachezaji wa Simba wakishangilia kombe lao
Katika
fainali hiyo iliyokuwa na ushindani wa hali ya juu, timu zote mbili
zimepata mabao haoyo katika 30 zilizoongezwa kufuatia dakika 90 za
kawaida kumalizika kwa timu zote kutoka nguvu sawa pasipo kufungana.
Alikuwa mshambuliaji wa kimataifa wa
Simba Fredrick Blagnon aliyeifungia Simba bao la kwanza dakika ya
108 kabla ya Mbao kusawazisha kupitia Robert Ndaki dakika ya 108 zikiwa
zimesalia dakika 12 mchezo kuelekea katika changamoto za mikwaju ya
penati.
bao hilo la Mbao lilitokana na
mabadiliko ambayo kocha wake aliyafanya katika dakika za mwisho kwa
kuwaingiza Rakesh Kotecha na Robert Ndaki wakati Mbao ikiwa nyuma, na
kuiwezesha kuongeza mashambulizi ya nguvu langoni mwa Simba hadi bao
hilo lilipopatikana na uzembe wa mabeki wa Simba waliodhani mfungaji
ameotea, na kumuacha pekee yeye na golikipa Dan Agyei.
Ramadhani Shiza Kichuya akafunga bao la
pili na la ushindi kwa Simba kwa penati baada ya mwamuzi kuamua adhabu
hiyo iliyozua utata kwa madai kuwa beki wa Mbao aliunawa mpira kwenye
eneo la hatari.
Wachezaji wa Mbao walitaka kuigomea
penati hiyo huku wakimzonga mwamuzi na kusababisha purukushani iliyodumu
kwa takriban dakika 2, na kisha penati hiyo kupigwa katika dakika ya
120, ambapo hadi kipyenga cha mwisho, Simba 2, Mbao 1.
James Kotei wa Simba ameibuka mchezaji
bora wa mchezo wa leo ambapo alionesha uwezo mkubwa katika safu ya
ulinzi ya Simba kwa kudhibiti vilivyo kasi ya washambuliaji wa Mbao FC,
huku Obrey Chirwa akiibuka mfungaji Bora wa michuano hiyo.
Mchezaji Bora wa Ligi Kuu msimu huu
Mohamed Hussein alilazimika kutolewa nje mwanzoni kabisa mwa kipindi cha
pili kutokana na maumivu aliyoyapata ambapo nafasi yake ilizibwa
vilivyo na Abdi Banda
Kwa ushindi huo Simba imejinyakulia
milioni 50 na kujikatia tiketi ya kucheza kunako michuano ya Kombe la
Shirikisho barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu msimu wa mwaka
2012/13, huku mshindi wa pili akiambulia patupu zaidi ya medali kwa kuwa
hakuna zawadi ya fedha kwa mshindi wa pili wa michuano hiyo.
Simba wakishangilia mfano wa hundi ya shilingi milioni 50
Simba baada ya kukabidhiwa medali zao
0 maoni:
Post a Comment