WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za
kulevya kwenda nchi za nje hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika
mipaka yote.
Amesema
kunatabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama
njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za Afrika
ya Kusini, Malawi na Zambia.
Alitoa
kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Julai 29, 2017) alipozungumza na
watumishi wa kituo cha forodha cha Kasumulu kilicho katika mpaka wa
Tanzania na Malawi wilayani Kyela.
Waziri
Mkuu alisema ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi
wa watu wanaopita kwenye maeneo hayo pamoja na mizigo
ukaimarishwa.“Endeleeni kufanya upekuzi wa kina wa magari, watu na
mizigo yote yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo lango la kupitishia
dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na jambo hilo.”
Pia
aliwataka viongozi hao kuhakikisha biashara zote za magendo
zinazifanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa
kuwa zinaikosesha Serikali mapato.
Alisema
ni vema yakawepo maduka ya kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili
kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku
Serikali ikikosa kodi.“Biashara za magendo zidhibitiwe katika maeneo
haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili biashara hiyo
ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato.”
Pia
Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani
kuhakikisha wanadhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la
kuimarisha ulinzi nchini.
Waziri
Mkuu alisema katika baadhi ya maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha
ambazo hapo awali hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika
matukio ya kihalifu.Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye ni Afisa Mfawidhi
wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi katika
kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo.
Alisema
mbali na kupambana na biashara za magendo pia watadhibiti uingiaji wa
wahamiaji haramu kwa kushirikiana na watumishi idara zote waliopo katika
mpaka huo wa Kasumulu.Bw. Magwaza alisema katika doria zilizofanywa
mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na kuchukuliwa
hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema
wahamiaji hao walitokea nchi za Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6)
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa
makwao na wengine walifungwa katika Gereza la mkoa wa Mbeya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 30, 2017
0 maoni:
Post a Comment